Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KESI YA KINA KITILYA: Nyaraka muhimu kesi ya kina Kitilya njiapanda

67492 PIC+KITILYA

Fri, 19 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Nyaraka muhimu katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili mkurugenzi wa kampuni ya ushauri wa uwekezaji, huduma za uwezeshaji na upatikanaji wa fedha ya Enterprise Growth Market Advisors Limited (Egma), Harry Kitilya na wenzake wanne ziko njiapanda baada ya kupingwa na mawakili wa utetezi zisipokewe mahakamani.

Mawakili hao wa washtakiwa wameweka pingamizi ili mahakama isizipokee nyaraka hizo na kuwa sehemu ya ushahidi wa upande wa mashtaka, pamoja na mambo mengine wakidai kuwa hazina uhusiano katika kesi hiyo.

Pingamizi hilo liliibua mvutano mkali wa kisheria baina ya mawakili wa pande zote mbili baada ya upande wa mashtaka nao kupinga hoja za mawakili wa utetezi kuwa hoja za pingamizi lao hazina mashiko ya kisheria.

Nyaraka hizo ni zile zinazohusu mchakato wa mkopo wa Dola za Marekani 600 milioni uliotolewa na Benki ya Standard ya Uingereza kwa kushirikiana na Stanbic Tanzania mwaka 2013, ambazo ndizo kiini cha kesi hiyo.

Upande wa mashtaka uliomba kuwasilisha mahakamani nyaraka hizo ili ziwe sehemu ya ushahidi wake kupitia kwa shahidi wa saba wa mashtaka ambaye ni shahidi wa nyongeza, Deodata Makani.

Shahidi huyo, ambaye awali hakuwa katika orodha ya mashahidi wa upande wa mashtaka aliombwa kuongezwa na upande huo, ukidai kuwa ni shahidi wao muhimu kulingana na nyaraka ambazo yeye ndiye anayeweza kuziwasilisha mahakamani.

Habari zinazohusiana na hii

Mbali na Kitilya, ambaye aliwahi kuwa kamishna mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni waliokuwa maofisa wa Stanbic, Shose Sinare na Sioi Solomon.

Wengine ni waliokuwa watumishi Wizara ya Fedha, Bedason Shallanda na Alfred Misana.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 58 yakiwemo ya kuisababishia Serikali hasara ya kiasi cha Dola 6 milioni, kujipatia fedha kiasi hicho kwa njia za udanganyifu na utakatishaji fedha kiasi hicho, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uwongo, kuongoza uhalifu na kumdanganya mwajiri.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Februari 2012 na Juni 2015 katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam na nje ya nchi wakati wa mchakato wa kuiwezesha Serikali kupata mkopo wa Dola za Marekeni 550 milioni kutoka Benki ya Standard ya Uingireza.

Kesi hiyo inasikilizwa na Jaji Immaculata Banzi katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Wakati akitoa ushahidi jana, Makani ambaye ni mkurugenzi wa utawala na raslimali watu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee, Watoto na Jinsia alieleza mahakama kuwa mwaka 2011 hadi 2016 alikuwa akifanya kazi Wizara ya Fedha na Uchumi akiwa na wadhifa huo.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Oswald Tibabyekomya, shahidi huyo alieleza kuwa miongoni mwa majukumu yake ni kutunza kumbukumbu zote za wizara zikiwemo nyaraka mbalimbali.

Alieleza kuwa mwaka Novemba 4, 2015 alipokea jalada kutoka kwa katibu mkuu likiwa na barua ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ikiomba nyaraka mbalimbali kuhusu mchakato wa mkopo huo na baadhi zilipatikana na akaziwasilisha Takukuru.

Shahidi huyo alizitaja nyaraka hizo kuwa ni pamoja na muhtasari wa kikao cha Kamati ya Taifa ya Usimamizi wa Madeni (NDMC) ambayo ina jukumu la kumshauri Waziri wa Fedha kuhusu masuala yote ya ukopaji ndani na nje ya nchi.

Nyingine ni makubaliano ya benki ya Standard na Stanbic katika kuiwesha Serikali kupata mkopo huo, ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na maelekezo ya aliyekuwa Waziri wa Fedha wakati huo, Dk William Mgimwa.

Baada ya kumaliza kuzitaja nyaraka hizo, shahidi huyo aliiomba mahakama hiyo izipokee ziwe sehemu ya ushahidi wa upande wa mashtaka, lakini mmoja wa mawakili wa Kitilya, Majura Magafu aliweka pingamizi akiungwa mkono na mashahidi wengine wa utetezi.

Pamoja na mambao mengine Wakili Magafu alidai kuwa nyaraka hizo hazihusiani kwa kuwa kile kile shahidi huyo alichokieleza katika msingi wake wa kuwasilisha nyaraka hizo ni kinyume na kile alichokiwasilisha.

Wakili Magafu alidai kuwa Takukuru pamoja na nyaraka nyingine waliomba majalada mawili na kwamba shahidi huyo katika barua yake ya majibu kwa Takukuru akielezea nyaraka alizoziwasilisha ameyataja majalada hayo na wakati akitoa ushahidi kizimbani alitaja majalada.

Alidai kuwa badala ya kuwasilisha majalada, yeye amewasilisha nyaraka mbalimbali ambazo hawajui na hakuna uhakika kama zimetolewa katika majalada yaliyotajwa kwenye barua ya Takukuru. Alidai kuwa kutokana na hali hiyo nyaraka hizo hazina uhusiano na ushahidi wa shahidi huyo, si halisi, haziaminiki na yeye anakosa mamlaka ya kuziwasilisha mahakamani.

Wakijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Awamu Mbagwa na Tibabyekomya walidai hoja za pingamizi la utetezi hazina mashiko kisheria na wakaiomba mahakama hiyo upilie mbali.

Jaji Banzi aliahirisha kesi hiyo hadi leo atakapotoa uamuzi.

Chanzo: mwananchi.co.tz