Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hivi ndivyo mume, mke walivyojiua

51117 Pic+mke

Mon, 8 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tabora. Mume na mke wamejiua mmoja kwa kunywa vidonge vingi na mwingine kwa kujinyonga.

Tukio hilo limetokea jana Jumapili Aprili 7,2019 katika kijiji cha Igombe, wilaya ya Tabora na kuleta huzuni kwa wakazi wa kijiji hicho.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Emmanuel Nley amesema katika tukio hilo, mke ndiye aliyeanza kujiua kwa kunywa idadi kubwa ya vidonge mbalimbali vikiwemo paracetamol na cloxacilin kwa siri.

Amesema chanzo cha kuamua kujiua ni baada ya kuona uchungu wa mtoto wake kuugua kwa muda mrefu na kuteseka kutokana na saratani ya kichwa.

Nley amesema Amina Juma pasipo kumueleza mtu wala mumewe, alichukua vidonge mbalimbali vya kutibu magonjwa akavimeza kisha akafariki dunia.

Amesema polisi walikwenda kuuchukua mwili wa marehemu na muda mfupi baadaye wakapata taarifa ya mumewe Kanuno Tano naye kuwa amejiua kwa kujinyonga.

Ameeleza kuwa mwanaume baada ya kupata taarifa za mkewe kujiua, aliona hawezi kuishi bila mkewe na kwenda kujinyonga kwenye msitu wa hifadhi Gombe kwa kutumia pazia.

Amewataka watu wenye matatizo kutochukua uamuzi wa haraka wanapokuwa na jambo linalowasonga ili kuona namna ya kupatiwa ufumbuzi.

Mmoja wa majirani wa marehemu, Said Maulid amesema walihangaika katika kumtibu mtoto wao ambaye anasema amewapa wakati mgumu.

"Mama wa mtoto kwa kweli alikuwa akimhurumia mwanae namna anavyoteseka na muda mwingi alikuwa akilia," amesema.



Chanzo: mwananchi.co.tz