Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hukumu kesi ya Lucky Vicent yapigwa kalenda hadi Juni 7

60177 Pic+luck+vicent

Thu, 30 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Hukumu ya kesi inayomkabili  mmiliki wa Shule ya Msingi Lucky Vicent, Innocent Moshi na mwalimu mkuu msaidizi wa shule hiyo, Longino  Vicent (40) kuhusiana na ajali ya basi la shule hiyo iliyosababisha vifo vya wanafunzi 32, walimu wawili na dereva itatolewa Juni 7, 2019.

Ajali hiyo ilitokea Mei 6, 2017, katika eneo la Rhotia wakati wanafunzi wa shule hiyo wakitoka Arusha majira ya saa 12 asubuhi kwenda wilayani Karatu, katika mitihani ya ujirani mwema katika Shule ya Tumaini Academy.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Niku Mwakatobe  leo Jumanne Mei 28, 2019 alikuwa asome hukumu hiyo lakini ameahirisha kutokana na kutokamilika kuandikwa.

Katika kesi hiyo, washitakiwa wanakabiliwa na jumla ya mashitaka matano ya kuvunja sheria za usalama barabarani, ikiwemo kuendesha gari za abiria bila kuwa na lesseni ya usafirishaji, gari lililosababisha ajali kutokuwa na bima, kushindwa kuingia mkataba baina ya dereva na mwajiri na kosa la kuzidisha abiria 13 katika gari lililopata ajali ambalo linamkabili mwalimu mkuu msaidizi.

Washitakiwa hao, wanatetewa na wakili, Method Kimomogoro ambapo walikana mashitaka hayo, katika utetezi wa mwisho ambao waliutoa Machi 19 mwaka huu.

Moshi aliieleza mahakama kuwa, Mei 9, 2017, alikamatwa na polisi na kuwekwa ndani kwa sababu ya ajali hiyo na baada ya siku tatu alipelekwa mahakamani na moja ya makosa aliyoshitakiwa ni kosa la kuendesha gari bila kuwa na leseni  ya biashara.

Habari zinazohusiana na hii

Alisema pia alishitakiwa kwa kosa la kutumia gari bila kuwa na bima na kuwapakia wanafunzi  38 ndani ya basi dogo kinyume na sheria kwani linapaswa kubeba abiria 25.

Alisema kuwa yeye hajatenda makosa hayo pia kampuni ya Lucky Vincent iliuziwa gari na Swalehe Kiluvia na kuwakabidhi kadi ya gari, bima ya gari na leseni ya gari hilo.

Mshitakiwa wa  pili Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo, Longino Vicent (40) aliieleza mahakama kuwa Mei 6, 2017, alifika shuleni saa 12 asubuhi na kushughulikia zoezi la usafiri wa wanafunzi aliopewa na mwalimu mkuu na gari tatu za kwenda Karatu.

Vicent alikanusha kuhusika na ajali hiyo kwani hakuwepo eneo la tukio na yeye alitimiza wajibu aliokabidhiwa na mkuu wa shule kuwasafirisha wanafunzi hao wakiwa na walimu wao.

Chanzo: mwananchi.co.tz