Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jaji akataa ombi la kina Sabaya

Sabaya Kesi Pic Jaji akataa ombi la kina Sabaya

Mon, 14 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Leo Februari 14, 2022, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, ilipanga kuanza kusikiliza mfululizo rufaa hiyo namba 129 iliyokatwa na Sabaya na wenzake wawili ambao ni Sylvester Nyegu na Daniel Mbura.

Wajibu rufaa (Jamhuri) iliwakilishwa na Mawakili wa Serikali Waandamizi Ofmedy Mtenga, Verdiana Mlenza na Wakili wa Serikali, Baraka Mgaya.

Waomba rufaa hao waliwakilishwa na jopo la mawakili sita wakiongozwa na Wakili Majura Magafu, Mosses Mahuna, Fauzia Mustafa, Edmund Ngemela, Sylvester Kahunduka na Fridolin Bwemelo.

Jaji Kisanya kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, amekataa ombi lililowasilishwa na Wakili Magafu aliyeomba mahakama hiyo kuahirisha rufaa hiyo hadi Februari 21, 2022.

Hata hivyo, Jaji Kisanya amesema Mahakama hiyo imepitia ombi la ahirisho ambapo kumbukumbu la shauri hilo linaonyesha lilipopangwa kwa ajili ya kutajwa Desemba 15, 2021 pande zote zilielezwa shauri limepangwa kuanza kusikilizwa leo.

Advertisement "Pande zote zilielezwa na kwa sababu hiyo waleta rufaa walipaswa kuomba na kuchukua nakala za vielelezo kabla ya usikilizwaji wa shauri hilo ili tunapokuja leo tuweze kusikilizwa," amesema Jaji Kisanya.

Kuhusu hoja ya Wakili Mahuna kuwa na kesi nyingine Mahakama ya Rufaa na hati ya wito Mahakama waliyopokea inaonyesha wakili huyo aliipata Januari 19, 2022 hivyo alipaswa kujulisha mahakma ili inapopanga usikilizwaji wake iweze kujua inakuwaje.

"Mahakama imeangalia mleta rufaa namba moja ukiachana na Wakili Mahuna ana Mawakili Magafu na Fauzia, hawa wote wanaweza kumwakilisha lakini pia nami nina majukumu mengine kusikiliza mashauri," alisema Jaji.

"Tarehe zinazoombwa na mimi nina session ya criminal nitaendesha Dar es Salaam, ombi la kuahirisha itakuwa ni vigumu na ili haki itendeke tuahirishe siku ya leo ili mawakili waweze kujipanga namna watawasilisha hoja zao na tukutane kesho saa tatu na waleta rufaa wapatiwe nakala za vielelezo," amesema.

Awali Wakili Mtenga ameieleza mahakama hiyo kuwa shauri hilo lilipangwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa na upande wao wako tayari kuendelea na usikilizwaji.

Hata hivyo, baadaye Wakili Magafu aliiomba mahakama ihairishe kusikiliza rufaa hiyo hadi Februari 21.

Wakili Magafu amesema ameunganishwa kwenye rufaa hiyo na hakuwepo wakati kesi inasikilizwa mahakama ya Hakimu Mkazi hiyo anaomba wapewe nakala za vielelezo ambavyo vilipokelewa wakati wa usikilizwaji mahakama ya chini.

"Nimeunganishwa kwenye hii kesi na sikuwepo wakati inasikilizwa kwenye trial mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi. Nimepewa instructions (maelekezo) kuungana na wenzangu na kupewa rekodi na judgement (hukumu)," amesema Wakili Magafu.

Wakili Magafu anayemwakilisha mleta rufaa wa kwanza (Sabaya), ametaja sababu ya pili kuwa Wakili Mahuna ambaye pia anamwakilisha Sabaya, anatakiwa kwenda Mahakama ya Rufaa Februari 15 na 16, hivyo wanaomba kesi iahirishwe ikizingatiwa Mahuna alikuwepo wakati kesi hiyo inasikilizwa Mahakama ya Hakimu Mkazi.

Wakili Mtenga aliieleza Mahakama kuwa wao walikuwa tayari kuendelea na rufaa hiyo hivyo wanaiachia mahakama iamue vile itakavyoona ni haki kwa pande zote mbili kutoa uwakilishi wao.

Oktoba 15 Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo, aliwahukumu Sabaya na wenzake wawili kifungo cha miaka 30 kila mmoja, baada ya kuthibitika na hatia katika makosa matatu ikiwamo unyang'anyi wa kutumia silaha.

Rufaa hiyo inatokana na shauri la awali la unyang'anyi wa kutumia silaha lililokuwa namba 105, 2021, lililokuwa likiwakabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live