Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hukumu ya Tido Mhando Desemba 18

Sat, 17 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam Desemba 18 itatoa hukumu ya kesi inayomkabili aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando.

Tido ameshtakiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka wakati akiongoza shirika hilo ambapo anakabiliwa na mashtaka manne ya kutumia madaraka vibaya na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh887.1 milioni.

Hatua hiyo ilifikiwa leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai kuieleza Mahakama kuwa wamekwisha wasilisha majumuisho yao ya mwisho mahakamani hapo.

Wakili wa Tido, Dk Ramadhani Maleta aliitaarifu Mahakama kuwa wakili mwenzake, Martin Matunda amefariki dunia na kwamba na wao pia wamekwisha wasilisha hoja zao za mwisho.

Baada ya kueleza hayo, wakili Swai aliiomba Mahakama kuipangia kesi hiyo tarehe ya hukumu na hakimu Shaidi akapanga kutoa hukumu Desemba 18.

Oktoba 30 Tido kupitia mawakili wake, Martin Matunda na Dk Ramadhani Maleta walifunga ushahidi wa upande wa utetezi.

Miongoni mwa  mashahidi  wa upande wa mashtaka waliotoa ushahidi  katika kesi hiyo ni ofisa uchunguzi wa Takukuru, Victor Lesuya, mwanasheria wa TBC, Gwakisa Mlawa na mkurugenzi Mkuu mstaafu wa TBC, Clement Mshana.

Katika kesi hiyo, inadaiwa Juni 16 mwaka huu akiwa  Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Tido ambaye alikuwa mkurugenzi wa TBC, kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa kuendesha na utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BV1) bila ya kupitisha zabuni, kitu ambacho ni kinyume cha Sheria ya Manunuzi na kuinufaisha BVl.

Katika shtaka la pili, Tido anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake Juni 20 mwaka huu aliposaini makubaliano ya utangazaji wa digitali duniani kati ya TBC na BVl.

Katika shtaka la tatu, anadaiwa Agosti 11 na Septemba mwaka huu akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa ununuzi, usambazaji, kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BVI na kuifaidisha BVI.

Katika shtaka la nne, anadaiwa kuwa Novemba 16 mwaka huu akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa kuendesha miundombinu ya utangazaji (DTT Broadcast Infrastructure) kati ya TBC na BVI na kuinufaisha BVI.

Katika shtaka la mwisho,  anadaiwa kuwa kati ya Juni 16 na Novemba 16 mwaka huu akiwa UAE, Tido aliisababishia TBC hasara ya Sh887,122,219.19.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz