Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jinsi mstaafu wa Bandari alivyouawa kwa mkasi Dar

36759 Mstaafupic Jinsi mstaafu wa Bandari alivyouawa kwa mkasi Dar

Wed, 16 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Taarifa za kuuawa kwa Tunsume Sakajinga, ambaye siku chache zilizopita alistaafu kazi Mamlaka ya Bandari, sio tu zimewashtua ndugu jamaa na majirani wa Mtaa wa Mgeninani, Kijichi jijini hapa lakini mazingira ya kifo chake yameacha simanzi na maswali mengi.

Mama huyo aliuawa Jumamosi iliyopita saa tano asubuhi kwa kupigwa na kitu kizito kichwani kisha kuchomwa na mkasi ambao uliachwa shingoni mwake.

Mwili wa Tunsume ulikutwa chini ya sinki la kuoshea vyombo huku ukiwa umefunikwa mkeka na kwa mujibu wa Jeshi la Polisi uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Emmanuel Lukula alisema bado wanafanya uchunguzi kubaini nani alihusika na tukio hilo.

Simulizi ya mashuhuda

Simulizi ya tukio hilo inaanzia kwa fundi wa grili, Thomas Ndimbo ambaye alisema dakika chache kabla Tunsume hajauawa, alimpigia simu akimuomba aende kufungua mlango wa moja ya vyumba vya nyuma yake ambao ulikuwa umejifunga.

“Aliponipigia simu aliniambia anahisi kuna mtu ndani ya chumba chake kwa hiyo sikukawia, nilitumia kama dakika tano tu kufika nyumbani kwake,” alisema Ndimbo.

Alipofika alikuta geti la nje likiwa limefungwa ikabidi aanze kugonga huku akibisha hodi bila mafanikio.

“Nilibisha sana hodi nikagonga baadaye akaja jirani nikamwambia simu za mama zinaita lakini sioni dalili ya mtu kwa sababu nagonga sifunguliwi. Basi tukasaidiana kugonga pale wakaja majirani wengine,” alisema.

Alisema ukimya ule uliwafanya wamuite mjumbe wa shina la mtaa huo ambaye alitoa taarifa polisi ambao walifika muda mfupi baadaye.

“Tukaazima ngazi kwa jirani tukapanda kama wanaume sita hivi tukaingia ndani na kufungua geti, baadaye tulizunguka nyumba nzima lakini ilikuwa imefungwa kwa ndani,” alisema.

Alisema walienda mpaka kwenye dirisha la chumba cha Tunsiime wakaona funguo ambazo walivuta kwa kutumia mti na kisha kuanza kujaribu kufungua mlango wa nje bila mafanikio.

“Nilikuwa na vifaa hivyo nikasaidia tukabomoa, tulipoingia ndani tulimkuta mama akiwa chini ya sinki huku mwili wake ukiwa umetokeza kwa nje,” alisema Ndimbo.

Mjumbe wa Shina Namba 15 la mtaa huo, Pili Lwanga alisema baada ya kuona mwili wake, walidhani kwamba amejeruhiwa hivyo kuhitaji msaada wa kuwahishwa hospitali.

“Tuliona damu na mchi uko pembeni, tulipomvuta tukaona alikuwa amechomwa mkasi ambao ulishindiliwa kiasi cha kubaki mishikio tu. Polisi mmoja alipomuangalia akasema alikuwa ameshafariki dunia.”

Alisema muda mchache baadaye walifika askari wengine ambao walianza kufanya upekuzi kwenye nyumba hiyo.

Lwanga alisema wakati polisi wakiendelea na upekuzi waliona mkeka ukiwa pembeni mwa friji na kwamba baada ya askari mmoja kuushika aliona na kuufungua walimuona kijana wa kazi wa mama huyo waliyemtaja kuwa ni Gideon Elias.

“Alipiga kelele akasema ‘msiniue’ tulishtuka kweli,” alisema na kuongeza kuwa baadaye kijana huyo aliwaeleza kwamba kuna watu wawili walikuwa wamevamia nyumba hiyo na kumfanyia ukatili mama huyo huku wakimtaka akae kwenye eneo hilo bila kujitokeza.

Kuhusu kijana huyo, Kamanda Lukula alisema “Bado tunachunguza na hakuna mwenye uhakika kama ‘houseboy’ wake ndiye alimuua. Siwezi kuthibitisha ila bado tunachunguza,” alisema.

Mjumbe huyo wa shina alisema hekaheka hiyo iliwachukua hadi saa mbili usiku wakati askari hao waliondoka na mwili wa mama huyo na kuuhifadhi katika Hospitali ya Rufaa ya Temeke.

Msemaji wa familia hiyo Kissa Mwankusye alisema, “Tumepigwa bumbuwazi kusema kweli. Tumesikitika mno tunaona ni kama sinema inatembea. Kulia tunashindwa yaani tumebaki kushangaa tukiwaza binadamu anawezaje kuwa katili kiasi hiki? Kweli imetuumiza sana.”

Alisema dada yake ambaye alistaafu Desemba 31, mwaka jana akiwa mfanyakazi wa Bandari, alikuwa na mtoto mmoja tu ambaye alimuozesha mwaka jana na hivi sasa anaishi nje ya nchi.

“Binti yake ameingia hapa Dar usiku wa kuamkia (leo) jana,” alisema.

Alisema siku kadhaa baada ya kustaafu, alienda kazini kwake kuwaaga wenzake kwa kuwaambia, “kwa herini mimi nimeshastaafu sasa”, alisema Mwankusye.

Alisema mbali na kijana wake wa kazi ambaye ameishi naye kwa zaidi ya miaka mitatu, mama huyo alikuwa akiishi pia na mtoto wa dada yake.

Jirani mwingine aliyekuwepo siku ya tukio hilo, Ipyana Kuchaka alisema mama huyo alikuwa mcheshi na aliishi vizuri na kila mtu.

“Wanadamu wenzangu wajue tu damu ni nzito kuliko maji, ukifanya mauaji utajulikana huna kwa kujificha. Tuache tamaa zisizo na maana,” alisema Kuchaka ambaye pia alikuwa akifanya kazi na mama huyo.



Chanzo: mwananchi.co.tz