Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jela mwaka mmoja kwa kumtukana mama mzazi

Jelaaaaaa Jela mwaka mmoja kwa kumtukana mama mzazi

Fri, 27 Aug 2021 Chanzo: ippmedia.com

MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala imemtia hatiani na kumuhukumu kwenda jela mwaka mmoja Zarina Sadiki kwa kosa la kutumia lugha ya kuudhi na kumtukana mama yake mzazi.

Zarina alihukumiwa jana mbele ya Hakimu Mfawidhi, Martha Mpaze, baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili.Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mpaze alisema Zarina anadaiwa Novemba 29, 2019, maeneo ya Kariakoo, Uhuru na Nyamwezi, alimtukana mama yake, Rafika Sadiki.

Hakimu alisema mshtakiwa anadaiwa kumwambia mama yake chizi, malaya mkubwa, sio mama yake, baba yake hajakumwoa, mwanaharamu, mwizi mkubwa, atahakikisha amemuua kwa njia yoyote ile au atamwagia tindikali afie mbali, maneno ambayo yalisababisha uvunjifu wa amani.Katika kesi hiyo, Upande wa Mashtaka ulikuwa na mashahidi wanne, akiwamo mama mzazi na mshtakiwa alikuwa na mashahidi watatu waliotoa ushahidi wa kumtetea.

Inadaiwa katika utetezi, mshtakiwa alikana kumtukana mama yake na anadai kesi ilitokana na masuala ya biashara na kwamba wanataka aondoke katika familia.Hakimu Mpaze alisema baada ya kupitia ushahidi wa Upande wa Mashtaka, hakuona sababu ya kutoamini ushahidi wa shahidi wa kwanza na mashahidi wengine watatu wa upande huo.

"Nimeshindwa kuona kwamba ushahidi wa shahidi wa kwanza na watatu ni ushahidi wa kutengenezwa."Mshtakiwa alitumia maneno hayo ya kuudhi dhidi ya mama yake hadi kusababisha mama kulia," Hakimu alisema.

Aliendelea kusema mshtakiwa anatambua maneno ya kuudhi na kwamba sio rahisi kuamini kwamba mzazi alikuja mahakamani kutengeneza kesi kwa mtoto wake wa kwanza na kama kuna mgogoro wa biashara, kwa nini mshtakiwa peke yake wakati eneo la biashara lina maduka 20.

"Upande wa Mashtaka umetbibitisha shtaka bila kuacha shaka. Mahakama inamtia hatiani kwa kosa aliloshtakiwa nalo," alisema.Wakili wa Serikali, Nancy Mushumbusi, aliomba mshtakiwa apewe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine kwa kuwa ni mkosaji anayerudia makosa.Wakili Nancy alidai mshtakiwa aliwahi kutiwa hatiani mara mbili katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo kwa makosa kama hayo, akaonywa na sasa ana kesi nyingine inaendelea katika Mahakama ya Mwanzo Ukonga.

Alidai mshtakiwa apewe adhabu kali kwa kuwa ametenda kinyume cha mila na desturi za Kitanzania kwa kumtukana mama yake mzazi ambaye alitoa ushahidi kwa uchungu huku akilia.

Akiomba kupunguziwa adhabu, mshtakiwa alidai ni mama mwenye watoto wanamtegemea, hajaolewa, anapitia changamoto nyingi za kisaikolojia, hivyo aliomba apewe nafasi nyingine atajirekebisha.

Hakimu Mpaze, akitoa adhabu, alisema amezingatia hoja za pande zote mbili na ameona mshtakiwa ni mkosaji wa mara kwa mara."Mshtakiwa angekuwa wa kubadilika, alivyotiwa hatiani asingerudia makosa. Ili iwe fundisho kwake na wengine wanaotukana wazazi wao, mahakama inakuhukumu kwenda jela mwaka mmoja gerezani," Hakimu Mpaze alihitimisha.

Chanzo: ippmedia.com