Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KESI YA KIHIYO: Lamwai aomba Kihiyo ahukumiwe miaka 21 jela-11

90169 Uchaguzipic KESI YA KIHIYO: Lamwai aomba Kihiyo ahukumiwe miaka 21 jela-11

Mon, 30 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Akiithibitishia mahakama hiyo, Clement Kato (47) alisema kuwa namba ya U1 iliyoko kwenye cheti cha Kihiyo ni sawa na ya vyeti vingine vilivyotolewa chuoni hapo kwani ni namba ya kituo cha kufanyia mtihani.

Alisema pia kwamba namba ya mtahiniwa 251 iliyoko kwenye cheti cha Kihiyo ilikuwa inaonyesha jina la Peter R. Mwaria katika orodha ya majina ya watahiniwa wa mwaka 1986 iliyoko katika chuo hicho.

Katika ushahidi wake, Kato aliiambia mahakama kuwa vyeti vyote vya waliohitimu mwaka 1986 vilitolewa siku moja ambayo ni Mei 15, 1986, hivyo ni tofauti na cheti cha Kihiyo ambacho kinaonyesha kilitolewa Mei 14, mwaka huo, na hivyo kuwa ni tofauti ya siku moja ya vyeti vilivyotolewa na Baraza la Mitihani.

Aliieleza mahakama kuwa ni wanafunzi watatu tu ambao walimaliza kozi yao mwaka 1986 ambao hawajachukua vyeti vyao kutoka BMT na kwamba kufuatana na utaratibu wa maandishi ya BMT, tarehe iliyoko katika vyeti vilivyotolewa ilikuwa ina mkato / katikati ya mwezi Mei na mwaka 1986 lakini cheti cha Kihiyo kilikuwa hakina mkato.

Kato pia aliieleza mahakama kuwa sahihi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu katika vyeti hivyo ilikuwa haishikamani na neno la Katibu Mkuu kama ilivyokuwa ikionyesha katika cheti cha Kihiyo.

Wakili Ndyanabo aliyekuwa anamtetea Tambwe Hiza alitaka kujua kama chuo hicho cha ufundi kilikuwa kinachukua wanafunzi kutoka shule za sekondari za kawaida kama vile Azania ambayo Kihiyo alidai alihitimu kidato cha nne na kwenda chuoni hapo.

Ndyanabo: Hivi chuo chenu kinachukua wanafunzi kutoka shule za kawaida kama Azania?

Kato: Miaka ya nyuma tulikuwa hatupokei wanafunzi kutoka shule ambazo zilikuwa si za ufundi.

Ndyanabo: Je, mwaka 1984?

Kato: Mwaka 1984 tulikuwa hatupokei wanafunzi kutoka shule zisizo za ufundi bali kwa miaka mitatu iliyopita.

Jaji Mapigano aliahirisha kesi hiyo hadi Jumanne ya Juni 4, 1996, siku ambayo hoja kuhusu kesi hiyo zingeanza kutolewa kabla Jaji Mapigano kupanga siku ya hukumu.

Wakati hayo yakiendelea, iliripotiwa kuwa Kihiyo alikuwa akijifungia tu chumbani kwake muda wote tangu Mei 28 alipojiuzulu wadhifa wake siku chache zilizokuwa zimepita kwa kile alichosema ni sababu za kiafya.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, majirani wa Kihiyo ambaye kwa wakati huo alikuwa anaishi Temeke, karibu na Kituo cha Polisi Chang’ombe, walidai kwamba tangu alipotoka mahakamani Alhamisi jioni, hakuonekana tena barazani wala ukumbini kwa siku kadhaa.

Majirani hao walidai kwamba awali Kihiyo katika harakati za kutafuta vielelezo vya kesi hiyo alikuwa akionekana sehemu nyingi ikiwa ni pamoja na mitaani na baa saa za jioni.

Ingawa tayari alikuwa ameshajiuzulu, kesi hiyo iliendelea tena Juni 4 ambapo wakili wa Serikali, Julius Malaba, aliomba muda zaidi wa kujiandaa kwa ajili ya kutoa maelezo. Jaji Mapigano aliahirisha kesi hiyo kwa siku moja.

Hata hivyo, baada ya mawakili kuwasilisha maelezo yao, hukumu ya kesi hiyo ilipangwa kutolewa Julai 25, 1996. Hii ni baada ya wakili Lamwai kumalizia kutoa maelezo yake na kumwomba Jaji amhukumu Kihiyo kifungo cha miaka 21 kwa kuidanganya mahakama.

