Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KESI MAUAJI YA LIBERATUS BARLOW: Mtaalamu aeleza alivyooanisha risasi, bunduki

16085 Pic+kesi TanzaniaWeb

Fri, 7 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Shahidi wa 19 katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow ameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza namna alivyotumia ujuzi na utaalamu wake kuoanisha maganda ya risasi yaliyookotwa eneo tukio na bunduki inayodaiwa kutumika kwenye mauaji hayo.

Akiongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Robert Kidandu kutoa ushahidi mbele ya Jaji Sirilius Matupa, shahidi huyo ambaye ni mkaguzi wa Polisi, Gilbert Lukaka aliiambia Mahakama kuwa alichunguza na kuoanisha maganda ya risasi na bunduki hiyo Juni 12, 2012 baada ya kukabidhiwa jukumu hilo na wakuu wake wa kazi.

Shahidi huyo ni mtaalamu wa uchunguzi wa bunduki na milipuko kutoka Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam.

Ifuatayo ni sehemu ya maswali na majibu ya shahidi huyo katika shauri la mauaji namba 192/2014 linalowakabili washtakiwa saba;

Wakili: Unafanya kazi gani?

Shahidi: Mimi ni askari polisi Dar es Salaam kitengo cha uchunguzi wa silaha za uhalifu na milipuko.

Wakili: Kwenye uchunguzi huo unachunguza nini hasa?

Shahidi: Nachunguza risasi, bunduki na maganda yaliyofanyiwa uhalifu.

Wakili: Umepata wapi utaalamu huo?

Shahidi: Nilipata mafunzo ya utaalamau huo kwa nyakati tofauti katika nchi za Marekani, Uturuki na Australia.

Wakili: Unakumbuka tarehe 6/12/2012 ulikuwa wapi?

Shahidi: Nilikuwa ofisini makao makuu ya polisi Dar es Salaam nilipokea barua kutoka kwa kiongozi wangu WP 5127 Ditektivu Salama.

Wakili: Barua ilitoka wapi na litaka ufanye nini?

Shahidi: Barua ile ilitoka kwa mkuu wa upelelezi Mkoa wa Mwanza niliifungua nikaisoma mle ndani kulikuwa na vilelezo vitatu.

Wakili: Ni vielezo gani hivyo? Ebu vitaje mbele ya mahakama.

Shahidi: Kilelezo cha kwanza ilikuwa ni bunduki moja aina ya Shortgun Greener yenye namba 13002 iliyokatwa mtutu ikiwa imewekewa alama A, ganda moja la risasi likiwa na alama B na nilipokea risasi moja aina ya shortgun iliyopewa alama ya C.

Wakili: Ile barua ilikutaka ufanye nini?

Shahidi: Nilitakiwa nichunguze kama hilo ganda na risasi vinaweza kutumika kwenye hiyo bunduki.

Wakili: Nini kilifuata baada ya hapo?

Shahidi: Baada ya hapo nilianza uchunguzi mara moja.

Wakili: Ebu ieleze Mahakama namna ulivyofanya uchunguzi wako.

Shahidi: Kwanza nilichukua kielezo A ambacho ni bunduki na kielezo C ambacho ni risasi kuona kama inafanya kazi. Kweli risasi hiyo niliiweka kwenye bunduki hiyo nikalipua na ililipuka hivyo nikaipa jina la TC kwa maana ya Test from C.

Baada ya hapo nilichukua risasi maabara nikajaribisha kwenye silaha hiyo nikaona zinafanya kazi.

Wakili: Kwa nini ulifanya hivyo?

Shahidi: Nilifanya hivyo kulinganisha ili kupata tabia na baada ya kufanya hivyo nilikuta tabia zote za vifaa hivyo zinafanana.

Wakili: Ulitumia nini katika uchuguzi wako?

Shahidi: Tulitumia kompyuta na microsope (hadubini) kubaini hizo tabia. Microscope ni kifaa kinachotumika kubaini vitu vidogo ambavyo havionekani kwa macho.

Wakili: Baada ya uchunguzi nini kilibainika?

Shahidi: Baada ya uchunguzi huo ulinipatia positive (chanya) kwa maana ya kwamba kielezo B ambalo ni ganda kilionekana kutumika kutoka kielezo A ambayo ni bunduki.

Wakili: Ulipomaliza ulifanya nini?

Shahidi: Baada ya kumaliza kuandaa ripoti na kuandika maoni yangu kuhusu uchunguzi huo kisha nikasaini nikagonga mhuri, nembo ya ya polisi katika vilelezo vyote kisha nikakabidhi kwa wakubwa wangu kisha ilipigwa simu Mwanza waje kuchukua ripoti hiyo.

Baada ya kukamilisha ushahidi wake, Wakili wa upande wa utetezi, Emmanuel Sayi naye alipata nafasi ya kumhoji shahidi huyo kama ifuatavyo;

Wakili: Hicho kielezo B ambalo ni ganda la risasi unajua lilitengenezwa wapi?

Shahidi: Sijui.

Wakili: Uchunguzi huo ulitumia muda gani?

Shahidi: Tulifanya siku mbili na kumaliza.

Wakili: Je, unaweza kujua hilo ganda lilitumika tarehe ngapi?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Je, aina hiyo ya risasi inaweza kutumika kwenye bunduki nyingine?

Shahidi: Ndiyo inaweza kama ni aina hiyohiyo ya silaha.

Wakili: Hizo risasi unaweza kuzipata wapi?

Shahidi: Unazipata mtaani popote maana ni za kiraia siyo za kijeshi.

Baada ya wakili Sayi kumaliza, alimka mwenzake Jonathan Wangubo naye alimhoji shahidi huyo na ifuatayo ni sehemu ya maswali na majibu:

Shahidi: Si mnatumia uchunguzi wa kisayansi na unafanyikia uchunguzi kwenye maabara katika makosa ya kijinai?

Shahidi: ndiyo.

Wakili: Kwenye masomo ya A level ulisoma masomo gani?

Shahidi: Nilisoma masomo ya art (sanaa)

Wakili: Nakuomba uyataje masomo hayo.

Shahidi: English, Kiswahihi, Hhistoria na siasa.

Wakili: Je, wewe ulifanya uchunguzi wa aina gani?

Shahidi: Nilifanya Physical (kitu halisi) na Comparison (ulinganisho).

Wakili: Ulianza kutumia microscope tangu mwaka gani?

Shahidi: Tangu mwaka 2000.

Wakili: Ni kweli kwamba chombo kinachotumia utaalamu kinaweza kupoteza ufanisi wake?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Baada ya kumaliza uchunguzi wako je ulifanya ulinganisho huo kwenye karatasi ambao unaweza kuonyesha hapa mahakamani?

Wakili: Sikufanya hivyo kwa sababu kompyuta ilikuwa imeharibika.

Wakili: Hayo matokeo yako yalitumwa lini kwenda Mwanza?

Shaidi: Sikumbuki taarifa ilitumwa lini.

Washtakiwa saba katika shauri hilo ni Peter Muganyizi, Chacha Waikena, Magige Mwita, Buganzi Edward, Bhoke Marwa, Abdallah Petro na Abdalrahman Ismail.

Kamanda Barlow aliuawa kwa kupigwa risasi usiku wa Oktoba 13, 2014 katika tukio lililotokea eneo la Kitangiri Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.

Shauri hilo linaendelea leo

Chanzo: mwananchi.co.tz