Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Idadi ndogo ya ndugu wajitokeza kusikiliza hukumu ya mjane wa Bilionea Msuya

Msuya Bilionea.jpeg Idadi ndogo ya ndugu wajitokeza kusikiliza hukumu ya mjane wa Bilionea Msuya

Fri, 23 Feb 2024 Chanzo: mwanachidigital

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeanza kusoma hukumu ya kesi ya mauaji inayomkabili mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa madini jijini Arusha, Erasto Msuya maarufu kama Bilionea Msuya, Miriam Mrita na mwenzake Revocatus Muyella maarufu kwa jina la Ray.

Hukumu hiyo inasomwa leo Ijumaa Februari 23, 2024 na Jaji Edwin Kakolaki aliyeisikiliza.

Washtakiwa hao, Miriam na Muyella wanakabiliwa na shtaka moja la mauaji ya kukusudia la kumuua Aneth Elisaria Msuya (wifi wa Miriam) aliyekuwa mdogo wa Bilionea Msuya.

Aneth aliuawa kwa kuchinjwa na kitu chenye ncha kali nyumbani kwake Kibada Kigamboni, Dar es Salaam Mei 25, 2016.

Katika hukumu hiyo Jaji Kakolaki ameanza kwa kurejea shtaka linalowakabili kisha ushahidi wa upande wa mashtaka akifanya muhtasari wa ushahidi wa kila shahidi.

Kisha atarejea utetezi wa washtakiwa kabla ya kuchanganua namna gani upande wa mashtaka umeweza au umeshindwa kuthibitisha shtaka bila kuacha shaka kwa washtakiwa wote.

Mtaalamu wa uchunguzi wa sayansi jinai

Jaji Kakolaki: Shahidi huyu alieleza jinsi alivyokwenda kufanya uchunguzi eneo la tukio ( chumbani kwa marehemu Aneth alikouawa), kwa maelekezo ya RCO, Richard Mchomvu.

Alieleza kuwa ndiye aliyekusanya vielelezo hivyo, yaani kisu, nguo ya ndani na filimbi.

Alisema alichukua kisu kwa kuwa aliona mwili wa marehemu una jeraha na nguo ya ndani ili kujiridhisha kama marehemu (Aneth) alikuwa ameingiliwa kabla ya kuuawa na filimbi alitaka kujua kama kabla ya kuuawa alijaribu kuomba msaada.

Shahidi huyu alieleza kuwa, ndiye alimkabidhi WP Mwaka (Shahidi wa 23) vielelezo hivyo hadi baadaye alipotumwa kwenda kuvichukua na kumkabidhi WP Elitruda ambaye alivipeleka kwa Mkemia (shahidi wa 15).

Hata hivyo, alipoulizwa na mawakili wa utetezi iwapo alichukua alama za vidole katika baadhi ya vitu kwenye eneo la tukio alisema hakuchukua.

Ushahidi wa vinasaba

Jaji Edwin Kakolaki amerejea ushahidi wa shahidi 15 wa upande wa mashtaka, Dk Fidelis Segumba aliyefanya uchunguzi wa kisayansi katika vielelezo vilivyochukuliwa eneo la tukio yaani, nguo ya ndani ya marehemu, filimbi, kisu na mpanguso wa mate kutoka kwa mshtakiwa wa pili, Revocatus Muyella.

Jaji Kakolaki amesema katika matokeo ya uchunguzi huo, Dk Segumba aliieleza Mahakama kuwa vinasaba katika mpini wa kisu vilioana na vinasaba katika mpanguso wa mate ya mshtakiwa wa pili, Muyella.

Idadi ndogo ya ndugu wajitokeza kusikiliza hukumu ya mjane wa Bilioane Msuya

Wakati Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ikiendelea kusoma hukumu ya kesi ya mauaji inayomkabili mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa madini jijini Arusha, Erasto Msuya maarufu kama Bilionea Msuya; Miriam Mrita na mwenzake

Idadi ndogo ya ndugu wa pande zote wamejitokeza kusikikiza hukumu hiyo, tofauti na kesi nyingine, huwa wengi hadi kukosa nafasi ya kukaa.

Leo Ijumaa Februari 23, 2024 ndugu, jamaa na marafiki wa washtakiwa na wale wa upande wa walalamikaji wameweza kuingia wote katika ukumbi namba moja wa Mahakama hiyo na kukaa bila changamoto yoyote ikilinganishwa na kesi kama ya kina Halima Mdee, idadi ya watu ilikuwa kubwa na kushauriwa wengine wakae nje ya chumba cha Mahakama wasubirie uamuzi.

Washtakiwa hao, Miriam na Muyella wanakabiliwa na shtaka moja la mauaji ya kukusudia la mauaji ya Aneth Msuya (wifi wa Miriam) aliyekuwa mdogo wa Bilionea Msuya.

Jaji Kakolaki akitoa muhtasari

Jaji Edwin Kakolaki anaendelea na muhtasari wa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka, kile walichokisema kila mmoja kwa ufupi.

Awali, alirejea ushahidi wa shahidi wa kwanza, WP Mwajima aliyeeleza kuwa ndiye aliyeandika maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa kwanza, Miriam Mrita akidai kuwa alikiri katika maelezo hayo kuhusika na kosa la mauaji ya wifi yake, Aneth Msuya.

Katika muhtasari wa shahidi wa pili, Mlinzi wa Amani, Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Ilala, Reunia Kajumlo amesema shahidi huyo pia aliieleza Mahakama kuwa aliandika maelezo ya mshtakiwa huyo ambako pia alikiri kosa.

Shahidi wa nne, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kigamboni, Richard Mwaisemba ameieleza namna alivyopata taarifa ya tukio la mauaji hayo kutoka kwa askari wa kituo kidogo cha Kibada.

Amedai kuwa, alifika eneo la tukio na kukuta alikuta mwili wa Aneth ukiwa umelala chini kwenye dimbwi la damu kisha akamtaarifu aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Temeke, (SSP) Richard Mchomvu ambaye pia alifika eneo hilo.

Mashahidi hao wawili wamedai kuwa, eneo la tukio pembeni ya mwili walikusanya vielelezo ambavyo ni nguo ya ndani ya marehemu, filimbi na kisu kilichokuwa na damu.

Chanzo: mwanachidigital