Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jukwaa la Kitaifa la Haki Mwanamke lazinduliwa

Ndumbaro Jukwaa la Kitaifa la Haki Mwanamke lazinduliwa

Thu, 8 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro amezindua Jukwaa la Kitaifa la Haki Mwanamke na ameliagiza lihakikishe linamnufaisha mwanamke moja kwa moja.

Amesema jukwaa hilo limelenga kurahisisha upatikanaji haki kwa mwanamke na kwa wakati, kuimarisha mifumo ya upatikanaji haki kwa mwanamke katika kesi za jinai na pia katika kesi za madai.

Uzinduzi wa jukwaa hilo umefanyika juzi kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa haki nchini wakiwamo baadhi ya wabunge, wadau wa maendeleo, asasi za kiraia, idara na taasisi za serikali.

Dk Ndumbaro alisema jukwaa pia linatakiwa kuhakikisha vikwazo vinavyomfanya mwanamke wa Kitanzania asipate na kufurahia haki za kiuchumi vinaondolewa. Pia kuhakikisha wanapata haki za kijamii, haki za kimazingira na haki za kisiasa ambazo zitatoa fursa kwa mwanamke na kufikia 50 kwa 50.

“Hivyo jukwaa liseme wanawake wenye sifa wanaogombea wanasaidiwaje,” alisema Dk Ndumbaro na kuongeza kuwa ili liwe na uhalisi na kuheshimika, ni lazima liguse mahitaji ya mwanamke wa Kitanzania na shughuli zake zifanyike nchini.

“Ili jukwaa lifanikiwe lazima wadau mbalimbali ikiwa ni serikali, asasi za kiraia, viongozi wa mila na dini sio tu kufanya kazi pamoja, pia kuzungumza lugha moja,” alisema.

Alisema matarajio ya Watanzania ni kuwa jukwaa litafanya kazi muhimu ya kulinda na kukuza uchumi wa mwanamke wa Kitanzania.

“Wizara ya Katiba na Sheria itaendelea kushirikiana na wadau wote katika kuhakikisha tunapaza sauti kuhusiana na mambo mbalimbali zikiwemo haki za binadamu, na leo tunaongelea haki ya mwanamke,” alisema.

Jukwaa hilo litakuwa la kipekee kuwezesha upatikanaji wa taarifa na ushahidi katika masuala yanayoathiri wanawake na changamoto zinazowakabili.

Aidha, jukwaa litabainisha maeneo ya kimkakati ambayo yatatengenezewa mikakati na kutekelezwa ili kusaidia mwanamke kupata haki, kuimarisha mfumo wa upatikanaji wa takwimu ambazo zitawezesha serikali kupanga mikakati ya namna ya ufikiwaji wa haki kwa mwanamke.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Pauline Gekul ambaye amepewa jukumu la kulea jukwaa hilo, alisema jukwaa hilo litawafikia wanawake kwenye kata zote nchini kuwapa elimu kuhusu masuala ya upatikanaji wa haki.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu, Mwanaidi Ali Khamis alisema wanawake wamekuwa kimya pindi wanapokumbana na changamoto za maisha hivyo jukwaa hilo litahakikisha wanapata haki zao.

Wakili wa Serikali, Ester Msambazi alisema ukatili bado upo kwa wanawake kwa kuwa mfumo wa haki haujamwezesha kupata haki kwa wakati hivyo kupitia jukwaa hilo watahakikisha suala hilo linawafikia kwa wakati.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mary Makondo alieleza wanawake hukosa haki kwa sababu ya ukosefu wa uelewa hivyo kupitia jukwaa hilo kila mdau atatimiza wajibu wake ili kuhakikisha malengo tarajiwa yanafikiwa na wanapata haki zao.

“Katika utekelezaji wa mpango huo, wizara imeweza kuimarisha mifumo ya sheria ikiwemo kutungwa kwa Sheria ya Msaada wa kisheria na kupitia sheria hiyo wanawake wamekuwa wanafaidika kisheria kwenye maeneo yao,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live