Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jela miaka 90 kwa kunajisi watoto

Sheria Law Jela miaka 90 kwa kunajisi watoto

Wed, 29 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Wilaya ya Kilombero imemhukumu kutumikia kifungo cha miaka 90 gerezani Leonce Matea (55), mkulima na mkazi wa Chicago A', Kata ya Kidatu, wilayani Kilombero, mkoani Morogoro baada ya kupatikana na hatia ya kunajisi watoto watatu.

Hukumu hiyo ilitolewa juzi mahakamani huko na Hakimu Bestina Saning'o baada ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Mkaguzi wa Polisi Thomas Kamsini kuomba kutolewe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa hiyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo za kunajisi watoto.

Mshtakiwa Matea aliomba mahakama kumpunguzia adhabu kwa kuwa umri wake ni mkubwa.

Hakimu Saning'o baada ya kusikiliza maombi ya kila upande, alimtia hatia mshtakiwa huyo na kumhukumu kutumikia kifungo cha miaka 30 gerezani kwa kila kosa aliloshtakiwa kwalo.

Hakimu Saning'o alisema kuwa ili iwe fundisho kwake na wengine, mahakama imemtia hatiana mshtakiwa katika mashtaka yote matatu ya kubaka na kila kosa atatumikia kifungo cha miaka 30, lakini adhabu hizo zinatekelezwa pamoja.

Baada ya kusomwa kwa hukumun hiyo na Hakimu Saning'o, Matea alichukuliwa na kupelekwa katika Gereza la Kiberege.

Novemba 24, 2023, Matea alifikishwa mahakamani huko na kusomewa mashtaka matatu ya kunajisi.

Katika shtaka la kwanza, ilidaiwa kuwa kati ya Juni Mosi, 2023 na Novemba 16, 2023, katika Kijiji cha Chikago, Kata ya Kidatu, Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro, alinajisi mtoto wa miaka tisa (jina limehifadhiwa).

Katika shtaka la pili, tarehe hizohizo na eneo lilelile, Matea anadaiwa kunajisi mtoto mwenye umri wa miaka 10 (jina limehifadhiwa).

Na katika shtaka la tatu, ilidaiwa kuwa kati ya Novemba Mosi, 2024 na Novemba 16, 2023 , Matea alinajisi mtoto mwenye umri wa miaka mitano (jina limehifadhiwa).

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Matea alikana kutenda makosa hayo. Upande wa Jamhuri ulipeleka mashahidi 12 wakiwamo na waathirika wa shauri hilo.

Hata hivyo, Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura 16, inaelekeza adhabu ya kifungo cha maisha gerezani kwa anayepatikana na hatia ya kunajisi mtoto mwenye umri chini ya miaka 10.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live