Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jalada kesi ya Ndama kwa DPP

60372 Pic+ndama

Thu, 30 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Jalada la  kesi ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu inayomkabili mfanyabiashara, Ndama  Hussein maarufu kama Pedeshee Ndama Mtoto ya Ng'ombe lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini ( DPP) kwa ajili ya kulipitia na kulitolea maamuzi.

Wakili wa Serikali, Glori Mwenda ameieleza hayo leo Jumatamo Mei 29 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Maira Kasonde wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mwenda alieleza kuwa kesi hiyo ilikwenda makakamani hapo kwa ajili ya kutajwa na kwamba jalada lake lipo kwa DPP kwa ajili ya kupitiwa.

"Jalada halisi la kesi hii lipo kwa DPP kwa ajili ya kulipitia na kulitolea maamuzi, hivyo tunaomba tarehe  nyingine ili tuje tuieleze Mahakama kuwa shauri hili lipo katika hatua gani" alieleza Mwenda.

Baada ya upande wa mashtaka kueleza hayo, wakili wa Ndama, Jeremiah Mtobesya alilalamika kuwa kesi hiyo ni ya muda mrefu na ina muondolea uhuru mshtakiwa asiweze kufanya mambo yake ya msingi.

" Naamini tarehe ijayo mtakuja na majibu juu ya jalada hilo lipo hatua gani" alisema Mtobesya.

Pia Soma

Hakimu Kasonde baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, aliutaka upande wa mashtaka kufuatilia jalada hilo ili kujua limefikia  hatua gani.

"Nawakumbusha tena, shauri hili limechukua muda mrefu na mpaka sasa bado kesi hii haijaanza kusikilizwa ushahidi licha ya upelelezi kukamilika na mshtakiwa kukiri baadhi ya mashtaka na kupigwa faini," alisema Hakimu Kasonde na kuongeza:

"Ni vizuri upande wa mashtaka tarehe ijayo mje na majibu kuhusiana na hilo jalada lipo katika hatua gani."

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Kasonde aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 14  itakapotajwa na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.

Ndama  anakabiliwa na mashtaka matano, yakiwemo ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu katika kesi ya jinai namba 442/2016.

Miongoni mwa mashtaka yanayomkabili ni, Februari 20, 2014 Dar es Salaam anadaiwa kughushi nyaraka ya kibali cha kusafirisha madini na sampuli za madini kwa kusudi la kuonyesha kuwa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited iliruhusiwa kusafirisha maboksi manne ya dhahabu yenye kilogramu 207 yenye thamani ya Dola za Marekani 8,280,000 kwenda nchini Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited wakati akijua si kweli.

Pia, Machi 6, 2014 jiji Dar es Salaam nadaiwa kughushi kwa kutengeneza hati ya kibali ya Umoja wa Mataifa ofisi ya Dar es Salaam akijaribu kuonesha kilogramu 207 za dhahabu kutoka nchini Congo zinatarajiwa kusafirishwa na kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited kwenda nchini Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited zimesafirishwa bila jinai yoyote wakati akijua si kweli.

Ndama anadaiwa pia kati ya Februari 26 na Machi 3, 2014, Dar es Salaam kwa njia ya udanganyifu alijipatia kutoka kwa kampuni ya nchini Australia ya Trade TJL DTYL Limited kiasi cha  Dola za Marekani 540,000 baada ya kudanganya kuwa atawapa na kusafirisha dhahabu hizo.

Chanzo: mwananchi.co.tz