Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jinsi alivyopangua kifungo cha miaka 97

46032 Pic+kifungo Jinsi alivyopangua kifungo cha miaka 97

Mon, 11 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kwa mtu mwenye elimu ya kidato cha nne, asiye na uwezo kiuchumi na ambaye familia yake inamuona kuwa anafanya makosa ya kujitakia, kifungo cha miaka 97 jela kingemkatisha tamaa ya maisha.

Adhabu hiyo kubwa ingekuwa ndio mwisho wa ndoto zake za maisha, lakini si kwa Kelvin Lwambano, mkazi wa Kinondoni; alipigana hadi mwisho na kushinda rufaa dhidi ya kifungo hicho.

Na si rufaa dhidi ya hukumu iliyomtia gerezani, bali pia kusaidia kukata rufaa na kushinda hukumu za vifungo kwa wafungwa wengine 200 aliowakuta gerezani na kusaidia watuhumiwa wengine 500 kupata dhamana.

Na sasa yuko huru uraiani akimsifu Mungu na kutangaza Injili, ikiwa ni kutimiza nadhiri aliyojiwekea wakati akiwa gerezani kuwa angeshinda rufaa, angejitolea maisha yake kumsifu Mola.

Luambano alitoa ushuhuda huo katika mahojiano na Mwananchi, ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kutoka kifungoni Machi 2018.

“Sikuwahi kukata tamaa ya maisha wakati nikiwa jela,” alisema Luambano. “Kwanza nilikubaliana na hali hiyo.”

Luambano, ambaye alikaa gerezani kwa miaka mitatu akiwa mahabusu na baadaye miaka mitano akiwa mfungwa, alikakamatwa Novemba 29, 2010 na kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu Desemba 10, 2010 na kusomewa mashtaka kumi tofauti ya jinai, yakiwemo makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha na mauaji yaliyomfanya asipate dhamana.

Alidaiwa kufanya makosa hayo mwaka 2010.

Kwa kuwa alikuwa na kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha na kosa la mauaji, Luambano hakupata dhamana na hivyo kuanza maisha ya gerezani tangu siku alipopandishwa kizimbani na kusomewa mashataka yake kwa mara ya kwanza. Alianza kuishi Gereza la Keko kama mahabusu wakati akisubiri hukumu hadi mwaka 2013 alipopatikana na hatia na kufungwa.

Baada ya hukumu hiyo, Luambano alihamishiwa Gereza la Ukonga ambako aliishi kwa miaka mitano hadi alipoachiwa Machi 2018.

Alihukumiwa kifungo cha jumla ya miaka 97 katika kesi mbili tofauti za jinai, kesi namba 233 na 226 za mwaka 2010.

Katika kesi ya jinai namba 233, alihukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka 37 baada ya kupatikana na hatia na katika kesi ya jinai namba 226 alihukumiwa kifungo cha miaka 60 baada ya kupatikana na hatia pia.

Lakini, badala ya kunung’unikia kifungo hicho, Luambano aliamua kuwekeza kwenye elimu na hivyo akaanza kujiendeleza kwa lengo la kusomea sheria, tofauti na ilivyo kwa wafungwa wengine.

Alisema kabla ya kuingia gerezani alikuwa na elimu ya kidato cha nne, hivyo mwaka 2014 akiwa Ukonga alisoma elimu ya kidato cha tano na sita kwa mwaka mmoja, akifundishwa na walimu ambao ni askari magereza na wafungwa ambao kabla ya kuingia gerezani walikuwa na fani ya ualimu na hivyo kuthibitishwa kufanya kazi hiyo.

Baada ya kufanikiwa, mwaka 2015 alisoma diploma ya sheria na anasema “nikaambiwa nimefaulu”.

“Hali ya gerezani ni tofauti,” alisema Luambano katika mahojiano hayo yaliyofanyika nyumbani kwake.

“Nilikuwa nasoma baadaye walimu wanatafuta mitihani, inaletwa tunafanya. Lakini kwa kuwa nilikuwa mfungwa, sikufahamu ilikuwa inatoka wapi; serikalini ama la. Ila ilikuwa inakuja ikiwa imechapwa.” Luambano alisema walikuwa wanapata vitabu na kuelezwa majibu ya mitihani lakini hawakuwa wakiruhusiwa kukaa na vitabu kwa kuwa mfungwa haruhusiwi kukaa na nyaraka zozote.

“Kuna chumba kimetengwa kama stoo. Huko ndiko vitu vyote vinahifadhiwa,” alisema Luambano.

Luambano alisema baada ya kupata elimu ya sheria akiwa gerezani, alianza kuandaa na baadaye kukata rufaa dhidi ya hukumu iliyomfunga.

“Nilifanikiwa kushinda mashtaka yote,” alisema.

