Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Huu hapa mchakato mzima rufaa ya Sabaya na wenzake

Cctv Sabaya Lengai Ole Sabaya, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Hai

Mon, 9 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Siku Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili walipohukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha, baadhi ya wananchi walishangilia wakiamini haki imetendeka. Wengine walitoa machozi ya uchungu wakidai haki haikutendeka.

Lakini juzi Mahakama Kuu ilipotengua mwenendo wa kesi iliyomhukumu na kuamuru aachiwe huru, wapo walioshangilia wakiamini haki imetendeka na kuwaacha wengine na maswali jinsi sheria inavyofanya kazi.

Sabaya alishtakiwa kwa tuhuma hizo alizozitenda akiwa madarakani, Arumeru alikokuwa mkuu wa wilaya hiyo.

Ni sababu zipi ziliifanya Mahakama ya Hakimu Mkazi, Arusha iwape adhabu hiyo na ni sababu zipi zimeifanya Mahakama Kuu kuitengua ndilo swali ambalo limeacha gumzo baada ya Sabaya na wenzake kuachiwa.

Gazeti lako la Mwananchi linakuletea ufafanuzi wa kina katika mfululizo wa mapitio ya hukumu iliyotamka Sabaya na wenzake si wafungwa tena bali watu huru.

Related Sabaya, wenzake washinda rufaa Hukumu rufaa ya Sabaya leoAdvertisement Ilivyokuwa

Juni 4 mwaka jana, Sabaya na wenzake wawili, Silvester Wenceslaus Nyegu na Daniel Gabriel Mbura walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha wakishtakiwa kwa makosa sita, yakiwamo ya kuhujumu uchumi na unyang’anyi wa kutumia silaha kinyume na Kifungu cha 287 (A) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Habari za kukamatwa Sabaya zilitawala vichwa vya habari vya magazeti na mitandao ya kijamii nchini kutokana na ukweli kuwa aina yake ya uongozi ilielezwa kuyaudhi makundi kadhaa ya watu na kuwafurahisha mengine.

Siku hiyo, mamia ya wananchi wa Mkoa wa Arusha na vitongoji vyake walifurika mahakamani hapo kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo iliyokuwa na mvuto ndani hata nje ya nchi.

Katika shitaka la kwanza, ilielezwa kuwa Februari 9 mwaka 2021 katika Mtaa wa Bondeni mkoani Arusha, akina Sabaya waliiba Sh2.7 milioni mali ya Mohamed Saad na baada ya wizi huo walimshambulia Numan Jasin, Hajirini Saadi Hajirin, Bakari Rahibu Msangi, Salim Hassan na Ally Shaban na walitumia bastola kuwatisha ili wachukue fedha hizo.

Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa siku hiyohiyo na mahali pale pale, watu hao waliiba Sh390,000 kutoka kwa Bakari Msangi na baada ya wizi huo walimfunga pingu, kumpiga wakitumia silaha aina ya bastola kumtisha ili wachukue pesa zilizokuwapo.

Jamhuri ilidai katika shitaka la tatu kuwa akina Sabaya waliiba Sh35,000 na simu moja ya mkononi aina ya Tecno POP1 kutoka kwa Ramadhani Rashid, maarufu kama Anusu, wakamfunga pingu na walitumia bastola kumtisha ili wazimiliki pesa zile.

Mahakama yapokea ushahidi

Shahidi wa kwanza katika kesi hiyo alikuwa Mohamed Saad Harijin, anayemiliki duka katika eneo la Soko Kuu. Alidai siku ya tukio (Februari 9 mwaka 2021) duka hilo lilikuwa likisimamiwa na Numas Jasin na Ally. Alidai muda wa saa 11 jioni kundi la watu wasiopungua 11 waliingia dukani kwake.

“Walikwenda hadi kaunta, wakakutana kwanza na Numas. Kiongozi wa kundi hilo alimuuliza alipo Mohamed ambaye ndiye mmiliki wa duka hilo. Mohamed hakuwepo dukani na kiongozi wa kundi hili alimwelekeza Numas ampigie simu na kumjulisha wanunuzi wa jumla katika duka lake walikuwa wakimtafuta.

Alipopigiwa, Mohamed alimjulisha Numas kuwa alikuwa mbali na duka. Alishikilia msimamo wake huo hata pale alipoambiwa kuwa watu waliokuwa dukani kwake walikuwa maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Jibu la Mohamed halikumfurahisha kiongozi wa kundi hilo ambaye aliomba simu kuongea naye na kumwamuru awe amefika dukani kwake ndani ya dakika tano.

