Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hofu ilivyotanda maziko ya ‘kamanda wa panya road’

34914 Panya+pic Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Salum Hamduni

Sat, 5 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Juzi asubuhi ulisambaa ujumbe mfupi wa maandishi kwenye mitandao ya kijamii unaosema, “Katika mtaa wangu Tabata darajani, mkuu wa Panya road kauawa jana (juzi), anazikwa leo (juzi) saa saba mchana. Panya road wote wa Dar es Salaam wamesema watalipiza kisasi baada ya mazishi, mkuu wa wilaya na mkuu wa mkoa tusaidieni.”

Kusambaa kwa ujumbe huo kulikuja baada ya Rajab Moris (20), anayedaiwa kuwa ni jambazi kuuawa na wananchi Januari 2, saa 11 alfariji katika eneo ya Tabata darajani alipokuwa akijaribu kupora simu ya mwanamke mmoja aliyemkuta barabarani akielekea kwenye shughuli zake.

Moris anahusishwa na kundi la Panya road lililowahi kuendesha matukio ya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam miaka ya nyuma.

Polisi wamhusisha na ujambazi

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Salum Hamduni aliwatoa hofu wananchi akisema Moris hakuwa Panya road, bali ni jambazi na hakuna kundi la Panya road.

Alisema uchunguzi wa tukio hilo unafanyika ili kubaini chanzo cha kifo na waliohusika na mauaji.

Kwa mujibu wa Hamduni, kijana huyo alikuwa anatuhumiwa kwa ujambazi lakini sio kweli kwamba ni kiongozi wa kundi hilo.

Kamanda huyo alisema polisi walifika eneo la tukio na kumkuta Moris akiwa na hali mbaya, ambapo walimchukua na kumpeleka Hospitali ya Amana, lakini baada ya muda mfupi alifariki dunia.

Hofu siku ya maziko

Lakini, hofu ilizidi kutanda zaidi ilipofika saa 9 alasiri ya juzi siku yalipofanyika mazishi yake pale baadhi ya wafanyabiashara wa maduka, vyakula, bucha na maeneo ya kutuma na kutoa fedha kwa njia ya mitandao eneo la Tabata Chama walipofunga shughuli zao kwa saa tatu wakihofia usalama wao.

Mmoja wa wamiliki wa duka linalotoa huduma ya kutuma na kutoa fedha aliyeomba jina lake lisitajwe gazeti alisema: “Nimeamua kufunga, hali ni tete, hawa watoto siyo wa mchezo. Nimesikia wanataka kulipiza kisasi kwa watu waliomuua rafiki yao wanayemwita kamanda.”

“Siyo mimi niliyefunga duka tupo wengi, angalia huo mtaa wa Darajani ambako kuna msiba. Nitafungua nitakapojiridhisha kuwa hali ni shwari, najua tutawaumiza wanaohitaji huduma, lakini hakuna jinsi.”

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi ulibaini kufungwa kwa maduka na magenge mengi ya mtaa huo hususan muda walipokuwa wakisubiri mwili wa Moris upitishwe kutokea hospitali kupelekwa nyumbani kwao, kisha makaburini kwa ajili ya maziko. Mtaa huo ulionekana kuwa tulivu huku watu wakionekana wamekaa kwenye vikundi mbele ya vibaraza vya nyumba zao wakizungumzia msiba huo.

Baadhi ya majirani walibaki kwenye nyumba zao na asilimia kubwa ya waliokuwa eneo la msibani walikuwa ni marafiki wa kijana huyo miongoni mwao waliodaiwa kujihusisha na uhalifu.

Wakati wa kusubiri mwili wa Moris ambaye alifahamika kwa majina mbalimbali kama ninja na kamanda, polisi waliokuwa na silaha za moto na mabomu ya machozi hawakubaki nyuma msibani hapo, bali waliimarisha ulinzi katika mtaa huo na karibu na nyumba ulipokuwa msiba.

Ilipotimu saa 10 jioni, mwili wa kijana huyo uliwasili nyumbani kwao na kupokewa na marafiki pamoja na majirani wachache.

