Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KESI MAUAJI YA LIBERATUS BARLOW: Kamishna wa polisi aeleza mshtakiwa alivyosimulia mkanda mauaji ya Barlow

16310 Mauaji+pic TanzaniaWeb

Sun, 9 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Shahidi wa 20 katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, Kamishna wa Polisi, Robert Mayala ameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kuwa mmoja wa washtakiwa saba katika shauri hilo, Magige Mwita alimwelezea namna mauaji hayo yalivyotekelezwa.

Akitoa ushahidi wake jana mbele ya Jaji Sirilius Matupa, shahidi huyo alidai mshtakiwa huyo pia alimweleza jinsi alivyoshiriki tukio hilo na aliyefyatua risasi iliyomuua kigogo huyo wa polisi katika tukio lililotokea usiku wa Oktoba 13, 2014 eneo la Kitangiri, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.

Akiongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Robert Kidandu, Mayala ambaye ni kamanda wa Polisi Kikosi cha Bandari, Dar es Salaam alisoma maelezo ya mshtakiwa aliyoyachukua na ifuatayo ni sehemu ya mahojiano na majibu kati yake na mawakili:

Wakili: Unakumbuka siku ya tarehe 24/10/2012 ulikuwa wapi?

Shahidi: Nilikuwa nyumbani nilipigiwa simu na kiongozi wangu niende Kituo Kikuu jijini Dar es Sa aam.

Wakili: Alikueleza nini baada ya kukupigia simu hiyo?

Shahidi: Aliniambia kuna mtu amekamatwa kuhusiana na mauaji ya aliyekuwa kamanda Barlow hivyo niende kumchukua maelezo.

Wakili: Ulipofika katika kituo hicho ulifanya nini?

Shahidi: Nilipofika nilimkuta mtuhumiwa Magige Mwita Marwa (mshtakiwa wa tatu), akiwa chini ya askari.

Wakili: Ulifanya nini baada ya kumuona mtuhumiwa?

Shahidi: Nilitafuta chumba kwanza kwa ajili ya mahojiano kisha nikamchukua kwenda naye kwenye chumba hicho.

Wakili: Ulifanya nini kabla ya kumchukua maelezo?

Shahidi: Nilijitambulisha kwake kwanza, nikamweleza kosa analotuhumiwa.

Wakili: Ulimweleza kwamba anatuhumiwa kwa kosa gani?

Shahidi: Kosa la mauaji ya kamanda (Barlow).

Wakili: Ulifanya nini baada ya hapo?

Shahidi: Nilimweleza haki zake za kisheria.

Wakili: Ni haki gani hizo ulimpa?

Shahidi: Nilimweleza kuwa ana haki ya kuwa na wakili wake, ndugu au rafiki yake wakati anachukuliwa maelezo.

Wakili: Nini kilifuata baada ya kumwambia hivyo?

Shahidi: Nilimuuliza pia kama anaweza kuandika mwenyewe au nimwandikie na akasema nimwandikie.

Wakili: Nini sasa kilifuata baada ya hapo?

Shahidi: Alinieleza kwamba yupo tayari kuchukuliwa maelezo na nikamwambia maeleo hayo yanaweza kutumika kama ushahidi mahakamani na akasema sawa yupo tayari nimchukue maelezo hayo na anaamini nitaandika kwa usahihi.

Wakili: Je, ukiyaona maelezo hayo unaweza ukayatambua?

Shahidi: Naweza kwa sababu ni mwandiko wangu, nilisaini pia kwenye hayo maelezo.

Baada ya mahojiano na majibu hayo, wakili Kidandu aliiomba mahakama kukubali shahidi huyo apewe maeleo hayo ili kuyatambua na kuyasoma mbele ya mahakama.

Katika maelezo hayo mshtakiwa alinukuliwa akisema aliwahi kufungwa Gereza la Butimba kwa kosa la kuiba nyanya wakati alipokuwa akifanya biashara soko la Mirongo mwaka 2000, alihukumiwa kufungwa miaka 30 jela.

Baada ya kukata rufaa na kushinda, alitoka gerezani Mei 2012 na kukuta mkewe aliyesema walikuwa wakiishi eneo la Mabatini, Mwanza ameolewa na mwanaume mwingine.

Melezo hayo yanadai mshtakiwa alimweleza shahidi kuwa alipokuwa gerezani, ndiko alikokutana na Muganyizi (Peter) ambaye ni mshtakiwa wa kwanza na Chacha ( Waikena), mshtakiwa wa pili, alisema walikuwa na kesi ya kukutwa na risasi tisa na unyang’anyi wa kutumia silaha.

Alidai baada ya kutoka gerezani alikutana na Muganyizi na Chacha Septemba 29 eneo la kambi ya Jeshi Nyashana wakiwa na mtu mwingine ambaye hakumfahamu, ambako walipanga namna ya kufanya uporaji maeneo mbalimbali ya jiji la Mwanza kama njia ya kujipatia kipato.

