Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jela miezi sita kwa kukutwa na Bangi gramu 3.12

Bangi Miezi 6 Jela miezi sita kwa kukutwa na Bangi gramu 3.12

Wed, 14 Jun 2023 Chanzo: Mwananchi

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu Robert Sanga (29) kulipa faini ya Sh500,000 au kutumikia kifungo cha miezi sita jela baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na gramu 3.12 za dawa za kulevya aina ya bangi.

Sanga ambaye ni mkazi wa Makongo CCM wilayani Ubongo jijini hapa, amehukumiwa kifungo hicho leo Jumatano Juni 14, 2023, baada ya kukiri shtaka lake wakati kesi yake ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Hata hivyo mshtakiwa huyo ameshindwa kulipa faini hiyo na hivyo atatumikia kifungo hicho.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Pamela Mazengo amesema mshtakiwa ametiwa hatiani kama alivyoshtakiwa.

“Kwa kuwa mshitakiwa umekiri kosa lako mwenyewe, Mahakama inakutia hatiani na kukuhukumu kulipa faini ya shilingi 500,000 kama utashindwa kulipa faini hiyo utatumikia kifungo cha miezi sita gerezani haki ya kukata rufaa iko wazi,” amesema Mazengo.

Kabla ya kutolewa na hukumu hiyo, Mahakama ilimpa nafasi mshtakiwa huyo kujitetea kwanini asipewe adhabu kazi.

Hata hivyo mshtakiwa aliomba mahakama imsamehe na kuahidi kubadilika.

"Mheshiwa hakimu naomba Mahakama yako inisamehe na naahidi nitabadilika, nimejifunza," amesema Sanga.

Awali Wakili wa Serikali, Aboud Yusuph aliieleza mahakama kuwa Februari 18, 2023 asubuhi Jeshi la Polisi Kikosi cha kupambana na dawa za kulevya wakiwa doria walipata taarifa za kiitelejensia kuwa kuna nyumba maarufu kwa jina la kwa Mama Sada wanafanya biashara ya bangi.

Wakili Aboud amedai kuwa kikosi cha askari wakiongozwa na Inspekta Msangi walifika eneo hilo na baadhi ya watu waliokuwepo eneo hilo walikimbia baada ya kuwaona na kufanikiwa kumkamata Sanga akiwa na mfuko wa plastiki na simu nyeusi.

Baada ya kumkamata Sanga aliitwa mjumbe wa eneo hilo, Asha Saidi na kuanza upekuzi ambapo walikuta majani makavu yakiwa katika mfuko huo na baadae mjumbe huyo alisaini fomu ya kukamata mbayo pia ilisainiwa na mshitakiwa na baadae mshitakiwa kupelekwa katika kitengo cha kupambana na dawa za kulevya ambako alikiri kukutwa na bangi.

Aboud alidai kuwa Aprili 19, 2023 Majani hayo yalipelekwa kwa mkemia kwa ajili ya kupimwa na baada ya kufanyika vipimo yaligundulika kuwa ni gramu 3.12 za bangi.

Alidai kesi hiyo ilikuwa na vielelezo vinne ambavyo ni maelezo ya onyo, hati ya kukamata, ripoti ya mkemia pamoja na bangi iliyokamatwa.

hata hivyo, Wakili Aboud alidai kuwa hakuna kumbukumbu ya mshitakiwa kutenda kosa kabla ya kukamatwa na kuiomba mahakama kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria kwa kuwa bangi imekuwa ikileta usumbufu katika jamii na kuharibu nguvu kazi.

Chanzo: Mwananchi