Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

House girl aeleza jinsi bosi wake alivyojiua ndani ya banda la kuku

16664 Pic+kujinyonga TanzaniaWeb

Tue, 11 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Happylight Mushi (65) mkazi wa Tabata Kisiwani jijini Dar es Salaam amekufa baada ya kujinyonga na kipande cha khanga ndani ya banda la kuku.

Tukio hilo limetokea leo saa 3 asubuhi nyumbani kwake.

Akielezea tukio hilo mfanyakazi wa ndani wa marehemu, Roida Mwoka alisema bosi wake (marehemu) aliamka asubuhi na mapena akiwa mzima na ilipofika saa 3:00 asubuhi alitoka nje akiwa amebeba misumari mkononi na kuingia katika banda la kufugia kuku.

“Tulikuwa hapa nje tunafua, tukamuona baba akiwa na misumari, aliingia ndani ya banda la kuku akawa anagongelea misumari, baada ya muda alitoka nje akaingia ndani na baadaye tena akarudi kwenye banda akaendelea kugongelea misumari,” alisema Mwoka.

Alisema baada ya kumaliza kugongelea misumari alimuona akizunguka nyuma ya banda la kuku na alikaa huko muda mrefu. “Baada ya muda alikuja mke wa marehemu, Martha Mushi alikuwa anaangalia mkaa akaulizia, baba yuko wapi?”

“Tukamwambia yuko kwenye banda la kuku, mama akaingia ndani ya hilo banda mara akaanza kupiga kelele akisema,’Baba Noel kwanini umefanya hivyo? Na mimi nikaenda kuangalia nikakuta baba kajinyonga kwa kutumia khanga,” alisema Roida.

Alisema baada ya kuona tukio hilo, mke wa marehemu alimtuma mjukuu wake,  Beatrice Isack akamuite mjumbe wa nyumba kumi, Seleman Juma.

Mwananchi lililofika nyumbani kwa marehemu lilishuhudia polisi wakiuchukua mwili wa marehemu na kuondoka nao.

Mke wa marehemu alisema hajui sababu ya mume wake kujinyoga kwani hakukua na ugomvi wowote na alikuwa vizuri tu siku hiyo.

Alisema jana jioni marehemu aliomuaga kuwa anakwenda saluni kutengeneza nywele zake kwani zimejaa mvi.

“Tuliagana vizuri akaenda saluni  baadaye akarudi tukala chakula cha jioni. Watoto  walikuwa wamepoteza  funguo za banda la kuku tulitafuta jana usiku  tukiwa pamoja lakini hatukuziona,” alisema.

Martha alisema baada ya kukosa funguo, marehemu aliamua kuvunja mlango wa banda la kuku huku akimuhidi angeamka asubuhi kuutengeneza kabla ya kwenda mjini.

Alisema usiku huo walilala vizuri na ilipofika asubuhi marehemu aliamka na kumsikia akizungumza na simu na watu wa idara ya maji akiwauliza mbona hawajaja kusoma mita ya maji.

 “Baada ya hapo marehemu alitoka nje na kuniacha ndani amelala. Nilitoka nje baada ya muda kuongea na vijana walikuwa wakitengeneza mkaa, baada ya muda nikasema ngoja nikaangalie kuku wangu kule bandani, nageuka hivi kuangalia chumba cha pili ndani ya banda nakuta mtu ananinginia.”

“Nikastuka nikamwambia wewe, naangalia hivi naona khanga” alisema mjane huyo.

Mjukuu wa marehemu ambaye alikuwa nje akifua nguo na mfanyakazi wa ndani alisema babu yake (marehemu) aliamka asubuhi akawakuta wanafua akawauliza:  “Mnafua nguo maji yanatoka?”

“Tulimwambia maji yanatoka kidogo akasema tusifue sababu maji yanatoka kidogo yanaweza kukatika muda wowote.”

“Baada ya kusema hivyo alizunguka nyuma ya banda hakurudi tena ndio baadaye bibi akaniita na kuniomba nikamuite mjumbe wa nyumba kumi baada ya kuona babu amejinyonga,” alisema Beatrice.

Alisema kabla ya babu yake kuchukua uamuzi wa kujinyonga jana alishinda nyumbani  na alikuwa akilalamika kuumwa lakini pia alionekana kuwa na mawazo hakuwa na raha kama walivyomzoea.

Chanzo: mwananchi.co.tz