Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hukumu ya Gugai na wenzake yaahirishwa mara tatu

Gaipic Hukumu ya Gugai na wenzake yaahirishwa mara tatu

Sat, 6 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, imeshindwa kutoa hukumu ya kesi ya aliyekuwa mhasibu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai na wenzake wawili kutokana na kushindwa kukamilisha kuandikwa hukumu hiyo kwa sababu Hakimu anayesikiliza shauri hilo, Thomas Simba kuwa na udhuru.

Hii ni mara tatu kesi hiyo kushindwa kutolewa hukumu, kwani Oktoba 6, 2021 ilishindwa kutolewa kwa maelezo kuwa hakimu anayesikiliza shauri hilo, bado hajamaliza kuandika hukumu hiyo.

Pia Oktoba 22, 2021, kesi iliahirishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya, ambaye alisema kuwa Hakimu anayeendesha shauri hilo hayupo.

Wakili wa Serikali, Faraja Ngukah ameieleza Mahakama hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Joseph Luambano kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya hukumu lakini Hakimu Simba amepata udhuru hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya washtakiwa kusomewa hukumu.

Ngukah baada ya kueleza hayo, Hakimu Luambano amesema kuwa hakimu anayesikiliza shauri hilo amepata udhuru na kwamba bado hajakamilisha kuandika hukumu.

" Hakimu anayesikiliza shauri hili amepata udhuru na pia bado hajamaliza kuandika hukumu, hivyo kutokana na sababu hiyo, naahirisha kesi hiii hadi Novemba 12, 2021 itakapokuja kwa ajili ya hukumu" amesema hakimu Luambano. Advertisement

Mbali na Gugai, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ya jinai namba 382/2017 ni George Makaranga na Leonard Aloys.

Katika kesi ya msingi, Gugai na mwenzake, wanakabiliwa na makosa 40, makosa 19 kati ya hayo ni ya kughushi, 20, ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali.

Gugai anakabiliwa na kosa la kumiliki mali kinyume na kipato chake, ambapo anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Januari 2005 na Desemba, 2015.

Inadaiwa mshitakiwa akiwa jijini Dar es Salaam kama mwajiriwa wa Takukuru alikuwa akimiliki mali za zaidi ya Sh3.6 bilioni, ambazo hazilingani na kipato chake cha awali na cha sasa, huku akishindwa kuzitolea maelezo.

Chanzo: mwananchidigital