Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jalada la raia 19 bado lipo kwa DPP

17906 Pic+jalada TanzaniaWeb

Wed, 19 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Jalada la kesi ya uhujumu uchumi  inayowakabili raia 19 wa China na Watanzania sita katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Hayo yameelezwa leo Septemba 18, 2018 na Wakili wa Serikali, Patrick Mwita mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huduma Shahidi wakati kesi hiyo ilipopangwa kwa kutajwa.

Wakili Mwita alieleza mahakamani hapo washtakiwa wote wapo mahakamani, kesi ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na kwamba jalada halisi la kesi hiyo lipo katika ofisi ya DPP linafanyiwa kazi hivyo waliomba ipangiwe tarehe nyingine ili waweze kutoa taarifa wamefikia wapi.

Miongoni mwa mawakili wa utetezi wanaowatetea washtakiwa hao ni Majura Magafu, Peter Kibatala, Jeremiah Mtobesya, Steven Bwana, Steven Mosha, Wallace Mfuko na Peter Isaya.

Kibatala kwa niaba ya jopo hilo la mawakili wa utetezi aliomba kesi hiyo ipangiwe siku saba ili upande wa mashtaka uweze kukamilisha taratibu zao na kesi iweze kuendelea kusonga mbele.

Baada ya kusikiliza hoja hizo Hakimu Shaidi aliiahirisha kesi hiyo hadi Septemba 25,2018 na kuutaka upande wa mashtaka ufikie na maelekezo sahihi siku hiyo.

Washtakiwa hao wanashtakiwa chini ya vifungu vya sheria ya uhamiaji, chini ya sheria ya watu ambao siyo raia wa Tanzania na uhujumu uchumi.

Washtakiwa hao  ni, Bo Song, Liu Yunley, Chen Chao Hui, Fu Zeng, Wu Hai Quing, Ke Qiu Fang, Frederick Kumalija, Jing Jing Lin, Ku Liao, Yan Yan Geng, Chen Ying Gong, Salim Mahsein Al-Amry, George Elikana, Fatuma Songoro, Bhoke Mwita, Kelvin Ponela, Chen Gwandi, Lin Ben, Rui Guo, Lin Xiangqui, Chen Fa, Wan Li, Robert Mkini na Revocatus Mugisha.

Inadaiwa kati ya Juni Mosi, 2017 na Mei 18, 2018 washtakiwa hao walitenda kosa chini ya sheria ya watu ambao siyo raia wa Tanzania kwa kutoa taarifa za uongo kwa lengo la kupata kibali cha kufanya kazi nchini.

Katika shtaka la pili inadaiwa kutoa taarifa za uongo kwa kamishna wa kazi kwa lengo la kupata vibali vya kufanyia kazi.

Katika shtaka la tatu, mshtakiwa Bo Song anadaiwa alijihusisha na kazi nchini bila ya kuwa na hati ya kuishi nchini. 

Katika shtaka la nne,  washtakiwa, Kumalija, Mwita, Songoro, Ponela, Mkini na Mugusha wanadaiwa kuwa kati ya Juni Mosi, 2017 na Mei 17, 2018 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, walimsaidia raia wa China, Bo Song kujihusisha na kazi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku wakijua kuwa hana kibali cha kuishi nchini wala kufanya kazi.

Katika shtaka la tano, washtakiwa wote wanadaiwa kuandaa, kusimamia na kusaidia kutoa taarifa za uongo kwa dhumuni la kujipatia kibali cha kufanya kazi na kuishi nchini.

Pia, washtakiwa wote kinyume na sheria ya uhujumu uchumi wanadaiwa walijihusisha na makosa ya udanganyifu kwa kuonyesha kwamba walikuwa na vibali vya kuishi nchini Tanzania kutoka idara ya uhamiaji na vibali vya kufanya kazi kutoka kwa Kamishna wa kazi nchini huku wakijua kuwa siyo kweli

Hata hivyo, washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi na washtakiwa wapo rumande.

Chanzo: mwananchi.co.tz