Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jacketi lilivyowakamatisha washitakiwa mauaji ya Msuya

Bilionea Msuya Ilivyokuwa.jpeg Jacketi lilivyowakamatisha washitakiwa mauaji ya Msuya

Mon, 18 Dec 2023 Chanzo: Mwananchi

Katika tolea la mwisho tuliwaletea ushahidi wa shahidi wa 21 wa upande wa mashtaka, Flotea Fidelis Mmasi, aliyeieleza mahakama kuwa ndiye aliyeuza pikipiki mbili aina ya Toyo namba T316 CLB na King Lion namba T751 CKB.

Pikipiki hizo ndizo ambazo mashahidi wa upande wa mashtaka walieleza zilitumiwa na wauaji wa mfanyabiashara Erasto Msuya kwenda eneo la tukio katika Kijiji cha Orkalili Agosti 7,2013, kufanya mauaji na kutoroka nazo.

Leo tunawaletea ushahidi wa mashahidi watano, ambapo shahidi wa 22, Scholastika Kilaghane (31) alieleza kuwa Januari 16, 2014 alipokea barua kutoka ofisi ya RCO Kilimanjaro, ikihitaji taarifa za simu namba 0682405323.

“Baada ya kupokea barua hiyo niliandika barua pepe kwenda idara ya IT (teknolojia ya mawasiliano) ili wanipe jina la mmiliki wa namba hiyo na taarifa nyingine. Watu wa IT walinipa taarifa zote nilizozihitaji,” alieleza Kilaghane.

Shahidi huyo aliomba aitoe taarifa hiyo kama kielelezo cha ushahidi wake, lakini mawakili wa utetezi walipinga wakisema hakuwa shahidi sahihi wa kukitoa na pia kuaminika kwa nyaraka yenyewe, ingawa jaji alikataa pingamizi hilo.

Akiongozwa na wakili wa Serikali, Kassim Nassir, shahidi huyo alisema laini hiyo ilisajiliwa Agosti 5, 2013 saa 7:19 mchana kwa jina la Moti Mongulu na wakati huo ilionyesha ilikuwa imezuiwa, hivyo kuonyesha ilikuwa na usajili wa muda.

Namba hiyo ndio iliyotumiwa na wauaji wa bilionea Msuya kumvuta hadi eneo la tukio, kwa kumghilibu wanataka kumuuzia madini aina ya Tanzanite.

Mkulima alishiriki kusaka SMG

Shahidi wa 23, Joseph Mushi (64) ambaye ni mkulima na mkazi wa kitongoji cha Tamaya, Kijiji cha Nkwansira wilayani Hai, alieleza namna Septemba 14,2013 akiwa shambani alivyoombwa na polisi kushiriki kutafuta bunduki aina ya SMG.

Bunduki hiyo ndio iliyoelezwa kutumika kumuua Msuya na ilifichwa hapo na mshtakiwa wa sita, Sadik Jabir maarufu kama Msudani au Mnubi ambaye alikamatwa Kaliua mkoani Tabora akiwa kwa mganga wa kienyeji.

Kwa upande wake, shahidi wa 24, Mrakibu wa Polisi (SP), Godfrey Luhamba, ambaye ni mtaalamu wa uchunguzi wa kisayansi na milipuka makao makuu wa Polisi, ndiye aliyechunguza maganda ya risasi 22 na bunduki ile ya SMG.

Akiongozwa na wakili Abdalah Chavula kutoa ushahidi, alisema Septemba 23,2013 akiwa ofisini kwake, alipokea vielelezo ambavyo ni SMG namba 1952 r KJ 10520 na maganda ya risasi, ili kuchunguza kama maganda yalipigwa na bunduki hiyo.

“Niliijaribu hiyo bunduki kwa kufyatua risasi tatu na kuthibitisha inafanya kazi vizuri. Kwa kawaida ukifyatua risasi lile ganda linabaki pale ulipofyatulia. Nilichukua yale maganda na kurudi nayo maabara,” alieleza shahidi huyo.

“Kwenye maabara yetu sasa hivi tuna microscope ya kidigitali ambayo ndio tunaitumia kulinganisha. Baada ya kufanya huo ulinganisho nilithibitisha kuwa maganda yale yaliyookotwa eneo la tukio yalipigwa na ile SMG,” alisema.

Shahidi huyo aliomba Mahakama ipokee ripoti aliyoiandaa na kuituma ofisi ya RCO Kilimanjaro ambayo ndio iliomba uchunguzi huo na upande wa utetezi haukuwa na kipingamizi. Mahakama ikaipokea kama kielelezo namba 16.

Ushahidi wa DNA ulivyokuwa

Baada ya shahidi huyo wa 24 kumaliza kujibu maswali ya dodoso kutoka kwa mawakili wa Serikali, upande wa mashtaka ulimwita shahidi wa 25, Gloria Omary ambaye mwaka 2013 alikuwa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Shahidi hiyo alikuwa katika idara ya uchunguzi wa kisayansi (Forensic Science) na uchunguzi wa vinasaba (DNA) na kwamba Oktoba 2,2013 alipokea kifurushi chenye sampuli kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Kanda ya Arusha ili azifanyie uchunguzi.

“Nililetewa sampuli na jaketi ili nithibitishe sampuli za nguo nilizoletewa zinatoka kwenye jaketi. Uchunguzi wangu ulithibitisha zilitoka kwenye lile jaketi. Niliandaa ripoti na naomba ipokelewe kama kielelezo,”alisema.

Mahakama ilipokea ripoti hiyo kama kielelezo, lakini pia akaomba atoe jaketi alilokuwa ameletewa kwa ajili ya utambuzi. Upande wa utetezi ulipinga vikali, lakini katika uamuzi wake mdogo, Jaji Salma Maghimbi alikubali ombi hilo.

