Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jalada la Mbowe larejeshwa Kisutu

9464 Mboeee+pic Jalada la Mbowe larejeshwa Kisutu

Thu, 14 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imerejesha jalada la kesi ya jinai ya uchochezi dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake kwenda Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kukusanya na kuandika mwenendo mzima wa kesi hiyo.

Kadhalika, mahakama hiyo imesema kama kuna mwenendo wa mahakama nyingine tofauti na Kisutu utengwe pembeni.

Amri hiyo ilitolewa jana na Jaji Ilvin Mgeta baada ya kusikiliza hoja za walalamikiwa kwamba wamepokea mwenendo, lakini nyaraka zake hazijatimia.

Alisema mahakama yake inaamuru jalada hilo kurejeshwa Mahakama ya Kisutu ikakusanye mwenendo jana na leo kuanzia kesi ilipoanza mpaka mwisho wa hukumu yake.

"Naagiza jalada hili lirejeshwe Mahakama ya Kisutu leo na kesho (jana na leo), wakakusanye mwenendo tangu kesi ilipoanza mpaka ilipotolewa hukumu, Ijumaa Mei 15, mwaka huu jalada lirejeshwe hapa ili pande zote mbili mpate nakala za mwenendo huo, Jumatatu Mei 18, mwaka huu tukutane hapa saa tatu asubuhi kuanza kusikiliza," alisema Jaji Mgeta.

Mapema mahakamani hapo, Wakili wa walalamikiwa, Peter Kibatala, alidai kuwa walalamikaji watano akiwamo, Mwenyekiti Taifa, Mbowe, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu, Visiwani Zanzibar, Salum Mwalimu, Katibu Mkuu, John Mnyika na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche walikuwapo mahakamani.

Kibatala alidai kuwa walalamikaji, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, wa Kawe, Halima Mdee na wa Bunda Ester Bulaya, wameshindwa kufika mahakamani kwa sababu ya matatizo ya afya zao.

Kibatala alidai kuwa walalamikaji wameridhia rufani hiyo kuendelea kusikikizwa bila uwapo wao. Upande wa walalamikiwa ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraji Nchimbi, akisaidiana na Wakili wa Serikali Salimu Msemo, ulidai kuwa kuendelea na kusikiliza rufani bila uwapo wa walalamikaji watatu hawana pingamizi wanaiachia mahakama.

Hoja ya walalamikiwa inajikita kwamba nyaraka walizopatiwa na Mahakama Kuu haziko sawa, zina kasoro ili waweze kuitetea rufani ya walalamikiwa dhidi yao.

Alidai kuwa katika hatua za usikilizwaji zilipitiwa na mahakimu wawili tofauti na kutakiwa kuwa na kurasa kati ya 566 au zaidi.

"Mtukufu jaji, katika nakala ya mwenendo tulionao unaonyesha kurasa namba 141 mpaka 570 zimethibitishwa na katika hukumu kurasa namba moja mpaka 104 zimethitishwa pia, hoja zetu hizo tunaomba kuahirishwa kusikilizwa rufani hii," alidai Nchimbi.

Akijibu hoja za walalamikiwa, Kibatala alidai kuwa mawakili wote walishiriki kesi hiyo tangu inaanza mbele ya Jaji (wakati huo akiwa Hakimu), Wilbard Mashauri.

Alidai kuwa wao ni, maofisa wa mahakama na Aprili 28, mwaka huu, Jaji Mfawidhi, Lameck Mlacha, rufani hiyo ilipotajwa mbele yake aliwauliza kama kuna yeyote anayepinga, lakini pande zote mbili zilieleza ziko tayari kuanza kusikiliza jana.

Mei 11, mwaka huu nilipata barua kutoka kwa Jaji Mfawidhi akisisitiza kwamba wafike mahakamani kwa ajili ya kusikiliza rufani hiyo.

"Tunapinga maombi ya walalamikiwa ya kutaka ahirisho, mahakama iwe na ukali kusimamia amri zake, kama itaahirishwa iwe kwa muda mfupi ili tuendelee na kusikiliza rufani hii," alidai Kibatala.

Jaji alisema mahakama yake imepokea majibu ya barua ya Mei 11, mwaka huu, kutoka kwa walalamikiwa wakielezea kasoro zilizopo kwenye mwenendo wa kesi hiyo kutoka Mahakama ya Kisutu mfano; hakuna mwenendo wa Februari 24, mwaka huu na kuendelea.

Mbowe na wenzake wamekata rufani Mahakama Kuu kupinga hukumu ya kulipa faini ya jumla ya Sh. milioni 320 au kwenda jela miezi mitano kwa kila kosa.

Rufani hiyo iliyosajiliwa kwa namba 76 mwaka huu imewasilishwa na wakili wa walalamikaji, Peter Kibatala ikiwa na sababu 14. Kwa mujibu wa hati ya rufani, walalamikaji wanadai kuwa Mahakama ya Kisutu, ilikosea kuwatia hatiani Mbowe na wenzake kwa sababu haikuchambua ushahidi wa Jamhuri wakati wa kuandika hukumu hiyo.

Hoja nyingine, Mahakama ya Kisutu katika hukumu yake haikuonyesha sababu za washtakiwa kutiwa hatiani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live