Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jicho kwa jicho, hizi hapa siku 226 za Mbowe mahabusu

Mbowepicc Siku 226 za Mbowe Mahabusu

Fri, 4 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katika hali isiyokuwa ya kawaida tofauti na mategemeo ya watu wengi, leo 04, Machi, 2022 Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali, DPP, amewasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi ya ugaidi n uhujumu uchumi iliyokuwa ikimkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na wenzake watatu katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Ikumbukwe kuwa leo ilikuwa siku ambayo washitakiwa walikuwa wakianza utetezi wao mara baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao na Mahakama kuwakuta na kesi ya kujibu.

Kesi hiyo imetimiza jumla ya siku 216 tangu ilipoanza kusikilizwa Mahakamani, huku ikiwa imepandisha jumla ya mashahidi wa mashitaka 13 waliohitimisha ushahidi wao wote kwa pamoja.

Tangu kesi hiyo ianze imesikilizwa na jumla ya majaji watatu ambao ni Elinza Luvanda, Mustapha Siyani na Joachim Tiganga.

Huku mawakili kutoka upande wa Jamuhuri wakiwa ni Robert Kidando, Pius Hilla, Abdallah Chavula, Jenitreza Kitali, Nassor Katuga, Esther Martin Tulimanywa Majige na Ignas Mwinuka.

Na upande wa utetezi wakiongozwa na jopo la mawakili 26 ambao ni pamoja na Peter Kibatala, John Mallya, Dickson Matata, Fredrick Kihwelo, Faraji Mangula na Idd Msawanga.

Itakumbukwa kuwa Agosti 09, 2020 washtakiwa wenzie na Mbowe ambao ni Halfan Bwire Hassan, Adam Hassan Kasekwa na Mohamed Abdallah Ling'wenya walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa makosa saba waliyodaiwa kuyatenda kati ya Mei 01 na Agosti 01, 2020.

Walidaiwa kukutwa na silaha, vifaa vya mlipuko, sare za Jeshi la Wananchi Tanzania JWTZ pamoja na dawa za kulevya aina ya Heroin.

Mnamo Julai 21, 2021, polisi waliwakamata watu wapatao 11 kwenye hoteli ya Kingdom iliyopo Jijini Mwanza na siku iliyofuata walithibitisha kuwakamata viongozi 15 wa CHADEMA akiwamo Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Aikael Mbowe.

Agosti 05, 2021 kesi ya Uhujumu Uchumi namba 63/2021 ilianza rasmi na kupangwa kufanyika kwa njia ya mtandao ambapo ilikwama kuendelea kutokana na hitilafu ya mtandao mbele ya Hakimu Mwandamizi Thomas Simba.

Walifikishwa tena Mahakamani tarehe 06 ya mwezi Julai 2021 ambapo upande wa mashtaka ulidai ukiukwaji wa utaratibu wa kufungua kesi hiyo kwani Mahakama ya Kisutu haina mamlaka kuisikiliza.

Agosti 13, 2021 iliitwa tena kesi hiyo na miongoni mwa watu waliohudhuria ni pamoja na Balozi wa Sweeden Anders Sjoberg, washtakiwa waliomewa mashtaka yao ambayo ni Uhujumu Uchumi pamoja na Ugaidi.

Mbowe alisomewa maelezo ya mashtaka matatu ikiwa ni pamoja na kufadhili vitendo vya ugaidi, kula njama za kumdhuru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya.

Upande wa mashtaka ulisema unatarajia kuwa na jumla ya mashahidi 24 akiwamo Mkurugenzi wa Upelelezi DCI, Robert Boaz pamoja na vielelezo vya maandishi 19.

Upande wa Utetezi wao waliweka wazi mashahidi wao wawili ambao ni IGP Simon Sirro na Ole Sabaya.

Na ilipofika Agosti 31, washtakiwa walifikishwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ambapo mawakili upande wa utetezi waliiambia Mahakama hiyo kuwa haina Mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Hoja hiyo ilipigwa na kesi iliendelea kusikilizwa Septemba 01, 2021.

Septemba 06, Jaji Luvanda alitangaza kujitoa kusikilia kesi hiyo mara baada ya washtakiwa hao kuieleza Mahakama hawana imani naye.

Septemba 08 kesi hii ilitajwa tena mbee ya Jaji Mustapha Siyani ambaye pia alikuja kujitoa kusikiliza kesi hiyo mara baada ya kuteuliwa na Rais Samia kuwa Jaji Kiongozi Oktoba 08, 2021.

Oktoba 20, 2021 Jaji Siyani aliyatupilia mbali mapingamizi yote yaliyowasilishwa na upande wa Utetezi katika kesi hiyo.

Baada ya kesi kusimama kwa muda wa siku nane hatimaye ilitajwa tena mbele ya Jaji Joachim Tiganga na kuanza kuwasikiliza mashahidi wote 13 kuanzia wa kwanza hadi wa mwisho

Februari 15 mara baada ya shahidi wa 1 upande wa Jamuhuri kumaliza ushahidi wake, Wakili upande wa mashtaka aliiambia Mahakama kuwa wamefunga ushahidi na kuiomba Mahakama iwaone washtakiwa wote kuwa na kesi ya kujibu.

Wengine waliotoa ushahidi wao ni Kamanda wa Polisi Kinondoni RPC, Ramadhani Kingai pamoja na Mkaguzi wa Polisi, Mahita Omary Mahita.

Februari 18,Mahakama hiyo iliwakuta washtakiwa hao kuwa na kesi ya kujibu na kupanga tarehe ya leo Machi 04, 2022 kuwa wataanza kujitetea.

Julai mwaka 2021 Mbowe alikamatwa na kuwekwa Mahabusu hadi hii leo Machi 04, 2022 zimetimia jumla ya siku 226 za Mbowe kuwepo Mahabusu.

Hatua hii imepongezwa na watu wengi ndani na nje ya nchi huku wakisifu kuwa maamuzi hayo ni busara na demokrasia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live