Alisema katika uamuzi wa Jaji Lugano Mwandambo wa Mahakama Kuu uliotolewa Februari 8, 2016 dhidi ya rufaa namba 7/2014, aliachiwa huru baada ya upande wa mashtaka, ulioongozwa na wakili wa serikali, Mosie Kaima kushindwa kuthibitisha pasipo kuacha shaka mashtaka dhidi yake.

Rufaa hiyo ilitokana na kesi ya jinai namba 226/2016 ambayo alihukumiwa kifungo cha miaka 60 jela baada ya kupatikana na hatia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Luambano, ambaye alizaliwa mwaka 1981, alisema mwaka 2015 aliachiwa huru baada ya kukata rufaa dhidi ya hukumu ya kesi ya jinai namba 223/2010 iliyompa kifungo cha miaka 37 jela.

Alisema katika kesi nyingine aliachiwa huru baada ya majaji wa Mahakama Kuu-Mwandambo na Richard Kibela-kubaini kuwa hakimu alipotoka kwa kuona upande wa mashtaka ulithibitisha mashtaka yao pasipo kuacha shaka. Majaji hao waliungana na hoja za mrufani kuwa alifungwa kimakosa.

Moja ya kesi dhidi yake ni ya mauaji ambayo ilikuwa ikiendelea wakati ameshahukumiwa kifungo cha miaka 97 kwa kukutwa na hatia ya unyang’anyi kwa kutumia silaha na makosa mengine, kwa mujibu wa ripoti za magazeti.

Alipofikishwa mahakamani Oktoba mosi 2014, Luambano alirushiana maneno na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Kisutu, Hellen Riwa akimtuhumu kuwa ana upendeleo baada ya kukubaliana na madai ya upande wa mashtaka kuwa upelelezi wa kesi yake haujakamilika na hivyo kuomba apange siku nyingine ya kuitaja.

Alidai kuwa kwa miaka mitano upande wa mashtaka ulikuwa na hoja hiyo kwamba uchunguzi haujakamilika wakati washtakiwa wakiendelea kuishi mahabusu.

Alimwambia hakimu huyo kuwa kesi hiyo ilishatupwa na Hakimu Mwandamizi Aloyce Katemana mwaka 2011 baada ya uchunguzi kutokamilika, lakini watuhumiwa, akiwemo yeye, walikamatwa tena na kushtakiwa kwa kosa lilelile.

Alisema katika kesi hiyo, watu tofauti walishawahi kukamatwa na kushtakiwa kwa kosa hilohilo la kumuua mtu mmoja na mara kadhaa ikatupwa, lakini washtakiwa walikamatwa tena na kufunguliwa mashtaka.

“Tulitegemea uchunguzi ungekuwa umefanyika na kuripotiwa mahakamani kuwa umekamilika. Tunakuomba uvae viatu vya Hakimu Katemana na kuitupa kesi hii kwa kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kukamilisha uchunguzi,” alidai Luambano wakati huo.

Lakini, upande wa mashtaka ukapinga hoja hiyo na hakimu kuikubali, ndipo Luambano alipocharuka na kumtaka hakimu huyo kujiondoa, akakataa kwa madai kuwa anachofanya ni kusikiliza hatua za awali za kesi hiyo.

“Kwa maana hiyo niondoe kwenye kesi. Andika kwamba simo. Sitakuja mbele yako tena, sitaki kukuona tena,” alisema, lakini hakimu akamshauri kuwa kama ana tatizo akate rufaa Mahakama Kuu.

Katika tukio jingine mwaka 2010, aliyekuwa kamanda wa polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alitangaza kuwa Jeshi la Polisi limekamata watu 17 waliokuwa wanatuhumiwa kujihusisha na ujambazi baada ya kufanya msako maeneo ya Kawe, Mbezi Beach, Goba, Salasala, Kimara na Mbezi Juu ambao ulifanikiwa kuwanasa majambazi hao.

Miongoni mwa waliotajwa alikuwemo Kelvin Luambano, ambaye Kova alisema waliwatambua kwa kutumia mbinu zao za kiaskari.

Mbali na kushinda rufaa dhidi ya hukumu yake, Luambano alisema alitumia maarifa aliyoyapata kusaidia wafungwa wenzake kushinda rufaa zao na mahabusu kupata dhamana.

“Nilitoa mafunzo kwa watu wote bila ubaguzi wa dini wala hali ya mtu. Pia wakati nikiwa gerezani niliandaa rufaa zaidi ya 200 na wote waliorudi kukata rufaa, waliachiwa huru. Pia niliandaa maombi ya dhamana ya zaidi ya mahabusu 500 na wote walipewa dhamana,” alidai Luambano.



Chanzo: mwananchi.co.tz