Maelezo hayo yanadai kuwa walikubaliana wakutane eneo la Shule ya Msingi Mbugani ambako waliwakuta watu wengine watatu ambao hawafahamu, mmoja wao akiwa na bunduki, mwingine rungu na aliyesalia akiwa na fimbo.

Walipokutana, bunduki ile alikabidhiwa Muganyizi huku kila mmoja akipewa majukumu ya kutekeleza.

Wakiwa katika utekelezaji wa shughuli ya kumpora kila waliyekutana naye kuanzia maeneo ya Nyamanoro na Kirumba, walikutana na mwanamke mmoja eneo la Kitangiri wakampora simu ya kiganjani na mbele wakaona gari limeegeshwa upande wao wa kulia ikiwa imewasha taa na kumpa ishara ya kumtaka dereva kuzima taa kwa kummulika kwa tochi lakini alikaidi.

Maelezo hayo yanadai baada ya kuona dereva amekaidi agizo lao, waliamua kulisogelea gari hilo huku Muganyizi aliyekuwa na bunduki akizunguka upande wa dereva ambaye pia alikuwa na mwanamke ndani ya gari hilo.

Baada ya kumfikia, anasema Muganyizi alimuuliza yule dereva sababu za kutozima taa lakini alijibiwa kuhojiwa kuwa hamjuhi kwamba yeye ni kamanda na kumwambia ngoja awaite askari.

Inaelezwa kitendo hicho kilimkasirisha Muganyizi na kuamua kumfyatulia risasi iliyompata eneo la shingoni.

Kitendo hicho kinadaiwa kilisababisha Muganyizi kulaumiwa na wenzake, kwa kumuua mtu huyo lakini ilibidi wenzake kunywea kwa kuwa mwenzao aligeuka mbogo kwa ukali.

Baada ya mauaji hayo, mshtakiwa anadaiwa kusema walitoa mwili wa marehemu ndani ya gari na kuulaza chini kabla ya kuwapokea yeye na mwanamke aliyekuwamo ndani ya gari na kuchukua mali na vitu walivyokuwa navyo ikiwamo simu ya kiganjani ambayo hata hivyo hakukumbuka alyeichukua.

Kutokana na taharuki iliowapata, kila mtu inadaiwa aliondoka kwa njia yake huku Muganyizi akimpatia Sh20,000 ilipofika asubuhi walisikia tangazo kuwa aliyeuawa alikuwa ni kamanda wa polisi mkoa.

Kutokana na hofu, Oktoba 18,2012 aliondoka kwa basi kwenda jijini Dar es Salaam ambako alipokewa na mshtakiwa wa pili, Chacha ambaye alimpeleka kujificha kwenye nyumba ya kulala wageni eneo la Vingunguti ambako pia alimkuta Muganyizi.

Oktoba 23, 2012 yeye na wenzake walikubaliana kutafuta bunduki kwa kupora silaha kutoka kwa askari wa kampuni ya ulinzi waliokuwa wakilinda jirani, lakini walikamatwa wakiwa eneo la Vingunguti na kufunguliwa kesi ya mauaji ya Barlow kabla ya kusafirishwa kwa ndege hadi Mwanza.

Washtakiwa wengine aliosema walisafirishwa pamoja kutoka Dar es Salaam ni Buganzi Edward, Bhoke Marwa, Muganyizi, Waikena na Magige Mwita.

Baada ya mahojiano na kusomwa kwa maelezo hayo, Wakili wa utetezi, Jonathan Wangubo naye alimhoji.

Wakili: Kwa kuwa haukumkamata mtuhumiwa hivyo huwezi kuithibitishia mahakama kuwa mtuhumiwa alikamatwa saa ngapi?

Shaidi: Ndiyo.

Wakili: Umesema ulimpa haki zake. Je, kwenye maelezo hayo uliyosoma hapa kuna sehemu umeandika hayo maneno.

Shahidi: Hapana.

Wakili: Wakili ndiyo advocate kwa kiingereza?

Shahidi: Sijui.

Wakili: Lakini Lawyer ni mwanasheria?

Shahidi: Ndiyo.

Kukamilika kwa ushahidi wa shahidi wa 20 kulitoa fursa kwa shahidi wa 21, D 4426 Sajenti Fred naye kutoa ushahidi wake akiongozwa na wakili Kidando akielezea alivyochukua maelezo ya mshtakiwa wa kwanza Muganyizi.

Washtakiwa saba katika shauri hilo ni Muganyizi, Waikena, Magige Mwita, Buganzi Edward, Bhoke Marwa, Abdallah Petro na Abdulrahman Ismail.

Soma Zaidi:

KESI MAUAJI YA LIBERATUS BARLOW: Mtaalamu aeleza alivyooanisha risasi, bunduki

Chanzo: mwananchi.co.tz