Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jaji kesi ya bilionea Msuya atishiwa kuuawa

14018 Pic+msuya TanzaniaWeb

Mon, 27 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi/Arusha. Jaji Salma Maghimbi aliyesikiliza kesi ya mauaji ya bilionea Erasto Msuya na kuwahukumu adhabu ya kifo washitakiwa watano, ametishiwa kuuawa na mtu asiyejulikana.

Taarifa zinadai mtu huyo alipiga simu kupitia simu ya mezani (ofisini) na kumtisha Jaji kuwa atamiminia risasi kama za bilionea Msuya kwa kitendo cha kumhukumu ndugu yake kunyongwa.

Msuya aliyekuwa akimiliki vitega uchumi kadhaa jijini Arusha aliuawa kwa kupigwa risasi na bunduki ya kivita aina ya Sub Machine Gun (SMG) Agosti 7, 2013 eneo la Mijohoroni wilayani Hai, Kilimanjaro

Eneo la tukio, kuliokotwa maganda ya risasi za SMG 22 huku gari ya marehemu Msuya aina ya Range Rover namba T800 CKF, bastola zake na simu zake mbili zikikutwa eneo la tukio.

Katika hukumu yake aliyoitoa Julai 23, 2018 mjini Moshi, Jaji Maghimbi aliyekuwa akitokea kituo cha Arusha aliwahukumu adhabu ya kifo washitakiwa watano na kumuachia huru mshitakiwa mmoja.

Soma zaidi:Aliyeachiwa mauaji ya bilionea Msuya aeleza mazito

Waliohukumiwa kunyongwa ni mshitakiwa wa kwanza, Sharifu Mohamed, mshitakiwa wa tatu, Mussa Mangu, mshitakiwa wa tano, Karim Kihundwa, wa sita Sadik Jabir na wa saba, Ally Majeshi.

Washitakiwa hao kupitia kwa mawakili wao, Hudson Ndusyepo, Majura Magafu, Emmanuel Safari na John Lundu wamekwishawasilisha notisi ya kupinga kutiwa hatiani na adhabu waliyopewa.

Katika hukumu hiyo, Jaji alimwachia huru mshitakiwa wa pili, Shaibu Jumanne maarufu kwa jina la “Mredii”, baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha shitaka dhidi yake.

Vyanzo mbalimbali vya ndani ya mahakama vimedai mtu aliyempigia simu Jaji Maghimbi alidai kama watashindwa kumuua nyumbani au barabarani, basi wangetekeleza mauaji hayo akiwa katika eneo la mahakama Kuu.

Taarifa hizo zinadai kutokana na vitisho hivyo, Jeshi la Polisi limemuongezea ulinzi jaji huyo ambaye sasa amehamishiwa divisheni ya Ardhi jijini Dar es Salaam lakini anamalizia kesi zake jijini Arusha.

Taarifa ya kuhamishwa kwa jaji huyo kupelekwa katika Mahakama Kuu divisheni ya Ardhi jijini Dar es Salaam ilitolewa juzi na mtendaji mkuu wa mahakama Mkoa wa Arusha, Edward Mbara katika hafla ya kuwaaga majaji watatu na mahakimu watano waliohamishwa mikoa mingine kutoka Arusha.

Jaji Maghimbi alipoulizwa juu ya kupokea simu ya vitisho alisema hawezi kulizungumzia suala hilo kwani si msemaji wa Mahakama na kuelekeza aulizwe Naibu Msajili wa Mahakama Kuu.

“Naomba uzungumze na Msajili atakueleza juu ya hili jambo,” alisema Jaji Maghimbi.

Naibu Msajili Mahakama Kuu Arusha, Seif Kulita alikiri kupata taarifa ya jaji huyo kutishiwa, lakini akasema suala la mahakimu na majaji wanaotoa hukumu dhidi ya wahalifu ni jambo la kawaida.

“Taarifa hizo nilizisikia, lakini haya mambo ya vitisho ni kawaida mahakamani na tumekuwa tukiwataka wanaopinga hukumu kufuata taratibu za kisheria,” alisema Kulita.

Naibu Msajili Kulita alitoa wito kwa watu ambao hawaridhiki na hukumu au uamuzi wowote au wanaona maamuzi ya Mahakama si mazuri wayapinge kwa kufuata utaratibu wa kisheria.

Hata hivyo Naibu Msajili huyo alisema jambo hilo halikuripotiwa rasmi mahakamani kama ambavyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Ramadhan Ng’anzi alivyosema kuwa halikuripotiwa kwao.

Akitoa hukumu ya adhabu ya kifo Julai 23, 2018, Jaji Maghimbi alisema mahakama imezingatia maelezo ya kukiri kosa na ungamo ya washitakiwa wanne na ushahidi huru kuunga mkono.

Maelezo ya kukiri kosa ambayo yalipokelewa mahakamani na kusomwa, yakieleza mpango mzima wa mauaji hayo na ushiriki wa kila mmoja ni ya Sharifu, Mangu, Karim, Sadick na Ally Majeshi.

Kwa mujibu wa Jaji Maghimbi, maelezo ya Sharifu ambayo yaliungwa mkono na mashahidi wengine wa Jamhuri, yanaeleza mpango mzima wa mauaji ulivyosukwa na bunduki ilivyonunuliwa.

Pia katika maelezo hayo, mshitakiwa huyo alieleza namna laini mpya za simu zilivyosajiliwa kwa majina ya Kimasai na namna pikipiki mbili zilizotumika katika mauaji hayo zilivyonunuliwa.

Soma zaidi: KESI MAUAJI YA BILIONEA MSUYA: Hukumu ya dakika 60 yawatia hatiani watano

Kuhusu mshitakiwa Mangu, Jaji huyo alisema ingawa katika maelezo yake ya kukiri kosa alianza kwa kujitoa na kuwabebesha mzigo washitakiwa wenzake, lakini alishiriki katika nia hiyo ovu.

“Ingawa alianza maelezo hayo ya kukiri kosa kwa kujitoa lakini alijua mpango huo wa mauaji na akaendelea kushiriki katika mipango hiyo ya mauaji hadi mwisho bila kujitoa,”alisema Jaji.

“Kitendo cha kutojitoa katika mpango mzima wa mauaji yanaonyesha nia yake ovu ya kutenda kosa hilo. Hakufanya juhudi zozote za kujitoa katika mipango hiyo miovu ya mauaji,”alisisitiza Jaji.

Jaji Maghimbi alisema maelezo ya mshitakiwa Karim anayeeleza kuwa ndiye aliyemfyatulia risasi nyingi marehemu, hadithi yake inaunganika na yale waliyoeleza Sharifu, Mussa na Mjeshi. Pia Jaji alisema maelezo hayo ya kukiri kosa na maungamo ya washitakiwa, yaliungwa mkono na mashahidi wengine wa Jamhuri na hivyo kuthibitisha shitaka la mauaji pasipo kuacha shaka yoyote.

Soma zaidi:KESI MAUAJI YA BILIONEA MSUYA: Hivi ndivyo mipango ya mauaji ilivyosukwa

Soma zaidi: Niliyojifunza siku 1,285 kesi mauaji ya Bilionea Erasto Msuya

Chanzo: mwananchi.co.tz