Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jela miaka 20 kwa kukutwa na kilo 32 za nyama ya Tandala

Mbaroniii Nyamapori.png Jela miaka 20 kwa kukutwa na kilo 32 za nyama ya Tandala

Tue, 5 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Wilaya ya Mufindi, imemhukumu Mbogo Tinda (45), Mkazi wa Kijiji cha Ihoanza Tarafa ya Malangali, wilayani hapa, kutumia kifungo cha miaka 20 gerezani, baada ya kumtia hatiani kwa makosa mawili.

Makosa hayo ni lile la kukutwa na nyara za Serikali (nyama ya Tandala – Kudu, yenye uzito wa kilo 32), lakini pia kujihusisha nyara za Serikali bila kuwa na kibali.

Hukumu hiyo imetolewa jana September 4, 2023; na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Benedict Nkomola, ambapo imedaiwa mshtakiwa huyo alipatikana na nyama ya Tandala yenye thamani ya Sh7, 859, 136 milioni.

Akisoma shtaka hilo, hakimu huyo amesema mnamo August 26, 2023 katika Kijiji cha Idope, Kata ya Ihoanza, wilayani hapa, mshtakiwa huyo alikutwa na nyama ya Tandala ambayo alikuwa anaiuza bila kuwa na uhalali wa kufanya shughuli hiyo.

Inadaiwa kuwa mshtakiwa alinunua na kuuza nyama ya Tandala kilo 32, yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha ambayo ni mali Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kuwa na vibali au leseni ya kuuza nyama hiyo.

Pia hakimu huyo amesema kosa hilo ni kinyume na kifungu namba 86(1) (2) (a) na kifungu (3) cha sheria ya uhifadhi wa wanyapori sura 283 rejeo la Mwaka 2022, ikisomwa pamoja na aya ya 14 Jedwari la kwanza la vifungu vya 57(1), na 60 (1) (2) vya sheria ya makosa ya uhujumu uchumi na makosa ya kupangwa, sura 200 rejeo la Mwaka 2022.

Aidha katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 11, 2023; mshtakiwa alikiri kutenda makosa hayo, ndipo mahakama ikamtia hatiani na kumhukumu kwenda jela miaka 20 kwa kosa la kwanza na pili ambapo adhabu hizo zitaenda sambamba.

Awali akizungumza kabla ya kutolewa hukumu hiyo, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Ahmad Magenda, aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa.

"Niombe mahakama yako itoe adhabu kali kwa washtakiwa wote ambao wanafanya makosa kama haya ya kuhujumu wanyapori ambao ni vivutio kwa watalii, sanjari na kukuza pato la mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla," amesema Magenda.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live