Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu aliyekuwa fundi Sanifu Maabara ya Afya, Chuo cha Maji, Habib Mnkumbi (33) kifungo cha miaka miwili jela, baada ya kupatikana na hatia ya kughushi vyeti vitatu kikiwemo cha Chuo Kikuu cha Tumaini, Makumira.
Mshtakiwa anadaiwa kughushi cheti cha Diploma ya Afya na cheti cha Maabara ya Afya kutoka chuo Cha Tumaini Makumira na kile Hospitali ya KCMC (KCMU-Co)
Hukumu hiyo imetolewa leo, Juni 28, 2023 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Evodia Kyaruzi, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya hukumu.
"Mahakama imeridhishwa na ushahidi wa mashahidi saba uliotolewa mahakamani hapa akiwemo Mkuu wa Chuo cha Tumaini Makumira, Dk Alex Malasusa, hivyo mahakama inakuhukumu kifungo cha miaka miwili jela," amesema Hakimu Kyaruzi.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Fatuma Waziri akishirikiana na Veronica Chimwanda, waliomba mahakama hiyo itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo, kwa kuwa ameaibisha vyuo hivyo, lakini amefanya kazi ambayo hajaisomea.
"Mheshimiwa hakimu tunaomba mahakama itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo, kwa sababu kazi hii hajasomea lakini alikuwa anatoa huduma, je huduma hizo zimathiri watu wangapi? Amehoji Wakili Waziri.
Mshtakiwa alikuwa anakabiliwa na mashtaka sita ya kughushi vyeti vya kitaaluma na kuviwasilisha Chuo cha Maji akionyesha kuwa amesoma kozi hizo katika vyuo hivyo na kupewa vyeti, wakati akijua kuwa ni uongo na hajawahi kusome kozi hizo.