Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jumanne atupwa jela miaka 20 kwa uhujumu uchumi

Operanews1678027839426 Jumanne Kulwa Sizya (31), mkazi wa Kata ya Ipole, Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora.

Sun, 5 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jumanne Kulwa Sizya (31), mkazi wa Kata ya Ipole, Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela baada ya kutiwa hatiani kwa makosa manne ya uhujumu uchumi.

Akitoa hukumu hiyo juzi, Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Tabora, Sigwa Mzige alisema mahakama hiyo imefikia hatua hiyo baada ya mtuhumiwa Sizya kukutwa na hatia katika makosa manne ambayo ni; kuingia kwenye hifadhi bila kibali, kupatikana na silaha, kukutwa na nyara za serikali, kupatikana na silaha za mlipuko pamoja na kujenga kambi hifadhini. 

Alisema mshtakiwa huyo alikamatwa na maofisa wa wanyamapori kwenye Kijiji cha Isimbila, kwenye Hifadhi ya Ugalla wilayani humo na alipopekuliwa, hakuwa na kibali chochote ambacho kinamruhusu kuingia hifadhini.

Mahakama hiyo ilifikia hatua hiyo kutokana na mshtakiwa kuthibitika kutenda makosa hayo ambayo yamemtia hatiani, ikieleza kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria ya nchi. 

Wakili wa Serikali Lucy Kyusa alidai mahakama huko kuwa mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo mnamo April 12, 2022 kwenye eneo la Isimbila, ndani ya Hifadhi ya Ugalla wilayani Sikonge mkoani Tabora.

Hakimu Mzige alisema mshtakiwa huyo katika kosa la kwanza alitakiwa kulipa faini ya Sh. 500,000 au kwenda jela mwaka mmoja. Kwa  kosa la pili hadi la nne, amepewa adhabu ya kwenda jela miaka 20.

"Mahakama hii inazingatia makosa aliyotenda mshtakiwa Jumanne Kulwa ya kuhujumu uchumi, ni kosa la kuingia kwenye hifadhi bila ya kuwa na kibali na kukutwa na silaha za moto, serikali hairuhusu," alisema.

Wakitoa ushahidi mahakamani huko, maofisa wa wanyamapori walidai walipofanya doria kwenye hifadhi hiyo kwa kufuata nyayo za baiskeli, walimkuta mshtakiwa akiwa ameweka kambi na walifanikiwa kumkamata hifadhini.

Mshtakiwa Kulwa katika utetezi wake alikana kukamatwa hifadhini na maofisa hao na kudai mahakamani kuwa alikuwa anatokea shambani kulima na alikuwa na jembe mkononi mwake huku akiiomba mahakama kumpunguzia adhabu kutokana na kwamba ana mke mmoja na watoto wawili wanaosoma.

Licha ya utetezi huo, mshtakiwa huyo alikuhumiwa kutumikia miaka 20 gerezani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live