Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KESI YA KINA KITILYA: Shahidi aibua utata kumtaja Shose

66997 Kitilya+pic

Tue, 16 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Shahidi wa nne upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili, Harry Kitilya na wenzake ameibua utata baada ya kumtaja mshtakiwa wa pili, Shoshe Sinare kuwa ndiye aliyewasilisha barua ya pendekezo la mkopo kwa Serikali kutoka benki ya Standard.

Shahidi huyo, Amisa Nyambi ambaye ni msaidizi wa mtendaji mkuu wa Idara ya Sera Wizara ya Fedha na Mipango alitoa ushahidi wake jana mahakamani akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Oswald Tibabyekomya.

Aliieleza Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kuwa mwaka 2012 alikuwa mwandishi mwendesha ofisi Idara ya Sera.

Alisema majukumu yake yalikuwa kupokea barua mbalimbali zilizokuwa zinaingia ofisini hapo na kwamba Juni 26, 2012 alipokea barua ya mapendekezo ya uwezeshaji wa mkopo kwa Serikali ikitoka Benki ya Standard.

Wakati akihojiwa na Wakili Majura Magafu anayemtetea Kitilya, shahidi huyo alidai kuwa barua hiyo iliwasilishwa na Shose ambaye alisema kuwa alikuwa anamjua kwa sababu alikuwa akifika ofisini hapo mara kwa mara, na kwamba siku hiyo alifika na mtu mwingine ambaye hamkumbuki jina lake.

Wakati akihojiwa na mmoja wa mawakili wa Shose, Zaharani Sinare, shahidi huyo alisema atakuwa tayari kubadili kauli yake hiyo kuwa Shose ndiye aliwasilisha barua hiyo iwapo atapewa ushahidi kuwa tarehe hiyo aliyoitaja, Shose hakuwepo nchini.

Pia Soma

Majibu hayo yalimfanya Wakili Sinare aombe hati ya kusafiria ya Shose ambayo alidai inashikiliwa ili kuonyesha kuwa tarehe hiyo hakuwepo nchini.

Lakini kiongozi wa jopo la mawakili wa Serikali, Tibabyekomya alijibu kuwa wao hawana na wala hawajui inashikiliwa na mamlaka gani.

Kutokana majibu hayo ya upande wa mashtaka, Jaji Immaculata Banzi anayesikiliza kesi hiyo aliomba mwongozo kwa wakili Sinare.

Jaji Banzi alimuuliza wakili Sinare katika mazingira hayo ambapo haijulikani hati hiyo inashikiliwa na mamlaka gani, atakuwa tayari kusimamisha usikilizwaji wa kesi hiyo hadi hati ipatikane au anaweza kuendelea wakati hati hiyo ikitafutwa ili aitumie wakati mwingine?

Baada ya kujadiliana na mawakili wenzake, wakili Sinare aliieleza mahakama kuwa hati hiyo inashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kwamba, wamekubaliana kuendelea kumhoji maswali shahidi huyo na hati hiyo wataitumia wakati mwingine ikipatikana.

Mbali na Kitilya ambaye alikuwa mkurugenzi wa Kampuni ya Enterprise Growth Market Advisors Limited (Egma) na Shose washtakiwa wengine ni Sioi Solomon, Bedason Shallanda na Alfred Misana.

Solomoni na Shose walikuwa ni maofisa wa benki ya Stanbic. Shose akiwa mkuu wa kitengo cha wateja wakubwa na uwekezaji na Sioi akiwa mwanasheria wa benki hiyo.

Shallanda na Misana walikuwa watumishi wa Serikali katika Wizara ya Fedha.

Washtakiwa wote wanakabiliwa na mashtaka 58, yakiwamo ya kuisababishia Serikali hasara ya Dola 6 milioni na kujipatia fedha kiasi hicho kwa njia za udanganyifu na utakatishaji fedha kiasi hicho, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uwongo, kuongoza uhalifu na kumdanganya mwajiri.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Februari 2012 na Juni 2015 jijini Dar es Salaam na nje ya nchi wakati wa mchakato kuiwezesha Serikali kupata mkopo wa Dola za Marekeni 550 milioni kutoka Benki ya Standard ya nchini Uingereza na Stanbic Tanzania .

Serikali inadai kuwa washtakiwa hao walishirikiana kupanga uhalifu kwa kughushi barua Standard Bank na Stanbic, kuonyesha kwamba zilikuwa zimefanya marekebisho katika vigezo na masharti hususan ada ya uwezeshaji wa mkopo huo kutoka asilimia 1.4 hadi asimilia 2.4 ya mkopo halisi.

Chanzo: mwananchi.co.tz