Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hukumu washtakiwa 3 Scolastica leo

61065 PIC+SCOLASTICA

Mon, 3 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Mahakama Kuu kanda ya Moshi, leo itatoa hukumu kwa washtakiwa watatu wanaokabiliwa na kesi ya mauaji ya kukusudia ya mwanafunzi wa Shule ya Scolastica, Humphrey Makundi.

Hukumu hiyo itasomwa na Jaji Firmin Matogolo aliyeisikiliza na tayari mawakili wa pande zote walipelekewa hati za kuitwa shaurini (summons).

Mwanafunzi huyo anadaiwa kuuawa Novemba 6, 2017 na mwili wake kutupwa mto Ghona uliopo mita 300 kutoka ilipo Shule ya Scolastica na baadaye ukazikwa na Manispaa ya Moshi kabla ya kufukuliwa.

Wakili David Shillatu anayemtetea mshtakiwa wa kwanza, Hamis Chacha ambaye ni mlinzi wa shule hiyo, aliiambia Mwananchi jana kuwa amepokea hati hiyo ikionyesha hukumu hiyo itasomwa kuanzia saa 3:00 asubuhi.

Mbali na Chacha, washtakiwa wengine katika kesi hiyo, mmiliki wa shule hiyo, Edward Shayo na mwalimu Laban Nabiswa.

Washtakiwa hao wanaotetewa na jopo la mawakili wanne, Elikunda Kipoko, Gwakisa Sambo, Shillatu na Patrick Paul, wamekanusha mashtaka hayo na kuiomba mahakama iwaachie huru.

Pia Soma

Katika utetezi wao, waliegemea ushahidi kuwa siku ya tukio hawakuwahi kufika Mto Ghona wala kufika karibu na mazingira ya mto huo, ambako maiti ya Humphrey ilipatikana.

Mshtakiwa wa kwanza, Chacha aliyakana maelezo ya ungamo ambayo ndio msingi wa kesi hiyo akisema aliyatoa baada ya kufanyiwa mateso ya aina nane ili akubali kuyaandika.

Hata hivyo, mashahidi wa upande wa mashtaka walipinga utetezi huo wa Chacha na kueleza kuwa maelezo hayo yanayoeleza namna mauaji yalivyotendeka, aliyatoa kwa hiari bila kushurutishwa.

Katika maelezo hayo, Chacha anadaiwa kueleza kuwa siku ya tukio usiku, alimkurupusha mtu aliyeruka ukuta na kumkimbiza hadi uraini ambako alimpiga kwa ubapa wa panga alilokuwa nalo.

Baadaye mtu huyo alianguka na kupasuka fuvu na yeye aliendelea kumpiga kwa ubapa hadi alipotulia, kisha akawapigia mmiliki wa shule na mwalimu Laban ambao walifika katika eneo hilo.

Kulingana na maelezo hayo, mmiliki wa shule ndiye anayedaiwa kutoa maelekezo kwa Chacha na Nabiswa kuubeba mwili huo na kwenda kuutupa Mto Ghona kwa maelezo kuwa atakuwa ni kibaka.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Joseph Pande, ulitoa mahakamani mawasiliano ya simu, ambayo unadai washtakiwa waliwasiliana usiku huo wakati wakiitana.

Chanzo: mwananchi.co.tz