Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jaji mkuu ataka majadiliano mfumo haki jinai

861d4f52a23e2cc08e4cc35650388769.jpeg Prof.Ibrahimu Juma, Jaji Mkuu Tanzania

Fri, 4 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amehimiza majaji kutoka mahakama za Tanzania na Uingereza kujadili jinsi mfumo wa haki jinai uliopo unavyoathiri waathirika na washitakiwa wa makosa ya jinai.

Akizungumza wakati wa kongamano lililowakutanisha majaji wa nchi hizo, alisema hiyo ni fursa mwafaka kwa Mahakama ya Tanzania na ile ya Uingereza kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali, hususani maeneo ya mfumo wa haki jinai ambapo mahakama zote mbili zinashiriki changamoto zinazofanana.

Jaji Mkuu Juma alisema Mahakama ya Tanzania imekuwa ikikumbana na ucheleweshaji mkubwa wakati wa kuendesha hatua za awali za mashauri ya jinai yanayosikilizwa na Mahakama Kuu, hivyo katika Kongamano hilo Mtaalamu kutoka Uingereza, Jaji Nic Madge ataweza kutoa uzoefu wake na namna nchi yake inavyofanya ili kuepuka ucheleweshaji huo.

Wawezeshaji wengine katika Kongamano hilo ni Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman, majaji wengine wabobezi kutoka nchini Uingereza, Jaji Lain Bonomy na Nicholas Blake, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Awamu Mbangwa, Edwin Kakolaki na Dk Zainab Mango pamoja na Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Laurean Tibasana.

Awali, akizungumza katika kongamano hilo, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Dk Gerald Ndika, ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani alisema programu hiyo iliyoandaliwa ni moja ya programu nyingi za maendeleo ya kitaaluma ambazo zimeundwa na chuo kwa kushirikiana na washirika wake.

Dk Ndika alisema kongamano hilo ni ushuhuda wa wazi kwamba chuo hicho kimekuwa kikijitahidi kutimiza majukumu yake chini ya sheria ili kuboresha utoaji wa haki nchini kwa kutoa mafunzo yanayofaa kwa maofisa wa mahakama na watumishi wengine.

Kongamano hilo limeandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Mahakama ya Uingereza na kuratibiwa na Taasisi ya Majaji Wastaafu nchini Uingereza ya Slynn Foundation wakishirikiana na IJA kupitia ufadhili wa Programu ya Kitaifa ya Kuzijengea Uwezo Taasisi za Umma Tanzania zinazohusika na kuzuia na kupambana na rushwa (BSAAT).

Kuandaliwa kwa kongamano hilo ambalo litafanyika kwa siku moja ni sehemu ya jitihada za Mahakama ya Tanzania katika kuwajengea uwezo maofisa wake na wadau wengine wa sheria ya haki nchini katika kutekeleza majukumu yao, hususani utoaji wa haki jinai.

Kongamano hilo pamoja na mambo mengine, limelenga kujadili uboreshaji mbalimbali uliofikiwa na Mahakama ya Tanzania katika utoaji wa haki jinai pamoja na kubadilishana uzoefu wa namna haki jinai kwa wahanga na washitakiwa unavyofanyika kati ya Mahakama ya Tanzania na Mahakama ya Uingereza.

Hii ni mara ya pili kongamano hilo linafanyika baada ya lile la kwanza ambalo lilifanyika katika Wiki ya Sheria, Februari 2020 Dar es Salaam.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live