Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jaji Mkuu aweka wazi kinachochelewesha kesi za mirathi

Law Photo Jaji Mkuu ataja kinachochelewesha kesi za mirathi

Thu, 10 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amesema ucheleweshwaji wa kesi nyingi za mirathi hapa nchini unaanzia kwenye mvutano wa mali wakati wa vikao vya familia huku mahakama ikitupiwa lawama.

Pia, amewataka Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutoka Kanda zote nchini, kila mmoja kujiwekea utaratibu wa kujipima kiasi gani katika Kanda au Divisheni yake wanatekeleza nguzo tatu zinazobeba dira ya maboresho ya mahakama na kuweka mikakati ya kuboresha huduma ya utoaji haki.

Profesa Juma amesema hayo leo Ferbuari 10, 2022, akizungumza katika kikao kazi cha siku mbili kilichokutanisha Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutoka Kanda zote nchini.

Amesema kuwa kupitia kikao kazi hicho Majaji hao watajadiliana kujua hali ya mrundikano wa mashauri kwa kubadilishana uzoefu na kuchambua mashauri yanayohitaji kipaumbele na yale yanayolalamikiwa katika jamii.

"Tunatoka katika Kanda na Divisheni mbalimbali tuna changamoto, sasa huu ni wakati ambapo sisi ni muhimu tuelewe hizo changamoto na tuweze kubadilishana uzoefu, changamoto kubwa ambayo tunalalamikiwa sana ni ucheleweshaji," amesema

Amesema tatizo hilo siyo Tanzania peke yake na hadhani kama kuna mfumo wowote wa utoaji haki ambao haulalamikiwi na ucheleweshaji hivyo kupitia kikao hicho ni vizuri wapambanue kwa undani ni vitu gani vinasababisha ucheleweshaji wa kesi.

Amesema katika kesi za mirathi, wanaohusika na mirathi wakiwa na makubaliano kutoka kwenye vikao vya familia wanachofuata mahakama ni amri tu lakini wanapoenda wakiwa na chuki, ugomvi na tamaa wanasababisha ucheleweshwaji wa mashauri hayo huku mahakama ikitupiwa lawama.

"Nikitolea mfano kwenye kesi za mirathi mara nyingi lawama za ucheleweshaji zinapelekwa kwa Mahakama. Lakini ukiangalia ukweli wa mashauri ya mirathi ucheleweshaji unaanzia kwenye vikao vya familia," amesema Profesa Juma.

"Ucheleweshaji wa kesi za mirathi zinaanzia kwenye mvutano wa mali wakati wa vikao vya familia, mara nyingi hamna kesi ambazo ni nyepesi kama kesi za mirathi. Wanaohusika na mirathi wakiwa na makubaliano kutoka kwenye vikao vya familia wanachotafuta mahakamani ni amri tu ya mwisho ya mahakama.

"Lakini wakija na zile tofauti zao, ugomvi, chuki, tamaa zao huo ucheleweshaji unakuwa ni lawama kwa Mahakama kwa hiyo huu ni wakati wa sisi kutafakari asili ya viini vya changamoto za mirathi kwa sababu mirathi zina taratibu zake,kuna taratibu za kidini,kifamilia,"amesema Profesa.

Profesa Juma amewataka Majaji hao kutambua kuwa wao ndiyo wasimamizi wakuu katika Kanda au divisheni hivyo sheria zinazotegemewa na ngazi mbalimbali za Mahakama katika kufanikisha utoaji haki, hivyo kunapotokea mabadiliko ya Sheria au kanuni ni wajibu wao kuyafahamu na kuwaelimisha watumishi wote kuhusu mabadiliko.

"Mfawidhi atafanikiwa endapo yeye mwenyewe atajitambua na kutambua uwezo wako na mapungufu yako kama kiongozi,vigezo binafsi na Kikanda/Divisheni kujipima, kujitathmini katika uongozi wenu, ni lazima kila mmoja wenu, ajiwekee utaratibu wa kujipima kwa kiasi gani,unatekeleza kwa vitendo nguzo tatu zinazobeba dira ya maboresho ya Mahakama,"amesema Jaji Mkuu.

Awali, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mustapher Siyani amesema kikao hicho kimeshirikisha Majaji Wafawidhi kutoka katika Kanda zote za Mahakama Kuu, Divisheni na Vituo na kuwa kikao hicho hufanyika kila mwaka.

Jaji Siyani amesema kutokana na dunia kukumbwa na janga la Uviko-19, mara ya mwisho kikao hicho kilifanyika mwaka 2019.

Amesema kasi ya usikilizwaji wa mashauri imeendelea kuonegzeka mwaka hadi mwaka kuanzia Mahakama Kuu hadi chini,idadi ya mashauri ya muda mrefu imepungua kwa wastani wa asilimia nne kutoka asilimia 15 mwaka  2020 hadi hadi asilimia 10.9 mwaka 2021.

"Wastani wa muda ambao mashauri yanachukua mahakamani kutoka kusajiliwa hadi kuamuliwa pia imeendelea kupungua. Niwapongeze majaji wafawidhi kwa juhudi kubwa na uongozi ikiwemo mambo yaliyowezesha jukumu la msingi la mahakama ambalo ni utoaji haki kutoathirika licha ya nchi yetu kukabiliwa na janga la Uviko-19,"amesema

Chanzo: www.tanzaniaweb.live