Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

IGP Sirro akerwa na mauaji

11355 Igp+pic.png TanzaniaWeb

Sat, 14 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Sengerema/Misungwi. Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro ameeleza kukerwa na mauaji ya watu yanayotokana na wivu wa kimapenzi yanayoendelea nchini.

Akizungumza na wananchi wilayani Sengerema akiwa ziarani kukagua utendaji kazi wa Jeshi hilo juzi, alisema kati ya vitu vinavyomuumiza kichwa ni matukio ya watu wanaouawa au kujiua kutokana na wivu wa kimapenzi.

IGP Sirro alisema kitendo hicho si cha kiungwana na kuwaomba viongozi wa dini kushirikiana na Serikali kukomesha mauaji hayo.

Alisema viongozi wa dini wana nafasi kubwa katika jamii kuhamasisha na kuhubiri amani.

IGP Sirro alitoa mfano wa wanandoa waliouana kutokana na wivu wa kimapenzi wilayani Sengerema Juni 19 katika Kijiji cha Kanyala kwenye nyumba ya kulala wageni ya Enjoy.

Katika tukio hilo, Michael Daudi (31) alimuua mpenzi wake Tekera Lutandula (30) na baadaye alijiua.

Akizungumza katika ziara hiyo, Padri Thomas Bilingi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Sengerema alisema wanapaswa kuisaidia Serikali katika jitihada za kupambana na mauaji hayo kwa kutoa elimu kwa waumini.

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole alisema umoja na mshikamano wa viongozi wa dini na Serikali ndiyo silaha ya kumaliza vitendo viovu.

Katika hatua nyingine, IGP Sirro ameikataa taarifa ya Mkuu wa Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, Juma Sweda kuwa hali ya ulinzi na usalama ni shwari wakati kuna mauaji ya wanawake.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Misungwi jana, IGP Sirro alisema hali si shwari kwa kuwa kuna vifo vinavyotokana na wanawake kunyongwa. Aliwataka viongozi kuimarisha ulinzi kwenye maeneo yao akisema, “Kuna haja gani ya mimi kuwapo kwenye nafasi hii iwapo kuna wananchi wanauawa, vivyo hivyo viongozi wengine ngazi ya mitaa, kijiji na wilaya kama wananchi wake wanauawa hafai kuwa kwenye nafasi hiyo.”

Awali, DC huyo alisema hali ya ulinzi na usalama wilayani kwake ni shwari hakuna matukio ya mauaji ya kutisha.

Katika mkutano huo, diwani wa Gulumungu, Enos Mihayo alisema kwenye kata yake kulitokea mauaji ya wanawake wawili walionyongwa mwezi uliopita huku Flora Marongo wa chama cha ACT Wazalendo akisema kuna matukio matatu yamejitokeza Misungwi ya vijana kuuawa wakiwa mikononi mwa polisi.

IGP Sirro alisema hayupo mtu aliye juu ya sheria, hivyo taarifa zilizotolewa na wananchi zitafanyiwa kazi.

Chanzo: mwananchi.co.tz