MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu inatarajia kutoa hukumu, dhidi ya aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Cosmas Mwaifwani, na mwenzake Oktoba 22, mwaka huu.
Uamuzi huo ulifikiwa jana katika mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Mwaifwani na aliyekuwa Meneja Ununuzi wa MSD, Fredrick Nicolous, wanakabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka na kusababisha Kampuni ya H.H Hillal kupata manufaa ya zaidi ya Sh milioni 400.
Wakili wa Serikali Janeth Kafuko akiiwakilisha Jamhuri, alidai kesi ilikuja jana, kwa ajili ya hukumu, washtakiwa wote walikuwapo, lakini mawakili wao hawakuwapo.
Hakimu Simba alisema pande zote mbili ziliwasilisha hoja za mwisho za majumuisho na mpaka jana alipokea hoja hizo, hivyo atazipitia na kutoa hukumu Oktoba 22.
Katika kesi hiyo, upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi 10 na upande wa utetezi washtakiwa walijitetea wenyewe.
Washtakiwa walifikishwa mahakamani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakidaiwa kutenda kosa hilo kati ya Machi Mosi hadi 19, 2013 katika makao makuu ya MSD, Keko, Temeke, Dar es Salaam.
Inadaiwa washtakiwa wote kwa pamoja wakiwa waajiriwa wa MSD walitumia vibaya madaraka yao kwa kuandaa na kufanya mabadaliko ya mkataba namba 1, wenye kumbukumbu MSD/003/Q/G/2010/2011/60 wa Machi Mosi, 2013 na kupitisha namba mbili wenye kumbukumbu namba kama hiyo wa Machi 19, 2013.
Inadaiwa kitendo hicho kilisababisha Kampuni ya H.H Hillal kupata manufaa yasiyokuwa ya halali ya Sh 482,266,000.