Dar es Salaam. Jalada la kesi ya kuisababishia Serikali ya Tanzania hasara ya Sh1.175 bilioni, inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu na wenzake watano, limepelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini( DPP) kwa ajili ya kulipitia.
Maimu na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 100, katika kesi ya uhujumu uchumi namba 7/2019, iliyopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Wakili kutoka Takukuru, Leonard Swai ameieleza mahakama hiyo, leo Jumanne Juni 25 2019, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.
Simon amedai mbele ya Hakimu Mkazi, Salum Ally kuwa, jalada la kesi hiyo limerudishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya kulipitia na kukamilisha upelelezi.
" Hivyo, kutokana na hali hii tunaiomba mahakama yako ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa" alidai Swai.
Katika hatua nyingine, mahakama hiyo imemruhusu mshtakiwa wa sita katika kesi hiyo, Sabina Raymond kusafiri nje ya mkoa wa Dar Es Salaam.
Pia Soma
- Wabunge waanza kupiga kura kupitisha bajeti ya Serikali 2019/2020
- Magufuli auita mradi wa NSSF ni bomu, atoa maagizo
- Michango ya wabunge kuhusu Muungano yamkera Makamba, Ndugai toa neno
" Mheshimiwa hakimu, mshtakiwa wa sita katika kesi hii anaomba ruhusa ya kusafiri kwenda Morogoro, ana matatizo ya kifamilia, lakini siku kesi hii itakapotajwa atakuwepo mahakamani hapa" amedia Allen.
Allen baada ya kueleza hayo, upande wa mashtaka umedai hauna pingamizi juu ya ruhusa hiyo kutokana na mshtakiwa huyo kuwa nje kwa dhamana.
Hakimu Ali, baada ya kusikiliza hoja za pande zote amesema maombi ya mshtakiwa wa sita yamekubaliwa na Mahakama.
" Mahakama imekuruhusu wewe mshtakiwa wa sita kusafiri kwenda mkoani Morogoro, lakini kesi hii itakapotajwa unatakiwa uwepo mahakamani hapa" amesema Hakimu Ali .
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Ali ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 8, mwaka 2019 itakapotajwa.
Mbali na Maimu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Meneja Biashara wa (Nida), Aveln Momburi; Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege; Ofisa Usafirishaji, George Ntalima; Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.
Hata hivyo, katika mashtaka hayo, mshtakiwa Momburi na Raymond wao hawana mashtaka ya utakatishaji, hivyo wako nje kwa dhamana baada ya kwenda kuomba dhamana yao Mahakama Kuu.
Kati ya mashtaka hayo 100 yanayowakabili washtakiwa hao; mashtaka 24 ni ya kutakatisha fedha, 23 ya kughushi, 43 ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanya mwajiri, mashtaka matano ni ya kuisababishia hasara Mamlaka hiyo.
Pia, mashtaka mawili ya kula njama ya kulaghai, mashtaka mawili ya matumizi mabaya ya madaraka, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na matumizi mabaya ya madaraka lipo moja ambalo linamkabili Maimu na Sabina.