Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, Ispecta Jumanne Malangahe ameileza Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake watatu namna alivyoshirikiana na Inspecta Mahita kuwakamata watuhumiwa wa ugaidi Adam Kasekwa na Mohamed Ling’enywa.
Akitoa ushahidi wake mahakamani hapo mbele ya Jaji Joachim Tiganga shahidi huyo amedai, Agost 4 mwaka 2020 akiwa ofisini kwake majira ya jioni alipigwa simu na ACP Ramadhani Kingai akimtaka ajiandae na safari kwenda Moshi mkoani Kilimanjaro kuna kazi ya kwenda kufanya.
Wakiwa Ofisini hapo ACP Kingai alitoa muhtasari juu ya kuwepo kwa kikundi cha kihalifu ambacho kinadaiwa kuratibiwa na Freeman Mbowe kufanya matukio ya kihalifu kwakulipua vituo vya mafuta, kuanzisha vurugu na maandamano, kukata magogo na kuweka barabarani ili kuzuia magari kupita na kudhuru viongozi wa Serikali akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.
Hivyo wakaagizwa waende Moshi eneo la Rau Madukani ambapo watuhumiwa wanadaiwa kuonekana ili kuzia uhalifu huo usitendeke na kuwakamata wahalifu hao.
Baada ya kupokea malekezo hayo waliondoka pamoja na ACP Kingai na askari wengine akiwemo Mahita Omari Mahita, Afande Aziz na Francis kwenda eneo la Rau Madukani katika Moja ya Grosari iliyopo Rau ili kukamata wahalifu muda saa 7 mchana.
Aidha, amedai kwamba baada ya watuhumiwa wawili Adam Kasekwa na Ling’enywa kukamatwa, mtu wa tatu ambaye ni Moses Lujenje alitoweka kusikojulikana na mpaka sasa hajulikani alipo ACP Kingai aliwaeleza kwamba wanatuhumiwa kwa kula njama ya kutenda vitendo vya Kigaidi.
Amedai kwamba wakiwa pale na watuhumiwa hao ACP Kingai alimuamuru watuhumiwa wafanyiwe upekuzi lakini kabla mashuhuda wengine wenyeji wa eneo hilo Anitha Mtaro na Ester Nduhulu waliombwa kushuhudia upekuzi huo.
Wakati wa upekuzi huo shahidi huyo amedai kumkuta mshitakiwa wa pili, Adam Kasekwa akiwa na bastola yenye risasi tatu, simu ndogo aina ya Itel, laini za simu Kampuni ya Airtel na Vodacom na kete 58 za dawa za kulevya huku mshitakiwa wa tatu, Mohamed Ling’enywa akikutwa na simu kubwa aina ya Tekno, laini mbili za simu kampuni ya Airtel.