Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, imemhukumu kifungo cha miaka 10 jela, Mkami Shirima, baada ya kumkuta na hatia ya kumuua bila kukusudia, aliyekuwa msaidizi wake wa ndani ‘house girl,’ Salome Zakaria (18), kwa madai kuwa alimuibia fedha alizokuwa ameweka kwenye ‘kibubu.’
Shirima ambaye ni mfanyabiashara, anadaiwa kumuua msaidizi wake kwa kumpiga na rungu, kumfungia ndani akimtuhumu kuwa alimuibia Sh2.5 milioni, alizokuwa amehifadhi kwenye kibubu hicho.
Hadi anatiwa hatiani na kupewa adhabu hiyo, mshitakiwa amekaa gerezani kwa muda wa miaka mitatu na miezi saba, na hii inatokana na sababu mbalimbali ikiwemo kusubiria kukamilika kwa upelelezi wa shauri hilo.
Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Aisha Bade, ametoa hukumu hiyo baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili za kesi hiyo.
Katika shauri hilo la mauaji namba 111/2022, Jaji Aisha amesema mshitakiwa alitenda kosa hilo Machi 6, 2020; nyumbani kwake, maeneo ya Mianzini, jijini Arusha, na shauri hilo lilianza kusikilizwa na mahakama hiyo Mei 23, 2023.
Amesema baada ya mahakama kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, imemkuta na hatia ya mauaji bila kukusudia kinyume na kifungu cha 195 cha kanuni ya adhabu, na kuwa mahakama baada ya kumtia hatiani mshitakiwa ina wajibu wa kutoa adhabu itakayoendana na kosa lililofanyika.
“Ukatili wa kijinsia kwenye jamii umezidi, upande wa utetezi waliomba mahakama imhurumie mteja wake kwa sababu mazingira ya kesi yanaonyesha alikuwa anajaribu kupata fedha zake alizoamini zimeibiwa na marehemu na kwamba mshtakiwa alimpeleka marehemu hospitali,” amesema Jaji Aisha na kuongeza;
“Mshitakiwa alitaka hadi kutoa damu ili kuokoa maisha ya marehemu, hivyo alijutia kosa lake japo hakukiri kisheria ila alikiri kwa mantiki kuwa alimpiga kwa ajili ya kumuadabisha na alieleza zaidi ni mama wa watoto watatu na mtoto wake mdogo ana miaka mitano, anahitaji matunzo ya mama yake.”
Jaji huyo amesema kwa kuangalia sababu zote zilizotolewa, silaha (rungu) ilitumika kumuumiza marehemu na kwa kuangalia ukweli marehemu alikuwa binti mdogo, na kwamba ndiyo kwanza alikuwa anaanza maisha yake.
Kwa mujibu wa jaji huyo, marehemu angeweza kuchangia katika jamii na nchi yake na kwamba alikuja kwa ajili ya kufanya kazi ili ajikimu, na familia yake ilikuwa inamtegema, hivyo mambo yote yanapaswa kuzingatiwa wakati tunatoa adhabu.
“Maoni yangu ni kama ifuatavyo, wasaidizi wengi wa kazi za ndani nchini, japo wana majukumu makubwa katika familia wankofanya kazi hizo, lakini wamekuwa wakinyanyaswa sana na waajiri wao...wanafanya kazi masaa mengi wanalipwa kidogo, hii ni kesi ni moja wapo ya yanayotokea kwenye jamii,” amesema Jaji Aisha na kuongeza;
“Huyu binti walimfungia ndani na ripoti zinaonyesha alipofungiwa hakupewa chakula jambo ambalo limegharimu maisha yake na akiwa amepigwa, hayo yote ni kutokana na kudaiwa ameiba fedha hizo, na hata kama ameiba mshitakiwa hakuwa na haki ya kumuadhibu kiasi hicho.”
“...kwa kuzingatia hayo yote ninamhukumu mshitakiwa kifungo cha miaka 10 jela ili iwe fundisho kwa wegine wenye tabia ya kuonea na kunyanyasa wafayakazi wa nyumbani, hasa ikizingatiwa wafanyakazi hao, hawana msaada wowote,” amesema jaji huyo.
Kwa kuwa mshitakiwa alishakaa rumande, Jaji Aisha amesema: “Mshtakiwa ana haki ya kupunguziwa adhabu ya kifungo (muda aliokaa unahesabika kwenye adhabu hiyo) na kifungo kinaanza mara moja.
Awali Mkami anadaiwa kuwa Machi 6, 2020 mshitakiwa akiwa nyumbani kwake alienda kwenye kibubu chake alichokuwa amehifadhi hela na kukuta kimevunjwa ambapo alimuita mtoto wake pamoja na marehemu na kuwauliza nani amevunja na kuchukua fedha zake ambapo wote wawili walikana.
Ilidaiwa kuwa alianza kuwachapa ndipo mtoto wake akadai kuwa marehemu alikivunja na wakagawana fedha ambapo alichukua Sh100,000, wakagawana na kwamba Shirima alichukua kirungu kilichokuwa ndani na kuanza kumpiga marehemu kuanzia Machi 6 hadi 8,2020,
Inadaiwa pia licha ya kipigo hicho, mshtakiwa alimfungia marehemu kwenye moja ya vyumba vya ndani kwake kabla ya kumpeleka hospitali baada ya kuzidiwa.
Ilidaiwa kuwa Machi 8, mtoto wa mtuhumiwa huyo alimweleza mama yake kuwa Salome hali yake imekuwa mbaya ndipo walipoamua kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya Mt Meru, ambapo binti huyo baadae alifariki.
Na kwamba Machi 10, 2020 mtuhumiwa alitoa maelezo yake, alikamatwa na kufunguliwa jalada ya shambulio la kudhuru mwili.
Baada ya kufanyika upekuzi katika nyumba ya Shirima ambapo miongoni mwa vielelezo vilivyochukuliwa nyumbani kwake na vilivyotolewa mahakamani hapo ni kibubu hicho cha mbao kilichokuwa kimevunjwa, noti moja ya Sh 10,000 iliyokuwa imekatika vipande vitatu, godoro lililokuwa na damu pamoja na kirungu.
Katika kesi hiyo ya mauaji upande wa mashitaka uliokuwa ukiwakilishwa na mawakili watatu wa jamhuri wakiongozwa na Wakili Charles Kagirwa, ilikuwa na mashahidi sita huku mshitakiwa akijitetea mwenyewe bila kuwa na shahidi mwingine.