Jaketi hilo liliokotwa eneo la Orkolili Julai 7, 2013 baada ya kuachwa na watu wawili wanaodaiwa kuwa na silaha, baada ya pikipiki waliyokuwa wakiitumia kupata pancha na kuamua kuitelekeza pamoja na koti hilo eneo la tukio.

Shahidi wa 26, Kaijunga Trifodi, alisema Septemba 19, 2013 alikuwa akifanya kazi katika Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Kanda ya Arusha na alikuwa Ofisa Mfawidhi wa Huduma za Maabara na moja ya majukumu ni kupokea vielelezo.

Alisema siku hiyo walifika maofisa wa polisi wakiongozwa na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Damian Chilumba ambapo Chilumba alimjulisha wameleta kielelezo ambacho ni jaketi pamoja na watuhumiwa wawili ili awachukue sampuli.

Shahidi huyo alieleza alichukua sampuli kutoka katika lile jaketi na kuvipa alama na kuvifunga kwenye bahasha na kisha akachukua sampuli za damu na mate kwa watuhumiwa na alianza na Karim Kihundwa na kisha Sadick Jabir.

Baadaye alizifunga sampuli zote na kuzipeleka Dar es Salaam ambapo alimkabidhi Gloria Machuve na kuiomba Mahakama ipokee risiti aliyowaandikia polisi kuthibitisha kupokea vielelezo hivyo, ombi ambalo halikupingwa na utetezi.

Baada ya kuonyeshwa alilitambua kuwa ndio lenyewe na kuomba kulitoa kama kielelezo, lakini mawakili wa utetezi John Lundu na Majura Magafu walipinga, pingamizi ambalo baadaye lilikubaliwa na Jaji Maghimbi.

Mwakili walivyopinga Jaketi

Katika hoja zake za kupinga jaketi hilo lisipokelewe kama kielelezo, wakili Majura alisema shahidi huyo si sahihi kulitoa kwa vile mnyororo wa makabidhiano (chain of custody) ulikatika.

Wakili Magafu katika hoja zake alieleza shahidi ameeleza tu kuwa koti hilo aliletewa na mkaguzi msaidizi wa polisi, Damian Chilumba, lakini haijaelezwa lilimfikiaje Chilumba kutoka eneo la tukio.

Akitoa uamuzi huo mdogo kuhusiana na pingamizi hilo, Jaji Maghimbi alisema kwa mujibu wa shahidi wa tatu, Raphael Karoli, ndiye aliyeliokota jaketi hilo na kumkabidhi shahidi wa tisa, Inspekta Samwel Maimu.

“Kwa mujibu wa ushahidi wa shahidi huyu wa 26 (Brassy) yeye alilipokea jaketi hilo kutoka kwa Chilumba. Mahakama za juu zimesisitiza umuhimu wa chain of custody kuzingatiwa katika mapokezano ya vielelezo,” alisema Jaji Maghimbi.

Jaji alisema katika kesi iliyopo mbele yake, Chilumba ndiye aliyekuwa na dhamana ya kidhibiti hicho na kukipeleka kwa shahidi wa 26 na kwamba kazi ya shahidi wa 26 ilikuwa ni kuchukua sampuli tu.

“Kazi ya shahidi wa 26 ilikuwa ni kuchukua tu sampuli kutoka kwenye hicho kidhibiti na wala hakuwa na wajibu wa ku tress (kufuatilia) kilitokea nini baada ya kumkabidhi shahidi wa 26 (Gloria Omary)”.

“Je anawezaje kutuambia ni kile kile (kidhibiti) kilichopatikana eneo la tukio? Hawezi (shahidi wa 26) kuwa katika nafasi ya kujibu maswali kuthibitisha kama jaketi hilo ndilo lililookotwa na Karoli.

“Kwa hatua ya sasa nakubaliana na hoja za pingamizi zilizoibuliwa na mawakili wa utetezi. Kwa hiyo kwa hatua ya sasa nakataa kielelezo hicho (jaketi) kupokelewa kama kielelezo cha kesi hii,” alihitimisha Jaji Maghimbi.

Baada ya uamuzi huo, shahidi huyo wa 26 aliendelea kutoa ushahidi wake kwa kuongozwa na wakili wa Serikali, Kassim Nassir. Akidodoswa na wakili wa utetezi Ndusyepo, shahidi alidai siku hiyo ya Septemba 19, 2013 alipokuwa ofisi ya Arusha na kuchukua sampuli hizo, ilikuwa ndio siku ya kwanza kuwaona washtakiwa hao.

“Sikuwahi kuwauliza kama walikuwa wametokea magereza ama polisi kwa kuwa hiyo si kazi yangu. Kazi yangu ilikuwa ni kuchukua tu sampuli kwa ajili ya upimaji wa DNA,”alisisitiza shahidi huyo.

Akihojiwa na wakili Magafu iwapo kuna uwezekano akaja mtu mwingine kabisa mbele yake na kujiita Sadick na mwingine Karim na yeye akaandika majina yao hivyo, shahidi huyo alisema yeye hajui.

Alipoulizwa kama kuna wakati wowote aliwahi kuomba uthibitisho kuthibitisha washtakiwa hao ndio walioko mbele yake, alidai hakufanya hivyo na wala hakuwahi kuomba vitambulisho vyao.

Wakili Magafu alimuuliza endapo itabainika alipigwa changa la macho na kuletewa watu wengine kabisa na si washtakiwa hao atasemaje kwa kuwa walikuwa magereza, akajibu yeye si mpelelezi. Usikose kufuatilia mfululizo wa simulizi hii kesho.

Chanzo: Mwananchi