Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jalada kesi ya mchunguzi wa Takukuru latua kwa DPP

Jalada kesi ya mchunguzi wa Takukuru latua kwa DPP

Sun, 9 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Jalada la kesi ya kuomba rushwa ya Sh200 milioni inayomkabili aliyekuwa mchunguzi mkuu wa Takukuru,  Cosmas Batanyita lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP).

Batanyita anakabiliwa na mashtaka saba likiwemo la kuomba rushwa na kutakatisha fedha katika kesi ya uhujumu uchumi namba 76/2019.

Wakili wa Serikali, Faraji Nguka ameieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Februari 7, 2020 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Mbele ya Hakimu Mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo, Godfrey Isaya, amesema kuwa jalada hilo kabla ya kupelekwa kwa DPP lilirudishwa polisi kutokana na baadhi ya maeneo kuhitaji kufanyiwa uchunguzi wa ziada.

 “Jalada la kesi hii kwa sasa lipo kwa mkurugenzi wa mashtaka kwa ajili ya kulipitia na kulitolea uamuzi. Upelelezi upo hatua za mwisho kukamilika, tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” amedai Nguka.

Hakimu Isaya baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 21, 2020 itakapotajwa.

Pia Soma

Advertisement
Mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na mashtaka ya kutakatisha fedha yanayomkabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Mshtakiwa alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Agosti 9, 2019 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 76/2019.

Kati ya mashtaka hayo saba, matatu ni ya kushawishi rushwa, moja la kuomba na kupokea rushwa na mashtaka matatu  ya kutakatisha fedha.

Katika kesi ya msingi, Batanyita akiwa mwajiriwa wa Takukuru anadaiwa Februari 9, 2019 katika eneo la Upanga alishawishi na kuomba rushwa  ya Sh200 milioni kutoka kwa Hussein Gulamal Hasham ili aweze kuharibu ushahidi katika kesi ya ukwepaji wa kodi ilivyokuwa inamkabili Husein wakati akijua  kuwa upelelezi wa kesi hiyo ulikuwa unaendelea Takukuru.

Anadaiwa Februari 10, 2019 katika eneo la Sabasaba, Batanyita alijipatia Dola 20,000  za Marekani kutoka kwa Faizal  Hasham ikiwa ni ahadi ya kuharibu ushahidi katika kesi ya ukwepaji kodi inayomkabili Hussein Hasham, wakati akijua upelelezi wa kesi hiyo ulikuwa unaendelea.

Chanzo: mwananchi.co.tz