Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jela miaka 20 kwa kukutwa na meno ya Kiboko, Tembo

88744 Jela+pic Jela miaka 20 kwa kukutwa na meno ya Kiboko, Tembo

Mon, 16 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar Es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam nchini Tanzania imemhukumu, Haika Mgao (26) kutumikia kifungo cha miaka 60 jela baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na meno ya tembo na ya kiboko yenye thamani ya Sh69.5 milioni, mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mgao ambaye ni mkazi wa Kimara Saranga, Dar es Salaam alikuwa anakabiliwa na mashtaka matatu katika kesi ya uhujumu uchumi namba 69/2018.

Miongoni mwa mashtaka hayo ni kukutwa na vipande vya meno ya tembo na kiboko, bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Akisoma hukumu iliyoandaliwa na Hakimu Kelvin Mhina, leo Jumatatu Desemba 16, 2019 Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Godfrey Isaya amesema mshtakiwa ametiwa hatiani kama alivyoshtakiwa.

Amesema upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi watatu ambao walithibitisha mashtaka hayo bila kuacha shaka.

Hakimu Isaya amesema ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaojihusisha na vitendo hivyo, mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka 20 jela, baada ya kutiwa hatiani katika shtaka la kukutwa na vipande vinne vya meno ya tembo yenye thamani ya Sh66.2 milioni.

"Pia, katika shtaka la kukutwa na meno mawili ya kiboko yenye thamani ya Sh3,310,500, Haika utatumikia kifungo cha miaka 20 jela na shtaka la tatu ambalo ni kujihusisha na biashara ya nyara za Serikali, utatumikia kifungo cha miaka 20 jela" alisema Hakimu Isaya.

Hata hivyo, Hakimu Isaya alifafanua adhabu hiyo kuwa inakwenda kwa pamoja, hivyo Haika atatumikia kifungo cha miaka 20 jela na kwamba kama hajaridhika na hukumu hiyo anaweza kukata rufaa.

Awali, kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon aliiomba mahakama hiyo itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo kutokana na tembo kupotea kwa sababu ya ujangili jambo ambalo linaathiri uchumi wa nchi.

"Mheshimiwa hakimu naiomba mahakama yako itoe  adhabu kali kwa  mshtakiwa huyu hasa ukizingatia mali asili zetu hususan tembo wanapotea kwa ujangili jambo ambalo linaathiri uchumi wetu moja kwa moja," alidai Simon.

 

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa alikuwa anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 69/2018 kwa kujihusisha na biashara ya meno ya tembo na Kiboko

Haika anadaiwa kutenda makosa hayo, Novemba 19, 2015 katika eneo la Kimara, wilaya ya Kinondoni.

Anadaiwa katika shtaka la kwanza, siku na eneo hilo, mshtakiwa alikutwa na vipande vinne vya meno ya tembo vyenye thamani ya dola za kimarekani 30,000 sawa na Sh66.2 milioni, bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Pia, siku na eneo hilo, Haika alikutwa na meno mawili ya kiboko yenye thamani ya dola za kimarekani 3, 310,500, bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Katika shtaka la tatu, mshtakiwa  anadaiwa kujihusisha na biashara ya nyara za Serikali, bila kuwa na leseni kutoka Mamlaka husika.

Chanzo: mwananchi.co.tz