Lamwai alimwomba Jaji Dan Mapigano amtie hatiani Kihiyo kwa kosa la kusema uongo chini ya kiapo cha kifungu 104 cha sheria ya makosa ya jinai na kwa kuwa uongo huo umemsaidia kuingia bungeni, aliomba amhukumu adhabu ya juu kiasi ambayo ni kifungo cha miaka saba jela.

Wakili huyo alimwomba Jaji amhukumu mshtakiwa jela miaka saba ikiwa ni adhabu ya juu kabisa kwa kosa la kutoa cheti cha uongo mahakamani kama kielelezo chini ya kifungu cha sheria ya makosa ya jinai cha 342 cha kutoa hati ya uongo.

Alimwomba pia Jaji amtie hatiani Kihiyo kwa kutoa maelezo ya uongo katika karatasi ya kuteuliwa ubunge na ampe adhabu ya juu ya kifungo cha miaka saba jela.

“Huyu ni mtu ambaye kama (Rais Benjamin) Mkapa angeteleza kidogo tu angekuwa waziri,” alisema Dk Lamwai.

Mahakama hiyo iliombwa pia itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu waelewe mahakama na vyombo vyote vya sheria haviendeshwi kitapeli, hivyo watu wasije mahakamani na kutoa vyeti vya uongo na liwe fundisho kwa wale wote wenye vyeti vya kughushi.

Awali kabla ya kuomba adhabu hizo, Lamwai aliieleza mahakama kuwa cheti kilichowasilishwa mahakamani hapo na Kihiyo kilikuwa kimeghushiwa kwa hali ya juu na kwamba licha ya Jaji kumtaka Kihiyo aieleze mahakama ukweli kuhusu elimu yake, yeye kwa macho makavu kabisa alidai kuwa alisoma Chuo cha Ufundi cha Dar es Salaam.

Jaji Mapigano alimweleza Lamwai kuwa iwapo Kihiyo atatiwa hatiani suala la kumwadhibu ni pana sana kwani kughushi kwake cheti hicho kunaweza kukagusa Mamlaka ya Maji Mjini (Nuwa), Baraza la Mitihani la Taifa na Chuo cha Ufundi Dar es Salaam.

Jaji alimwambia Dk Lamwai kuwa kuliko yeye amhukumu mshitakiwa halafu hao wengine waje wahangaike ni bora ashtakiwe kwa makosa hayo yote pamoja na kupata hukumu, lakini alikubali kuwa anao uwezo wa kutoa hukumu hizo kama ilivyopendekezwa na Wakili Lamwai.

Lamwai alimweleza Jaji Mapigano kuwa kosa la kutoa ushahidi wa uongo chini ya kiapo na kutoa cheti cha uongo kama kielelezo yalifanyika mbele ya Jaji na anaamini na aliamini Jaji anao uwezo wa kuyatolea uamuzi na kwamba kosa la kughushi DPP anaweza akamshtaki Kihiyo katika mahakama ndogo kama ya Kisutu.

Lamwai aliiomba mahakama itoe amri kwa Kihiyo kulipa gharama za kesi hiyo na asiruhusiwe kugombea ubunge kwenye uchaguzi ujao, na pia alisema dai kubwa walilokuwa wanalitaka lilishatimizwa kutokana na kujiuzulu kwa Kihiyo Mei 28.

Lamwai pia aliieleza mahakama kuwa kitendo cha Kihiyo kumkataza wakili wake, William Erio, kuendelea na kesi ni kwamba anakubaliana na walalamikaji kuwa yote waliyoyasema ni kweli na hana jinsi ya kuyakataa.

Wakili huyo alitoa mfano wa suala la rushwa na kusema kuwa hilo ni kosa kubwa iwapo jaji ataona limefanyika na hata DPP anaweza kukubali kutendeka kwa kosa hilo.

Lamwai alisema hata katika barua ya Kihiyo ya kujiuzulu, Kihiyo alishindwa kusema ukweli kwani alidai kuwa alijiuzulu kwa matatizo ya afya wakati kila siku alikuwa akionekana mahakamani na kwamba angeweza kusema ukweli kuwa anajiuzulu kwa sababu ya kusema uongo na alishasema uongo sana mahakamani.

“Bwana Kihiyo alianza kudanganya siku alipojaza fomu ya kugombea ubunge hadi siku alipojiuzulu,” alisema Lamwai na kuisisitizia mahakama kuwa mashahidi wote walioletwa na mahakama walikuwa watuhumiwa na kwa vyovyote walikuja kukanusha kulinda maslahi yao.

Chanzo: mwananchi.co.tz