Wiki iliyopita nilimsikia mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro akitangaza operesheni ya mwezi mmoja kudhibiti ajali, lakini ni vyema operesheni hii isilenge tu madereva wa malori na mabasi, bali iende hadi kwa waendesha pikipiki.
Nasema hivyo kwa sababu, pengine tumeshtushwa tu na ajali za barabarani zilizotokea mfululizo takribani wiki tatu na kuharibu maisha ya watu zaidi ya 50, lakini ukweli ni kwamba hata bodaboda na bajaji ni janga la taifa hili.
Nimemsikiliza kwa umakini sana IGP Sirro, lakini ukichambua kauli yake na maagizo yake ni kama yamewalenga tu madereva wa magari madogo, mabasi na malori lakini bodaboda na bajaji ni kama wao wana sheria zao za barabarani.
Nasema hivyo kwa sababu Agosti, 2021 ni IGP huyu huyu alitangaza operesheni ya mwezi mmoja dhidi ya waendesha pikipiki au bodaboda ili waheshimu sheria za barabarani, operesheni ambayo pengine ilifanyika mikoa michache sana.
Akitangaza operesheni hiyo, IGP Sirro alisema sasa hivi waendesha pikipiki huko mitaani wanaendesha vyombo hivyo vya moto bila kuvaa kofia ngumu (helmet) na kwamba hiyo ni kulidhalilisha jeshi hilo lionekane halisimamii sheria.
Lakini leo anapotangaza operesheni nyingine ya mwezi mmoja, anafahamu namna bodaboda wengi na abiria wao wanavyofariki kwa ajali huko barabarani? Hivi alishafanya tathmini ya operesheni yake hiyo kama ilikuwa na mafanikio ama la?
Advertisement Kwa sababu bado hali ni ileile, wanaendesha vyombo vya moto hawana leseni, hawavai helmet, wanabeba mishikaki, wanaendesha mwendo hatari, wanaonyesha indiketa wasipokwenda na wanayapita magari upande wa kushoto.
Mwaka jana nilimsikiliza Rais Samia Suluhu Hassan akisema takwimu zinaonyesha katika kipindi cha miaka mitano, jumla ya wapanda pikipiki 2,220 wamepoteza maisha kutokana na ajali za barabarani na kusababisha majeruhi 4,202.
Rais alisema hii ni kusema kwa kipindi cha mwaka mmoja ndani ya kipindi hicho, tumepoteza vijana 445 kwa mwaka wanaoendesha bodaboda na hospitali zetu zilikuwa na vijana 850 kila mwaka wanaotokana na ajali za bodaboda.
Ndiyo maana nimetangulia kumkumbusha IGP Sirro kwamba sheria ni msumeno, hukata mbele na nyuma, kwamba tunataka tuone yeye na Jeshi lake wakiguswa pia na vifo vinavyotokana na ajali za bodaboda tusibaki kwenye magari tu.
Sitaki sana kumlaumu IGP Sirro, wapiganaji na wadau wengine katika suala la usalama barabarani kwa sababu sote ni mashahidi jinsi trafiki waliowakamata bodaboda na bajaji awamu iliyopita walivyodhalilishwa.
Bahati mbaya sana katika kipindi cha miaka mitano (2015-2020) katika nchi yetu limekuja jambo la kutisha sana, kwamba tunasema hakuna mtu au taasisi ambayo iko juu ya sheria au nje ya sheria lakini bodaboda na bajaji hawaguswi.
Tunasema kila mmoja wetu anawajibika kwa sheria, iweje upo utawala wa siasa? Yapo maamuzi yanayofanyika kwa kuwapendeza watu fulani ambao bila kufanya hivyo itakuwa hasara ya kisiasa na hapo sheria inawekwa pembeni.
Kwa maneno mengine, maamuzi yanafanywa kwa woga kukidhi mahitaji ya kisiasa ya wakati husika, na sio kwa kuheshimu sheria ambayo haipindi haki wala wajibu kama suala la bajaji na bodaboda lilivyokuwa miaka hiyo mitano.
Tukiacha siasa itawale badala ya sheria, utekelezaji wa sheria bila woga wala upendeleo unasahauliwa, na ni vigumu kuelezea kwa ukamilifu hasara ambayo utawala wa siasa utailetea nchi yetu kama ilivyo sasa bodaboda na bajaji.
Leo hii ni kama Bodaboda na Bajaji wanasimamiwa na sheria tofauti na wana kinga ya kufanya makosa ya barabarani ambayo ni chanzo cha vifo vingi vya watu wasio na hatia, kwa sababu hawavai helmet na wanapita mbele ya trafiki.
Lakini leo tukifanya operesheni ni Bodaboda na Bajaji wangapi wana leseni au vyombo vyao vimekatiwa bima nafikiri tutaingia kwenye kitabu cha maajabu ya dunia cha Guiness kwa kuwa nchi iliyoshindwa kusimamia sheria zetu.
Ni kweli kama IGP alivyosema ni jambo lisilokubalika watu wanakufa 20 kwa mpigo kwenye ajali za barabarani, lakini hebu awaangalie kwa jicho la huruma pia watanzania wanaopoteza maisha kutokana na ajali za Bodaboda na Bajaji.
Inawezekana bado kuna kivuli cha awamu ya tano bado kinawasumbua watendaji wengi, lakini tukubali kuwa Rais Samia Suluhu anairudisha nchi kwenye utawala wa sheria, hivyo polisi timizeni wajibu wenu tuone kama mtawajibishwa.
Operesheni zisilenge tu madereva wa magari madogo, mabasi na malori na kama nilivyosema sheria ni msumeno, hebu fanyeni pia operesheni ya kudhibiti ajali za Bajaji na Bodaboda kwa sababu uhai wa watanzania unaopotea unatisha.
0656600900