Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jela maisha kwa kumbaka mtoto akimfundisha kuogelea

Kifungo Jela maisha kwa kumbaka mtoto akimfundisha kuogelea

Thu, 1 Sep 2022 Chanzo: Mwananchi

Mahakama ya Wilaya Kinondoni jijini Dar es Salaam, imemhukumu Dunia Suleman (36) maarufu P squre, kutumikia kifungo cha maisha jela, baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka binti wa miaka nane.

Suleman, ambaye ni Beach Boy na mkazi wa Msasani wilaya ya Kinondoni, anadaiwa kumbaka binti huyo wakati akimfundisha kuogelea katika ufukwe wa Coco, uliopo Bahari ya Hindi.

Mshtakiwa huyo amehukumiwa kifungo hicho na Hakimu Mkazi Mkuu, Erick Rwehumbiza, baada ya mshtakiwa huyo kukiri shtaka lake.

Pia, Mahakama hiyo imetoa amri tube ya tairi ya gari, iliyotumika kutendea kosa hilo, iharibiwe.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Rwehumbiza alisema mshtakiwa ametiwa hatiani kama alivyoshtakiwa.

“Mahakama imekutia hatiani kama ulivyoshtakiwa baada ya kukiri shtaka la kubaka mtoto, hivyo utatumikia kifungo cha maisha jela ili iwe fundisho kwa wenzako,” alisema Rwehumbiza.

Advertisement Awali, Wakili wa Serikali, Michael Shindai, aliiomba mahakama itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa kwa kuwa vitendo vya ubakaji watoto vimekuwa vikiongezeka kila siku.

“Mheshiwa hakimu, kwa kuwa mshtakiwa amekiri shtaka lake mwenyewe bila kulazimishwa na mtu, naomba mahakama yako itoe adhabu kali kukomesha vitendo hivi,” alidai Shindai.

Pia upande wa mashtaka uliwasilisha vielelezo vinne ambavyo ni fomu ya PF3, maelezo ya onyo ya shahidi, hati ya gwaride la utambuzi na hati ya kuchukulia mali ambayo ni tube ya tairi la gari lilitumika kutendea kosa.

Kabla ya kupewa adhabu hiyo, Mahakama hiyo ilitoa nafasi kwa mshtakiwa kujitetea kwa nini asipewe adhabu kali.

Hata hivyo, mshtakiwa aliomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa ni kosa lake la kwanza na kwamba alipitiwa na shetani.

“Naomba mama wa mtoto huyu, anisamehe sana, nilipitiwa na shetani, naomba msamaha,” alidai mshtakiwa.

Hakimu Rwehumbiza alitupilia mbali maombi ya mshtakiwa huyo na kumhukumu kifungo cha maisha jela.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, P square anakabiliwa na kesi ya jinai namba 183/2022.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Agosti 13, 2022 katika ufukwe wa Coco, uliopo wilaya ya Kinondoni.

Inadaiwa siku hiyo ya tukio, Suleman anadaiwa kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 8, kinyume na kifungu 130(1)(2)e na kifungu 131(1) cha kanuni ya adhabu.

Wakili Shindai alidai kuwa mshtakiwa alipewa watoto wawili wa familia kuwafundisha kuogelea, lakini badala ya kuwafundisha alimchukua binti huyo na kumpeleka baharini na kisha kumbaka.

Hata hivyo mshtakiwa baada ya kusomewa shtaka lake, alikiri na ndipo mahakama hiyo ilipomtia hatiani.

Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alifikishwa katika Mahakama hiyo, Agosti 24 mwaka huu kujibu shtaka hilo.

Chanzo: Mwananchi