Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

IGP Sirro afunguka mazito mauaji Mtwara

Sirropic Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro

Fri, 18 Feb 2022 Chanzo: mwananchidigital

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro amesema haikuwa kazi rahisi kuchunguza, kuwakamata na kufikishwa kortini maofisa saba wa jeshi hilo mkoani Mtwara kwa tuhuma za kumuua mfanyabiashara wa madini na kumpora mamilioni ya fedha.

Alisema ugumu wa suala hilo ulitokana na kuwahusisha maofisa wa jeshi hilo hivyo uchunguzi wake kuhitaji muda na umakini mkubwa.

IGP Sirro alisema sakata hilo lilianza Oktoba mwaka jana lakini lilifika mezani kwake Januari 17 mwaka huu.

Januari 26, kupitia gzei la Mwananchi ilitoka taarifa kuhusu sakata hilo kuwa inadaiwa maofisa hao walimpora mfanyabiashara wa madini, Hamis Mussa Sh70 milioni na kisha kudaiwa kumuua kwa kumchoma kwa sindano ya sumu na kuutupa mwili wake baharini.

Vyanzo mbalimbali kutoka ndani ya Jeshi la Polisi vililidokeza kuwa mauaji hayo yalifanyika katika hospitali ya Jeshi la Polisi mjini Mtwara Oktoba mwaka jana, lakini taarifa za mauaji hayo zikavuja mwezi uliopita.

Sirro alisema baada ya kupata taarifa za tuhuma hizo zinazowahusu maofisa wa jeshi hilo walianza kufanya uchunguzi uliowezesha wahusika kufikishwa mahakamani.

“Ukweli hili jambo lilikuwa na ugumu kwa kuwa liliwahusisha maofisa wa polisi, hivyo hata namna ya kwenda nalo lilihitaji weledi na umakini, lakini sisi tumefanya kazi kubwa ambayo nilitarajia ingechukuliwa kwa mtazamo chanya lakini hali ilikuwa tofauti,” alisema.

“Sisi ndiyo tuliochunguza na baadaye tukawa wazi kwa kutangaza kwa umma hatua tulizozichukua dhidi ya maofisa wale, hatuna kitu cha kuficha kwa kuwa anayefanya uhalifu hatumwi na taasisi yetu bali ni tabia yake,” alisema.

Sirro alisema si sahihi watu kulihusisha Jeshi la Polisi na matukio au tabia za ukiukaji wa maadili, haki za binadamu, uhalifu, sheria, taratibu na miongozo ya taasisi hiyo zinazofanywa na baadhi ya waajiriwa.

“Unajua tunaajiri askari si kutoka Marekani au taifa jingine lolote, tunaajiri kutoka kwenye jamii, hivyo kama kuna wahalifu tusitarajie watakosekana kwenye taasisi yetu, la msingi tunalolifanya ni kuwawajibisha wale wote wanaokwenda kinyume” alisema

Akiongea kwa tahadhari, IGP Sirro alisema suala la maofisa hao lilifanyika kwa kificho ndiyo maana lilichukua muda kubainika na kuanza kwa uchunguzi.

Alisema kwa kuwa jambo hilo lilikuwa likiwahusu maofisa ambao walikuwa eneo la tukio, hivyo haikuwa rahisi kwa watu wengine kubaini kilichofanyika lakini kwa kuwa Jeshi la Polisi lina watu wenye weledi wanaoijua kazi yao, walifanikiwa kujua nini kilifanyika

“Asilimia 90 ya tuhuma za mauaji zinazotokea hapa nchini Jeshi la Polisi tunafanikiwa kuwatia mbaroni wahusika ndiyo maana huwa nashangaa ninaposikia malalamiko ya watu yanayoonyesha jeshi letu ni la kulinda wasiofuata maadili ya kazi waliyopewa,” alisema.

Kuhusu kukithiri kwa matukio ya uhalifu, mkuu huyo wa polisi alisema si kazi ya taasisi yake pekee katika kuyazuia, bali kunahitajika ushirikiano wa wadau mbalimbali kwa kuwa nchi inapokuwa na amani shughuli mbalimbali zinafanyika kwa uhuru na ufanisi zaidi.

Chanzo: mwananchidigital