Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hukumu rufaa ya kina Pima yakwama tena

Sef Pima Ded Arusha Hukumu rufaa ya kina Pima yakwama tena

Fri, 9 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hukumu ya rufaa iliyokatwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dk John Pima na wenzake wawili iliyopangwa kutolewe leo imeahirishwa hadi Februari 16, 2024.

Akiahirisha hukumu hiyo leo Februari 9, 2024, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Fredrick Lukuna amesema jaji aliyekuwa akisikiliza rufaa hiyo yuko nje ya kituo cha kazi, hivyo hukumu itasomwa Februari 16, 2024.

Hii ni mara ya pili kuahirishwa kwa hukumu hiyo, awali ilipangwa kutolewa Januari 18, 2024, siku hiyo Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mariam Mchomba alisema bado haikuwa imekamilika kuandikwa.

Dk Pima na wenzake, aliyekuwa mweka hazina wa Jiji, Mariam Mshana na aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Mipango, Takwimu na Ufuatiliaji, Innocent Maduhu walihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja.

Mchomba alieleza rufaa hiyo ilipangwa kwa ajili ya hukumu ila kutokana na hukumu hiyo kutokukamilika kuandikwa, inaahirishwa hadi Februari 9, 2024.

Dk Pima na wenzake, baada ya kutoridhishwa na hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, walikata rufaa iliyosikilizwa mwishoni mwa mwaka 2023 na Jaji Angaza Mwipopo.

Waomba rufaa hao walikuwa na sababu saba za rufaa ikiwemo Mahakama iliyowafunga haikuwa na mamlaka kwa sababu hakukuwa na idhini ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), kumshitaki mteule wa Rais.

Nyingine wanadai kesi hiyo haikuwa imethibitishwa kupita kiwango cha mashaka na hakimu kushindwa kuchambua ushahidi ipasavyo na makosa mengine hayakuthibitika.

Agosti 31, 2023 Hakimu Mkazi Serafini Nsana aliyekuwa akisikiliza kesi ya uhujumu uchumi namba 5/2023 aliwahukumu kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja.

Walikuwa wakikabiliwa na makosa tisa, likiwamo utakatishaji wa Sh103 milioni.

Mei 24, 2022 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwasimamisha kazi watumishi sita wa Halmashauri ya Jiji la Arusha akiwamo Dk Pima ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Mbali na kesi hiyo, kina Dk Pima wanakabiliwa na mashauri mengine mawili, wakishtakiwa kwa makosa manane, likiwamo la ufujaji, ubadhirifu na matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri.

Katika mashauri hayo, washtakiwa walishasomewa maelezo ya awali na zilikuwa zikisubiri kukamilika kusikilizwa kesi namba 5/2022 ndipo zianze kusikilizwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live