Wakati huohuo, kiongozi huyo aliwaamuru wenzake waliojulikana kama walinzi wake au mabaunsa wake kufanya upekuzi, kumtia nguvuni na kumpiga Ally.

Mohamed alidai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kuwa walinzi hao waliendelea na upekuzi na walimpiga na kumtia nguvuni Mzee Salim na Ramadhani Rashid ambao walikuwa wameingia dukani hapo kwa nyakati na mahitaji tofauti.

Kwa mujibu wa ushahidi wa Ramadhani, simu yake aina ya Tecno POP1 na kiasi cha Sh35,000 zilichukuliwa na watu hao.

Ilidaiwa pia kuwa haukupita muda, Hajirin ambaye alikuwa ameombwa na Mohamed kufika dukani pale kwa lengo la kujua kilichokuwa kikiendelea aliwasili.

Katika ushahidi wake, Hajirin alidai kumtambua kiongozi wa kundi lile kuwa alikuwa Lengai Ole Sabaya kwa kuwa alizoea kumwona kwenye televisheni na kwenye mitandao ya kijamii.

Hajirin alidai katika ushahidi wake alioutoa kwa kiapo kuwa kiongozi huyo alimwamuru ampigie Mohamed. Alidai baada ya Mohamed kuwa hapatikani tena kwenye simu yake, watu wale walimpekua, wakampiga na kumtia nguvuni.

Wakati hayo yakiendelea, mtu mwingine, Bakari Msangi ambaye ni Diwani wa Sombetini aliingia dukani hapo. Aliwasalimia na kuanza kuongea na Sabaya kwani tayari walikuwa wakifahamiana. Msangi alimjulisha Sabaya kuwa alikuwa ameombwa na Ally Hajirin (kaka wa Mohamed) kufika pale na kujua nini kimetokea kwenye duka lake.

Baada ya kumweleza hayo, Bakari alidai kuwa Sabaya alimweleza kuwa Mohamed alikuwa ametenda kosa la uhujumu uchumi kwa kuuza bidhaa bila kutoa risiti na kubadilisha fedha bila leseni.

Na Bakari alipomweleza Sabaya kuwa mamlaka yake kama mkuu wa Wilaya ya Hai yasingeweza kuvuka hadi Wilaya ya Arusha, Sabaya aliwaamuru mabaunsa wake wampekue, wampige na kumtia nguvuni. Alidai pia kuporwa Sh390,000.

Kwa mujibu wa ushahidi wa Abu Mansur, Ramadhani Anas, Ally, Mzee Salim na Bakari Msangi waliachiwa na Numas Jasin na Hajirin Saad waliendelea kushikiliwa na Sabaya na mabaunsa wake.

Ilielezwa zaidi mahakamani hapo kuwa Sabaya na mabaunsa wake walikusanya nyaraka mbalimbali, mashine ya EFD, simu za mkononi na Sh2.6 milioni kutoka kwenye duka hilo.

Mohamed aliendelea kudai kuwa baada ya operesheni hiyo, Sabaya na kundi lake waliwapeleka Numas na Hajirin hadi Kituo Kikuu cha Polisi Arusha na kuwakabidhi kwa Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Gwakisa Venance Milinga.

Vilevile, Msangi aliripoti tukio hilo polisi, ripoti ambayo anadaiwa ndiyo iliyosababisha kuanzishwa kwa upelelezi wa tukio hilo hatimaye kukamatwa na kushtakiwa kwa Sabaya na wenzake.

Watu wengine waliotoa ushahidi katika kesi hiyo ni Selemani Kassim Msuya ambaye alidai kumwona Sabaya na walinzi wake wakiingia katika duka la Mohamed, ASP Milinga, wakati huo akiwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha ambaye alilipeleleza tukio hilo.

Wengine ni Magdalena Malya aliyejitambulisha kama mke wa Msangi, Inspekta Evarist Mwamengo, askari polisi aliyeendesha gwaride la utambuzi, Niana Mtui, daktari aliyemtibu Msangi na askari mpelelezi James.

Mbali na mashahidi hao, Jamhuri ilitoa vielelezo vinane wakati wa usikilizaji wa kesi hiyo.

Usikose mwendelezo wa mfululizo huu kesho ambapo tutaona jinsi washitakiwa walivyojitetea mbele ya hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha. Tukutane kesho...

Chanzo: www.tanzaniaweb.live