Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jela miaka 3 kwa kuvunja nyumba, kuiba

Jela (1).webp Jela miaka 3 kwa kuvunja nyumba, kuiba

Thu, 14 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kinondoni, jijini Dar es Salaam imemhukumu, Omary Sadiki, kwenda jela miaka mitatu baada ya kukutwa na hatia ya kosa la wizi wa mali yenye thamani ya Sh. milioni 3.1.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi, Lilin Silali, aliyesikiliza kesi hiyo.

Alisema bila kuacha shaka upande wa Jamhuri umethibitisha makosa dhidi ya mshtakiwa na mahakama hiyo inamtia hatiani katika makosa yote mawili, ikiwamo kuvunja nyumba na kosa la wizi.

"Mshtakiwa utakwenda jela miaka miwili kwa kosa la kwanza na kosa la pili la wizi mshtakiwa atakwenda jela mwaka mmoja, adhabu yote itakwenda sambamba," alisema Hakimu Silali.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa Septemba 24, 2018 Tandale Muhalitani, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, alivunja nyumba ya Mohamed Juma na kuingia ndani kwa lengo la kuiba.

Ilidaiwa kuwa mshtakiwa aliiba luninga moja, sabufa, king'amuzi cha Startimes, deki na Sh. 3,192,000 mali ya Juma.

Ilidaiwa mahakamani hapo kwamba, siku ya tukio, mshtakiwa alikamatwa na askari wa doria saa tisa usiku akiwa na vitu hivyo alivyobeba katika kiroba.

Ilidaiwa kuwa mshtakiwa alipohojiwa hakuwa na majibu sahihi na alikiri kwamba vitu hivyo ameiba.

Upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi wawili na wakati wa utetezi, mshtakiwa alichagua kukaa kimya ili mahakama iamue na ndipo mahakama ilipoona mshtakiwa alitenda makosa hayo.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali Ester Chale, aliiomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine licha ya kutokuwa na historia ya makosa hapo nyuma.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live