Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Je, hizi zaweza kuwa sababu kukithiri kwa mauaji nchini?

Kisu Damu Hizi hapa Sababu za kukithiri kwa mauaji nchini

Sun, 23 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Unaweza kujuliza ni nini kinasababisha kukithiri kwa matukio mengi ya mauaji hapa nchini kwa sasa? kila kukicha vyombo vya habari vimekuwa vikitangaza matukio haya kana kwamba ni mambo ya kawaida ama utamaduni wetu.

Kukithiri kwa matukio haya kumemuibua Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya Jinai nchini DCI, Camillius Wambura ambaye ameweka bayana sababu zinazochochea majanga hayo.

DCI amefunguka kusema kuwa vitendo na imani za kishirikina, uchu wa kupata mali, wivu wa mapenzi, migogoro ya kifamilia na ardhi vimekuwa sehemu kubwa ya kutokea kwa matukio hayo ya kikatili.

Akifafanua kuhusu imani za kishirikiana na wivu wa mapenzi amesema mara nyingi watu wamekuwa wakipotoshwa na waganga wa kienyeji kwa kuwataja watu wao wa karibu kuwa ni wachawi jambo ambalo limekuwa likiibua hasira na hisia kali hadi kupelekea mtu kufanya mauaji kwa mke, mume au wazazi wake huku akiamini kuwa amemaliza tatizo.

Kuhusu wivu wa mapenzi amesema kuwa kukosekana kwa uaminifu, na upendo wa dhati mara nyingi hupelekea mauaji ambayo huacha uchungu kwa familia zote za walengwa.

Kwenye migogoro ya kifamilia na ardhi, hapa DCI amesema kuwa kukosekana kwa usuluhishi thabiti kumepelekea mauaji ya wengi, migogoro hiyo ambayo huusisha familia moja na nyingine, ndugu wa familia moja imekuwa ikiacha alama ambazo ni ngumu kufutika.

Ameongeza kwa kufafanua kuhusu sababu nyingine ambayo ni tamaa za mali, kwa kusema kuwa watu wengi wamekua wakitamani utajiri wa haraka hivyo kuwapelekea kufanya maamuzi ambayo hayana mantiki kama mauaji ili waweze kurithi mali.

Itakumbukwa kuwa, siku za hivi karibuni kumetangazwa kuhusu binti aliyemuua mama yake mazazi mkoani kilimanjaro kisha kumzika huku lengo likiwa ni kujipatia mali na utajiri.

Sanajari na hayo ametoa muongozo wa kile anachoamini kuwa kitasaidia kukomesha matukio hayo ya kikatili zaidi katika jamii zetu kwa kusema kuwa viongozi wa dini wasisitize zaidi kuhusu maadili na njia ambazo zinawapasa watu kuishi ili kujitoa kwenye tamaa zisizo na mantiki na tija kwa taifa kwa ujumla.

Amesisitiza pia kuhusu malezi bora yenye misingi na tamaduni za kiafrika ikiwa ni pamoja na wazazi kutenga muda wa kushiriki katika malezi ya watoto wao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live