Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

#KESIYAMBOWE:Panda shuka siku 93 za ushahidi

Mbowe Kesipic Panda shuka siku 93 za ushahidi

Thu, 2 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu, wanaotuhumiwa kwa makosa ya ugaidi, imesimama kwa muda kusubiri uamuzi wa kesi ndogo ndani ya kesi hiyo ya msingi, unaotarajiwa kutolewa Desemba 14, 2021.

Kesi hiyo ndogo inatokana na maelezo yanayobishaniwa na mawakili wa pande zote, yaani upande wa mashtaka na upande wa utetezi.

Wakati upande wa mashtaka unadai kuwa maelezo hayo yalitolewa na mshtakiwa wa tatu, Mohamed Abdillahi Ling'wenya katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, wakati akihojiwa na mmoja wa maafisa wa Polisi waliowakamata mjini Moshi na kuwasafirisha hadi Dar.

Lakini mshtakiwa huyo kupitia kwa mawakili wake amepinga kuwa hajawahi kufikishwa kituoni hapo bali alifikishwa kituo cha Polisi Tazara na kwamba hakuwahi kutoa maelezo hayo bali alipewa tu nakala ya maelezo yaliyokuwa yameshaandaliwa akiwa katika kituo cha Polisi Mbweni na akalazimishwa kuyasaini bila kuruhusiwa kuyasoma huku akitishiwa.

Baada ya Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kusikiliza ushahidi wa pande zote katika kesi hiyo ndogo, jana ilipanga kutoa uamuzi wake Desemba 14.

Mpaka sasa kesi hiyo imeshachukua muda wa siku 93, tangu ilipoanza kusikilizwa kwa mara ya kwanza Agosti 31, 2021.

Katika kesi ya msingi jumla ya mashahidi wanane wa upande wa mashtaka wameshasimama kizimbani na kutoa ushahidi wao.

Mashahidi Saba kati yao wakiwa wameshakamilisha ushahidi wao na shahidi wa nane akiwa bado hajakamilisha baada ya kesi hiyo ya msingi kusimama kusubiri kumalizika kwa hiyo kesi ndogo.

Kesi hiyo ndogo iliibuka baada ya shahidi huyo wa nane kuiomba mahakama hiyo iyapokee maelezo yanayodaiwa kuwa ya mshtakiwa wa tatu yawe kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka na mawakili wa utetezi kuyapinga.

Mashahidi hao ambao wameshatoa ushahidi na ushahidi wao kwa ufupi ni pamoja na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni (RPC), Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Ramadhani Kingai ambaye ndiye aliyefungua pazia la mashahidi hao wa upande wa mashtaka.

Mbowe na wenzake wanakabiliwa na kesi ya uhujumu Uchumi namba 16/2021 yenye mashtaka sita yakiwemo ya kula njama na kufadhili vitendo vya kigaidi, vinavyodaiwa kuwa vikilenga kuleta hofu katika jamii ya Wananchi wa Tanzania.

Vitendo hivyo ni pamoja na kutaka kulipua vituo vya mafuta, maeneo ya mikusanyiko ya watu, kuzuia barabara kwa miti na magogo na kutaka kumdhuru aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo Agosti ,2020 katika maeneo ya Moshi, Arusha na Dar es salaam.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live