Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jalada kesi ya Hariri mikononi mwa DPP

Wed, 27 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Jalada la kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin inayomkabili mfanyabiashara Hariri Mohamed Hariri lipo ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka  nchini (DPP) kwa ajili ya kupitiwa ili kukamilisha upelelezi.

Hariri anaendelea kusota rumande takribani mwaka mmoja na siku sita sasa, kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokamilika.

Kwa mara ya kwanza, Hariri alifikishwa Kisutu Machi 20, 2018 kujibu shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya.

Hata hivyo, leo  Machi 26, 2019 wakili wa Serikali, Daisy Makakala, amedai mbele ya Hakimu Mkazi Janet Mtega, kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

“Kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa na jalada halisi la kesi hii liko ofisi ya DPP, kwa ajili ya kukamilisha taratibu za upelelezi, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi umekamilika," amedai Makakala.

Baada ya Makakala kueleza hayo, wakili wa utetezi Saimon Patrick aliomba upande wa mashtaka kueleza upelelezi umefikia hatua gani ili mshitakiwa aweze kutendewa haki yake.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, hakimu Janeth, aliutaka upande wa mashtaka kuhakikisha tarehe ijayo wanaeleza upelelezi umefikia hatua gani.

“Tarehe ijayo nataka muwe mmeshawasiliana na DPP ili kufahamu upelelezi umefika hatua gani kwani mshtakiwa ana haki ya kujua kesi yake imefikia hatua gani," alisema Hakimu Janeth.

Hakimu Janeth aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 8, 2019 na mshtakiwa kurudishwa rumande kutokana na shtaka linalomkabili kutokuwa na dhamana.

Katika kesi ya msingi, Hariri anadaiwa kutenda kosa hilo, Machi 2, 2018 Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Mshtakiwa anadaiwa siku ya tukio alikutwa akisafirisha gramu 214.11 za dawa za kulevya aina ya heroin.

 

 



Chanzo: mwananchi.co.tz