Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hukumu faini ya Sh200,000 kwa raia wa kigeni mjadala

Jongoo Jongoo Hukumu faini ya Sh200,000 kwa raia wa kigeni mjadala

Fri, 21 Jul 2023 Chanzo: mwanachidigital

Hukumu ya raia wa China, Wei Zhang (54) kutakiwa kulipa faini ya Sh200,000 baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na kilo nne za majongoo bahari yaliyo hatarini kutoweka, imezusha mjadala miongoni mwa wadau, wakiwamo wanasheria.

Hatua hiyo imetokana na kile walichodai kuwa, baadhi ya sheria zimekuwa zikitoa mwanya kwa watuhumiwa wa makosa makubwa, yakiwemo yanayoangukia kwenye uhujumu uchumi, kuepuka vifungo huku wengine waliotenda makosa yanayoonekana ya kawaida kufungwa gerezani.

Kutokana na hatua hiyo, baadhi ya wadau wameshauri kufanyike marekebisho ya sheria, ikiwemo kuweka adhabu kali ama kupunguza kwa makosa mbalimbali ili kuendana na uzito na wakati pia.

Juzi, Zhang ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Kinondoni, Dar es Salaam, alihukumiwa adhabu hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kukiri shtaka lake.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kumiliki samaki hao walio hatarini kutoweka kinyume cha sheria kifungu cha 23(1) cha Sheria ya Uvuvi ya mwaka 2003, kikisomwa pamoja na kifungu cha 13(2), 67, 128 na aya ya C ya jedwali la tatu la Kanuni ya Sheria ya Uvuvi ya mwaka 2009.

Kupitia sheria hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, alimhukumu kulipa faini ya Sh200,000 au kwenda jela mwaka mmoja.

Mshtakiwa huyo alilipa faini hivyo kukwepa adhabu ya kifungo.

Akizungumza na Mwananchi, Wakili, Timon Vitalis alisema ni vyema sheria zilizopo zikapitiwa upya na kuzifanyia marekebisho pale inapobidi ili ziendane na mazingira na mahitaji ya sasa. Alisema baadhi ya adhabu, ikiwemo vifungo na fidia, zilikuwa zimeangalia mazingira ya wakati huo ambapo huenda faini ya Sh200,000 ilikuwa pesa nyingi.

“Unajua hizi sheria, vifungu vya adhabu kuna vya aina mbili, moja vinavyoweka adhabu ya juu bila kuweka adhabu ya chini, hivyo vinampa mtu uamuzi wa kukadiria adhabu kulingana na mazingira ya kesi.

“Aina ya pili ya vifungu vya adhabu, kuna vifungu vinavyombana mtoa adhabu, kwa kuweka kiwango cha chini cha adhabu na kuna vifungu ambavyo vinaweka adhabu ya chini itakuwa ni hii na ya juu itakuwa ni hii,” alisema.

Hata hivyo, alisema kuwa changamoto kubwa ni thamani ya fedha kushuka ama kupanda na hivyo kuleta athari.

“Mfano sheria ya uvuvi ya mwaka 2003, mtu kulipa faini ya Sh200,000 ilikuwa ni pesa nyingi kwa wakati huo, hata waliokuwa wanalipwa mshahara wa Sh200,00 serikalini walikuwa ni wachache. Sasa unaweza kuona kwa wakati huo kiasi hicho cha fedha kilikuwa ni kikubwa, hivyo hata watu waliokuwa wanapewa adhabu kwa wakati ule ya kulipa faini hiyo ilikuwa ni adhabu kubwa. Kwa muktadha huo, nadhani kuna haja ya kupitia baadhi ya sheria na kuzifanyia marekebisho pale inapobidi ili ziende na wakati,” alisema Vitalis.

Mwenyekiti wa Mawakili Vijana kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS,) Edward Heche alisema zipo sheria nyingi ambazo zinatakiwa kufanyiwa marekebisho ili kwenda na wakati, ikiwemo ya makosa ya usalama barabarani.

“Adhabu aliyopewa raia wa China inachochea wengine kufanya kosa zaidi kuliko kujutia kosa kwa sababu wanajua adhabu yake ni kulipa faini, hivyo ni vizuri Serikali iweke adhabu kubwa ili kuendana na wakati wa sasa,” alisema Heche.

Hukumu ilivyotolewa

Mbali na mahakama hiyo kutoa adhabu dhidi ya mshtakiwa huyo, pia imetaifisha majongoo hayo na kuwa mali ya Serikali na yatarejeshwa kwenye mamlaka husika.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, alisema:

"Kwa kuwa mshtakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza, mahakama hii inakupiga faini ya Sh200,000 na ukishindwa kulipa basi utatumikia kifungo cha mwaka mmoja jela.’’

Kabla ya kutoa adhabu, aliuliza majongoo hayo yapo katika hali gani. Mmoja wa maofisa wa viumbe hai wa baharini, aliyekuwa ameyabeka katika mfuko aliyafungua na kuonyesha Mahakama kuwa yapo katika hali nzuri kwa sababu yamekaushwa.

Baada ya maelezo, Hakimu Shaidi alitoa uamuzi wa kuyataifisha kuwa mali ya Serikali. Mshtakiwa alipopewa nafasi ya kujitetea aliomba apunguziwe adhabu kwa kuwa ni kosa lake la kwanza na hakujua kuna sheria inayokataza kumiliki jongoo hao.

Chanzo: mwanachidigital