Haikuchukua muda mwili huo, uliondolewa kupelekwa makuburini kwa jeneza lake kubebwa na marafiki zake ambao baadhi walikuwa wamebeba vibegi vidogo mgongoni ambavyo hakuna aliyejua ndani yake walihifadhi nini.

Hata hivyo wakati safari ya makubirini ikianza, baadhi ya watu walisikika wakipeana ushauri kuwa wasiambatane na msafara, bali watafute njia mbadala ya kufika kwa kuhofia kuongozana na vijana hao.

“Ni heri kukaa nyuma kuliko kwenda mbele, maana hapa lolote linaweza kutokea tukajumuishwa kwa sababu mazingira ya leo siyo mazuri, ndiyo maana polisi wapo hapa,” alisikika mmoja wa wakazi wa eneo hilo.

Mwingine alisikika akiwaambia wenzake waweke simu zao katika hali ya mtetemo ili hata zikiita zisisike kuepuka kuporwa na vijana hao.

Mtaa wa Darajani ulizidi kuwa tulivu wakati msafara huo ukielekea makaburi ya Chama, lakini polisi walikuwa nyuma wakiufuatilia kwa karibu na kuimarisha ulinzi huku baadhi ya watu wakionekana kuangalia kupitia madirishani kutokea katika makazi yao.

Baada ya kufikia makuburi yaliyokuwa yamezungushiwa uzio, baadhi ya watu wakiwamo majirani, walilazimika kukaa nje ya makubiri hayo wakihofia usalama wao licha ya polisi kuweka kambi eneo hilo huku wengine wakisikika wakisema kamanda anazikwa chini ya ulinzi.

Shughuli za maziko zilianza baada ya mwili kuingizwa kwenye kaburi na baadhi ya vijana walitoa ushauri wa kutumia mikono kuweka udongo kuufukia badala ya makoleo (chepe) kama ilivyozoeleka.

Hatua hiyo iliwafanya baadhi ya walioshiriki msiba huo kuhimizana kuondoka eneo hilo, mmoja wao akisema, “Jamani hapa shughuli imeshaisha kama mlivyosikia wenyewe wanataka kumfukia kamanda wao kwa kutumia mikono.”

Hata hivyo, polisi waliendelea kuimarisha ulinzi katika eneo hilo hadi taratibu za kumhifadhi marehemu zilipokamilika na waliwaamuru watu waliokuwa wamekaa jirani na makaburi waondoke kwa kile walichodai shughuli hiyo imeisha.

Katika kuhakikisha walidhamiria kuimarisha ulinzi, magari mawili ya polisi yaliingia katika mtaa huo baada ya maziko kumalizika.

Awali, kabla ya mwili huo kuwasili, mkazi wa Tabata Chama, Zainabu Mrisho alisema kijana huyo alikuwa anaonekana mara kadhaa akiwa na kundi la vijana wanaodhaniwa kujihusisha na kundi la panya road, na alifahamika kwa matukio ya wizi mtaani hapo.

“Nilikuwa sifahamu (Moris) anapoishi lakini niliambiwa na rafiki yangu kwamba yumo kwenye kikundi cha panya road na hivi ameuawa watatafuta namna ya kulipiza kisasi,” alisema Zainabu.

Mjomba amlilia mpwaye

Hata hivyo, mjomba wa Moris, Kassim Shaibu alielezea kusikitishwa na kifo cha mpwaye licha ya kwamba alishapokea taarifa kuwa anajihusisha na vitendo vya wizi.

“Tunasikitishwa na kifo chake kwa sababu alikuwa bado kijana mdogo, lakini siyo mara ya kwanza kusikia kwamba ni mwizi. Bahati mbaya sikuwepo wakati anapigwa, siwezi kusema aliiba nini,” alisema Shaibu.

Naye jirani yake Gerald Solomon alisema Moris alikuwa akionekana mara chache mtaani hapo hasa wakati wa mchana anapokwenda kubadilisha nguo na kwamba, kuna wakati wiki ilimalizika bila kumuona.



Chanzo: mwananchi.co.tz