Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jaji aamua kesi ya waliopelekwa jela miaka 10 isikilizwe upya

HUKUMU Jaji aamua kesi ya waliopelekwa jela miaka 10 isikilizwe upya

Wed, 17 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu imeamuru kusikilizwa upya kwa kesi inayowakabili wakazi wawili wa Ifaraka waliohukumiwa kifungo cha miaka 10 jela kwa kukutwa na vifaa vya kuvunjia nyumba na cha kuiba simu kupitia dirishani.

Hati ya mashtaka inadai tukio hilo lilitokea Julai 19, 2022 eneo la Mhola katika mji wa Ifaraka, ambapo walikamata na begi dogo likiwa na kichoteo cha simu na vifaa vingine vya kuvunjia nyumba, ambavyo ni bisibisi, spana, mapanga na simu za wizi.

Washtakiwa hao, Said Kanji na Nikolaus Uliza, mwaka jana walihukumiwa kifungo cha miaka 10 jela na Mahakama ya Wilaya ya Kilombero baada ya kuwatia hatiani.

Hata hivyo, Kanji pekee aliamua kukata rufaa kupinga hukumu hiyo.

Baada ya kusikiliza hukumu hiyo, Jaji Hadija Kinyaka wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, ameamuru kusikilizwa upya kwa kesi hiyo baada ya kubaini dosari za kisheria, kwamba walishtakiwa kwa kifungu kinachohusu kosa lililotendwa mchana wakati tuhuma dhidi yao zinadaiwa kutendwa usiku.

Kulingana na Jaji Kinyaka, wakati anaandaa hukumu hiyo, alibaini katika hati ya mashtaka na hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Kilombero, kuwa watuhumiwa walishtakiwa chini ya kifungu 298(d) cha kanuni ya adhabu.

Kifungu hicho kinasema mtu yeyote anayekutwa katika mojawapo ya mazingira matano au sita ikiwamo kumiliki wakati wa mchana chombo chochote cha kuvunja nyumba kwa kusudi la kutenda kosa, atakuwa ametenda kosa la jinai.

Hata hivyo, Jaji alisema ushahidi uliowatia hatiani unaonyesha walikamatwa na vifaa hivyo kati ya saa 5:00 usiku na 6:00 usiku na sio mchana. Hivyo kama ni kushtakiwa walistahili washtakiwe kwa kifungu 298(c) na sio kifungu cha 298(d).

Kifungu cha 298(c) kinasema iwapo mshtakiwa atakutwa anamiliki wakati wa mchana, chombo chochote cha kuvunja nyumba kwa kusudi la kutenda kosa, atakuwa ametenda kosa la jinai.

Akirejea hati ya mashtaka, Jaji alisema hati hiyo sio tu ilinukuu kifungu kisicho sahihi cha 298(d) cha kanuni ya adhabu, bali pia katika maelezo ya kosa waliloshitakiwa nalo, pia haikuonyesha muda ambao kosa lilitendeka.

“Maudhui ya kifungu 298(c) na (d) ya kanuni ya adhabu yanatofautiana. Tofauti ya kwanza ni muda wa kutenda kosa,”alisema Jaji na kueleza kifungu cha (c) kinataka kama kosa limetendeka usiku wakati kifungu (d) ni kama limetendeka mchana.

“Nimepitia kwa umakini mwenendo wa kesi wa mahakama iliyosikiliza shauri hili na kubaini ushahidi wa mashtaka na wa utetezi uko wazi, kuwa washtakiwa walikutwa na vifaa hivyo usiku na kosa linaangukia kifungu cha 298(c),” alisema.

"Pia, mwenendo wa kesi wala hukumu ya mahakama iliyoonyesha kama washtakiwa walijulishwa matakwa yaliyopo katika kifungu 298 (c), kwamba kosa waliloshtakiwa nalo liliwataka watoe utetezi wao juu ya uhalali wa hivyo vitu,” alieleza.

"Mwenendo wa kesi hauonyeshi popote kwamba hati ya mashtaka ilifanyiwa marekebisho ili kutimizwa takwa la kifungu 234(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA),” alisema Jaji Kinyaka katika hukumu yake.

"Nimebaini mwenendo uliosababisha hukumu, hauonyeshi kama washtakiwa walijulishwa shitaka linalowakabili ambalo liliwataka kuthibitisha au kukanusha kuwa vifaa hivyo walikuwa navyo kihalali au la,” alisema.

"Usikilizwaji wa awali (PH) na uamuzi mdogo wa kama wana kesi ya kujibu na hukumu unaonyesha upande wa mashtaka na utetezi waliongozwa kujitetea kama washtakiwa walikamatwa na vifaa hivyo usiku,” alisema.

Jaji alisema ili kutenda haki na haki ionekane imetendeka, anamuru jalada la kesi lirejeshwe mahakama ya Wilaya ya Kilombero na kesi hiyo isikilizwe upya na haraka mbele ya hakimu mwingine na washtakiwa wataendelea kushikiliwa mahabusu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live