Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KESI YA MAUAJI: Ushahidi ‘tata’ waweka huru watuhumiwa

99031 Pic+mauaji KESI YA MAUAJI: Ushahidi ‘tata’ waweka huru watuhumiwa

Mon, 16 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Mahakama kuu kanda ya Dodoma imewaachia huru washtakiwa wawili waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji yaliyotokea miaka minne iliyopita.

Washtakiwa hao Selemani Mwalimu na Mateso Isaya waliachiwa huru baada ya mashahidi kushindwa kutoa ushahidi wa kuwatia hatiani.

Akitoa hukumu hiyo jana, Jaji mfawidhi wa mahakama hiyo, Mustapher Siyani alisema baada ya kusikiliza ushahidi wa upande mashtaka na utetezi ameona kuwa washtakiwa hao hawana hatia dhidi ya kesi ya mauaji ya Kalasa Budala.

Washtakiwa hao wakazi wa Kijiji cha Chifutuka wilayani Bahi mkoa wa Dodoma, walidaiwa kumuua kwa kumchinja na msumeno Bundala na kumkata sehemu zake za siri Machi 16, 2016.

Jaji Siyani alisema upande wa Jamhuri umeshindwa kutoa ushahidi wa kuwatia hatiani washtakiwa hao, ingawa ni kweli Bundala aliuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na kukatwa sehemu zake za siri.

Alisema haikuonyesha kwamba mshtakiwa wa kwanza alichukuliwa maelezo ya onyo au kukiri kutenda kosa mbele ya mlinzi wa amani kwa kuwa maelezo hayo hayakupelekwa mahakamani.

Pia Soma

Advertisement
Pia alisema shahidi wa pili na wa nne wa Jamhuri walidai waliwaona washtakiwa wakimchinja Bundala kwa kutumia msumeno na kumkata sehemu za siri, hawakutoa maelezo hayo mahali popote hata polisi, bali waliyatoa kwa mara ya kwanza mahakamani.

“Kwa mahakama makini haiwezi kuupokea ushahidi huo kwa kuwa si salama na hauaminiki kwa sababu kama kweli mashahidi waliwatambua washtakiwa wangetoa taarifa mapema hata kwa polisi, ili wakamatwe lakini walinyamaza kimya mpaka walipokuja hapa mahakamani.

“Mahakama haiwezi kuupokea ushahidi wao kwa kuwa haujaungwa mkono na shahidi mwingine yeyote,” alisema Jaji Siyani.

Alisema pia mashahidi wengine walishindwa kupeleka vitu vilivyotumika kufanyia mauaji hayo ikiwemo jiwe na msumeno ambavyo ni ushahidi muhimu katika kesi hiyo.

Pia, alisema maelezo ya onyo na ya ungamo kwa mlinzi wa amani yanaonekana hayakutolewa kwa hiari yao, hivyo ushahidi huo haukupokelewa.

Washtakiwa hao walikuwa wanatetewa na mawakili wawili ambao ni Hubert Lubyama na Fred Kalonga huku upande wa Serikali ukiwakilishwa na mwanasheria, Judith Mwakyusa.

Chanzo: mwananchi.co.tz